
Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) na waangalizi wa kikanda na kimataifa wamesifu uchaguzi wa rais wa Septemba 16 nchini humo na kusema kuwa ulikuwa huru na wa haki.
Mwenyekiti wa MEC, Annabel Mtalimanja alisema Jumatano usiku kabla ya kutangaza matokeo ya mwisho kwamba tume hiyo imefuatilia kwa makini mchakato mzima wa uchaguzi kwa misingi ya sheria inayosimamia uchaguzi nchini Malawi. Alisema: Tathmini ya Tume, kwa hiyo, ni kwamba uchaguzi huu wa rais ulikuwa huru na wa haki,” .
Hata hatua ya Rais Lazarus Chakwera kukubali kushindwa kwenye uchaguzi huo imepongezwa sana. Ahadi yake ya kuiunga mkono serikali mpya ya Mutharika imepongezwa pia na waangalizi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Kabla ya hapo pia Umoja wa Afrika AU nao ulikuwa tayari umeipongeza Tume ya Uchaguzi ya Malawi kwa kusimamia na kuendesha uchaguzi huru na wa haki pamoja na kupevuka kisiasa kulioneshwa na Rais Chakwera na kukubali kushindwa kwenye uchaguzi huo.
Mtalimanja imesema: “Matokeo haya ya uchaguzi ni taswira ya kweli ya mapenzi ya watu wa Malawi kama inavyotarajiwa chini ya Kifungu cha 12 cha Katiba ya Jamhuri ya Malawi.”
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi alitangaza Jumatano usiku kuwa Rais wa zamani Peter Mutharika, aliyegombea kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, ameshinda urais kwa karibu kura milioni 3.04, sawa na asilimia 56.8 ya kura halali zilizopigwa — na kuvuka kiwango cha asilimia 50 ongeza 1 kinachohitajika kwa ushindi wa moja kwa moja. Rais wa sasa Lazarus Chakwera wa Chama cha Malawi Congress alipata takriban kura milioni 1.77, ikiwa ni asilimia 33.
Saa chache kabla ya matokeo kutangazwa, Chakwera, mwenye umri wa miaka 70, alihutubia taifa kwa njia ya televisheni na kukubali kushindwa — kitendo ambacho kinaelezwa kuwa ni ishara ya ukomavu wa kidemokrasia katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.