
Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa Iran iko tayari kikamilifu kwa hali yoyote endapo nchi za Ulaya zitaendelea na hatua ya kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa kupitia kile kinachoitwa utaratibu wa snapback, na ameonya kwamba mazungumzo ya kidiplomasia yatakuwa hayana maana chini ya vikwazo vilivyorejeshwa.
Akiwa katika mkutano na mwenzake wa Bolivia, Luis Arce Catacora, pembezoni mwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Alhamisi, Rais Pezeshkian alisema Iran inatumai kuwa utaratibu wa snapback hautatekelezwa.
Tarehe 28 Agosti, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kama wahusika wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 (JCPOA), waliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba wamameanzish kile kinachoitwa utaratibu wa snapback — mchakato wa siku 30 wa kurejesha vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, wakidai kutokufuata kwa Iran masharti ya makubaliano hayo.
Hatua hiyo ilifuatia kura iliyopigwa Ijumaa iliyopita ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikataa azimio ambalo lingeliondoa kabisa vikwazo dhidi ya Iranvinavyohusiana na nyuklia. Iwapo kama makubaliano mapya hayatapatikana, vikwazo vitarejeshwa kiotomatiki ifikapo Septemba 28.
Rais Pezeshkian ameashiria sera za upande mmoja za Marekani, akibainisha kuwa mbinu kama hizo hazilengi tu Iran bali pia nchi zote zinazokataa kufuata ajenda za Marekani.
Ameongeza kuwa: “Katika mazingira haya, nchi zinazotafuta uhuru lazima ziongeze uwezo wao wa kisayansi na kiteknolojia ili kulinda kwa nguvu mamlaka na maslahi yao ya kitaifa.”
Rais wa Iran pia alionya kwamba hatua yoyote ya kurejesha vikwazo itafanya mazungumzo kukosa maana. “Mazungumzo ya kidiplomasia hayataweza kuwa na maana kama nchi tatu za Ulaya zitarejesha vikwazo dhidi ya Tehran,” alisema.
Katika sehemu nyingine ya maelezo yake, rais wa Iran alitoa shukrani kwa ushirikiano wa Bolivia na Iran katika vipindi mbalimbali na akabainisha kuwa maendeleo ya baadaye ya uhusiano kati ya Tehran na La Paz yanategemea dhamira ya pamoja ya viongozi wakuu wa mataifa yote mawili.
Kwa upande wake, rais wa Bolivia alieleza sera za uchokozi wa Marekani, hasa katika ukanda wa Karibiani, kuwa tishio kwa amani na usalama wa kimataifa.
Alisifu uwepo “chanya na amilifu” wa Iran katika Amerika ya Kusini na kutangaza matakwa ya nchi yake ya kudumisha na kuimarisha uhusiano wa kirafiki na kupanua ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali.