Kuanza tena meneva ya kijeshi kati ya Uturuki na Misri, sambamba na kupelekewa idadi kubwa ya wanajeshi wa Misri katika Peninsula ya Sinai, kumeutia wasiwasi utawala wa Kizayuni.
Kwa mujibu wa ripoti ya Pars Today, kuanza tena meneva ya pamoja ya kijeshi kati ya Uturuki na Misri baada ya kusimamishwa kwa muda sambamba na kutumwa idadi kubwa ya wanajeshi wa Misri katika Peninsula ya Sinai kumewatia wasiwasi na hofu Wazayuni. Gazeti la Kizayuni la Maariv limeandika kuhusu suala hili kwamba hii ni mara ya kwanza katika muda wa miaka 13 iliyopta ambapo Uturuki na Misri zinaendesha maneva ya pamoja ya kijeshi kati yazo. Hatua hii imesadifiana na hali ya usalama isiyo shwari katika eneo la Mashariki ya Kati na kuwepo wasiwasi kuhusu uwezekano wa kushadidi zaidi hali ya mivutano katika eneo hili. Gazeti hilo la lugha ya Kiebrania limebainisha kuwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Misri na Uturuki unaashiria mabadiliko yanayoweza kutokea katika uhusiano wa kikanda na ushirikiano wa kiusalama. Gazeti la Maariv limeandika kuwa “hatua hii ni sehemu ya juhudi kubwa za Uturuki na Erdogan za kutaka kudhihirisha msimamo wa nchi hiyo kama pande kuu mchezaji katika Mashariki ya Kati baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Assad huko Syria. “Chombo hicho cha habari cha lugha ya Kiebrania kimeendelea kuandika kuwa: Misri pia haina shaka katika kudhihirisha msimamo madhubuti kwa kuzingatia matukio ya kikanda. Nchi hiyo hivi karibuni imetuma wanajeshi katika Peninsula ya Sinai.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Uturuki, maneva ya pamoja ya baharini kati ya Uturuki na Misri kwa jina la Kiarabu Bahr al Sadaqa yaani “Bahari ya Urafiki” yalianza shughuli zake tangu tarehe 22 mwezi huu mashariki mwa Mdediterania na yanamalizika leo Ijumaa.
Brigedia Jenerali Gharib Abdel Hafez, Msemaji wa jeshi la Misri alitangaza katika taarifa kwamba kikosi cha askari jeshi wanamaji wa nchi hiyo wamewasili Uturuki kushiriki katika mazoezi ya pamoja ya jeshi la majini na Uturuki yaliyopewa jina la “Bahari ya Urafiki 2025.” Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi yamefanyika “kwa siku kadhaa mwezi huu Septemba kwa kuvishirikisha vikosi vya jeshi la wanamaji la Misri na la Uturuki.” Menava hayo yanajumuisha kutolewa hotuba mbalimbali na kutekelezwa shughuli za baharini n.k ili kuongeza ujuzi wa askari jeshi wanaoshiriki na hivyo kuimarisha uwezo wao wa kupambana na kutekeleza misheni mbalimbali kwa ufanisi na mafanikio.
Wakati huo huo gazeti la Rai al-Youm limeandika katika dokezo kuhusu sababu na matokeo ya meneva hayo ya pamoja kati ya Misri na Uturuki kwamba nukta ya kuzingatiwa hapa ni miungano iliyoasisiwa baada ya mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Doha. Kufuatia kufichuliwa uungaji mkono wa Marekani kwa Israel katika mashambulizi yake dhidi ya Qatar, si Saudi Arabia pekee iliyogeukia Pakistan yenye silaha za nyuklia ili kuungwa mkono; bali hofu ya ukatili wa Israel dhidi ya eneo hili pia imesababisha kuasisiwa muungano kati ya Misri na Uturuki na kuanza tena mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya baharini kati ya nchi mbili hizo katika Bahari ya Mediterania kwa jina la “Bahari ya Urafiki”. Rai al -Youm limeashiria kuanza tena muungano kati ya Misri na Uturuki baada ya kusita kwa miaka 13 na kuongeza kuwa maneva ya pamoja ya kijeshi ya baharini kwa jina la “Bahari ya Urafiki” yalianza tangu mwaka 2009 katika maji ya Bahari ya Mediterania na kuendelea hadi mwaka 2013 hitilafu zilipotokea kati ya nchi mbili hizo baada ya kuanguka kwa utawala wa Mohammed Morsi na kufuatia uungaji mkono wa Ankara kwa kundi la Ikhwanul Muslimin. Huu ni ujumbe mzito kwa Israel wakati huu, ambayo imeshadidisha matamshi yake dhidi ya Cairo na Ankara, hasa ikizingatiwa kuwa Israel inaamini kuwa nchi zote ni tishio kwa usalama wake. Chombo hicho cha habari kimeongeza kubainisha kuwa: Uturuki na Misri ni mataifa mawili ya Kiislamu yenye nguvu katika Mashariki ya Kati ambayo leo hii yamesimama bega kwa bega; na badala ya kukabliana na kushambuliana kupitia vyombo vya habari, nchi mbili hizi zimeshikamana; na hili kwa hakika linaitia hofu Israel.

Inaonekana kuwa Israel inatiwa hofu na ina wasiwasi na maneva ya pamoja ya kijeshi kati ya Misri na Uturuki kwa sababu kadhaa za kimkakati na kiusalama.
Sababu ya kwanza: Ina wasiwasi na kuimarishwa ushirikiano wa kijeshi wa kikanda: Uturuki na Misri ni nchi mbili muhimu na zenye nguvu katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Sababu ya Pili: Kuimarishwa uhusiano kati ya Misri na Uturuki: Baada ya miaka mingi ya mvutano wa kidiplomasia kati ya Misri na Uturuki, ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili unaweza kupelekea kuimaria uhusiano kati ya pande mbili na hivyo kuwa changamoto mpya kwa Israel.
Sababu ya Tatu: Uwezo mpya wa kijeshi: Uturuki na Misri zote zina wanajeshi wenye nguvu.
Nne: Michuano ya kijiopolitiki: Israel ina wasiwasi kwamba kuimarisha ushirikiano wa kijeshi kati ya Misri na Uturuki kutapelekea kushudhudiwa mabadiliko ya kijiografia katika eneo ambayo yanaweza kuwa tishio kwa nafasi ya kimkakati ya Israel.
Na Tano: Wasiwasi wa kiusalama na vitisho vya moja kwamoja: Uturuki na Misri hivi sasa zina uhusiano uliojaa mivutano na Israel. Kama wanavyodai Wazayuni wenyewe, ushirikiano wowote mpya wa kijeshi kati ya Cairo na Ankara unaweza kuibua vitisho vya moja kwa moja dhidi ya Israel khususan katika maeneo kama Syria, Gaza au hata katika mipaka ya baharini.