Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Patrick Muirhead
- Nafasi, BBC
Kisiwa kidogo, katika Bahari ya Hindi kimekuwa uwanja wa vita vya kisiasa katika uchaguzi wa wikiendi hii huko Ushelisheli.
Kisiwa cha Assumption, kilicho magharibi mwa Bahari ya Hindi – hakina vitu vingi vilivyotengenezwa, kina joto jingi, ukubwa wake ni kama Uwanja wa Ndege wa Heathrow wa London.
Kisiwa hiki cha tropiki – kilicho mbali kijiografia, na wala sio kisiwa cha paradiso – ni mahali pa nguvu za kijiografia na wanaharakati wa mazingira, pamoja na ushindani wa kisiasa huko Ushelisheli.
Kiko umbali wa kilomita 1,140 (maili 700) kutoka kisiwa kikuu chenye watu wengi zaidi cha Ushelisheli, Mahé kinachovutia watalii.
Kisiwa hiki kiko karibu na Njia ya Hariri ya karne hii – njia ya meli zenye shughuli nyingi za kibiashara zinazobeba bidhaa na nyenzo za viwandani kutoka Asia Mashariki hadi Afrika na kwingineko. India ilikuwa na nia ya kujenga kituo cha kijeshi kwenye kisiwa cha Assumption lakini ilikataliwa.
Jamhuri hiyo ndogo inapoingia kwenye kura za urais na ubunge, kisiwa hiki ni sehemu kuu ya uchaguzi.
“Chini ya urais wangu, hakutakuwa na kambi ya kijeshi ya nchi za kigeni Ushelisheli,” Rais Wavel Ramkalawan aliambia BBC News. “Hatupendezwi na siasa za aina hiyo.”
Kwa hivyo kukikodisha Kisiwa chote cha Assumption, au sehemu ya kisiwa, kwa familia ya kifalme ya Qatari kumeleta mjadala. Kupitia kampuni ya uwekezaji ya Mashariki ya Kati, Assets Group, Qatar inajenga hoteli ya kifahari huko, na uwanja wa ndege wenye uwezo wa kupokea ndege ndogo.
“Assumption ina mojawapo ya fukwe ndefu zaidi nchini Shelisheli, ambayo pengine ni mojawapo ya fukwe muhimu zaidi kwa kasa wa kijani katika nchi yetu,” anasema mwanaharakati wa mazingira Lucie Harter.
Kisiwa cha Assumption ndio lango la kuelekea kwenye kisiwa cha Aldabra kilichoorodheshwa na Unesco katika urithi wa dunia, kiko kilomita 27 tu (maili 17) kuelekea kaskazini.
Aldabra ni nyumbani kwa spishi 400 ambazo hazipatikani mahali pengine popote kwenye sayari. Sir David Attenborough aliielezea kama “hazina kubwa ya asili ulimwenguni.”
Rais wa Sasa

“Tumeona picha ya ganda la kobe ambalo limevunjwa na mitambo ya ujenzi,” asema Bi Harter. “Uangalizi uko wapi? Hakuna uwazi. Maamuzi yanafanyika kwa siri.”
Notisi ya kusitisha ujenzi, iliyotolewa na mamlaka ya mipango mwezi Mei mwaka huu, inaonekana kupuuzwa. Kazi ya ujenzi inaendelea.
Wiki iliyopita, vikundi viwili vya mazingira, Friends of Aldabra na Seychelles at Heart, vilifungua kesi dhidi ya serikali katika Mahakama ya Kikatiba ya nchi hiyo kusitisha mradi huo, ili kusubiri uchunguzi kamili na wa huru, juu ya athari za mazingira na kuhakikisha kwamba waangalizi wa kimataifa watahakikisha mazingira asili yanalindwa.
Ramkalawan, kasisi wa Kianglikana ndiye alitia saini mkataba huo na Qatar mwaka jana. Ushelisheli ina wakazi zaidi ya 120,000, na ukodishaji wa Assumption, unahusisha ukaaji wa Qatar kwa miaka 70 na malipo ya chini ya dola milioni 20 (£15m).
“Kwani hoteli hiyo ina tatizo gani?” anauliza. “Tuna hoteli za Hilton. Qatar italeta kampuni ya kifahari ya Rosewood ili kuendesha hoteli hiyo. Inabidi tutafute wawekezaji ili tuweze kuendelea kuishi,” anasema Ramkalawan.
Mhubiri huyo na chama chake, Linyon Demokratik Seselwa (LDS), alishinda urais miaka mitano iliyopita kwa kampeni za kupambana na ufisadi, akichukua madaraka katikati ya janga la Covid 19.
Covid-19 iliondoa watalii katika hoteli na nyumba za wageni za Seychelles, baada ya muda mfupi, iliathiri hazina ya umma. Hata hivyo licha ya juhudi zake za kurudisha uchumi wa Ushelisheli, umaarufu wake unazidi kupungua.
Ulinzi wa kisiwa cha Assumption unaonekana kuwa muhimu zaidi kwa wapiga kura wengi kuliko uwekezaji wa kiuchumi.
Nchi hiyo ina deni la wastani la taifa na Pato la Taifa la 58%. Kiwango cha chini cha ukosefu wa ajira ni 3.5%. Na matarajio ya uchumi kukuwa kwa asilimia 5.8 kwa mujibu wa IMF.
Mpinzani Mkuu
Chanzo cha picha, ALDABRA
Hesabu zinaweza kusema uwongo, anasisitiza mpinzani mkuu wa Ramkalawan katika kiti cha urais, Dk Patrick Herminie, kiongozi wa chama cha upinzani cha United Shelisheli (US).
“Tuna shaka sana juu ya viwango hivyo vyote,” anasema. “Tunazidi kuwa maskini. Watu hawawezi kumudu milo miwili kwa siku. Ukadiriaji huu unatokana na takwimu zilizotolewa na serikali hii. Na serikali hii inajulikana kwa kupika takwimu.”
Serikali imekanusha kupikwa takwimu.
Wengi wanafikiri mzozo juu ya kisiwa cha Assumption unaweza kumsaidia Dk Herminie kuingia madarakani, huku akifanya kampeni za kusafisha siasa na kuondoa ufisadi katika utawala wa umma.
Anaambia BBC kukamatwa kwake miaka miwili iliyopita kwa tuhuma za kutumia uchawi kujinufaisha kisiasa “kulimshtua.” “Nilishangaa zaidi kwamba rais kweli aliamini mapinduzi ya kijeshi yanaweza kufanywa kwa uchawi. Walikuja hapa kutafuta miili ya watu waliokufa na mifupa.”
Chama chake pia kimeahidi kupunguza umri wa kustaafu hadi miaka 63, kupunguza nauli ya mabasi ya kisiwa kwa 40% na kuongeza faida za hifadhi ya jamii.
Herminie ameahidi, hakutakuwa na kurudi kwenye maisha ya giza ya Ushelisheli ambayo ni pamoja na mauaji, watu kufurushwa na kutoweka kwa wapinzani wa kisiasa.
Wagombea wengine

Kutoka wagombea 11 – kwa sasa wamebaki wagombea wanane kwenye kinyang’anyiro hicho. Duru ya pili ya uchaguzi inaweza kutokea ikiwa upigaji kura wa awali hautatoa mshindi wa moja kwa moja. Wapiga kura pia watachagua wajumbe wa Bunge lao la viti 26.
Mmiliki wa gazeti la Firebrand na mgombea binafsi wa urais Ralph Volcere ametumia gazeti lake la kila wiki kumshutumu kasisi-rais kama mtawala dikteta – na tangu wakati huo limezuiwa kushiriki mikutano ya rais na wana habari Ikulu.
“Kila mradi, kila sekta, ufisadi upo,” anasema Volcere.
“Nilichokuwa nikipigania ni haki,” anasema. “Huwezi kukwepa mchakato wa kisheria. Haijalishi wewe ni nani.”
Hata hivyo, Volcere mwenyewe amekashifiwa kwa kumtemtea Mukesh Valabhji – mfanyabiashara tajiri wa Ushelisheli na mshauri wa zamani wa marehemu Rais René – mwenye kesi ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.
Pia anasubiri kesi ya pili ya mashtaka ya rushwa, pamoja na aliyekuwa Mke wa rais Sarah René na wengine. Valabhji anatuhumiwa kwa kujipatia mamilioni ya dola – pesa taslimu zilizotolewa na Imarati. Anakanusha kosa lolote.
Kubwa kati ya sera za Volcere ni kulalalisha bangi, jambo hilo anaamini litawafanya wafanyabiashara wa dawa za kulevya wa Ushelisheli kuachana na Biashara hiyo na kupunguza idadi kubwa ya watu wenye umri wa kufanya kazi ambao wameathirika na dawa za kulevya – kwa sasa wanafikia 10%, kulingana na data rasmi ya serikali.
Sehemu kubwa ya heroini inayotua kwenye visiwa hivi hupatikana kwenye njia za meli zinazopita karibu na Kisiwa cha Assumption. Hakuna mtu amepata njia ya kuizuia.
“Kinachokosekana kwa muda mrefu sana,” anasema Volcere, “ni utawala bora, uwazi na uwajibikaji.”