Waziri Mkuu wa Sudan, Kamil Idris, siku ya Alhamisi ameitaka jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kulitambua kundi la waasi la RSF nchini humo kama “kundi la kigaidi.”

Akiwa anahutubia kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Idris aliitaka jumuiya ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kusitisha mtiririko wa silaha na wapiganaji wa kulipiwa kuingia Sudan.

Alisema “watu wa Sudan wamekabili vitisho na hatari za uwepo wao kwa sababu ya RSF, kundi  ambalo limechukua sera ya kuwatisha raia.”

Idris alisema taifa lake linakabili “changamoto na hatari kubwa zinazotikisa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na mfumo wa pande nyingi, zikihatarisha uthabiti wa kikanda na kimataifa, huku misingi ya sheria za kimataifa ikidhoofika, na uhalifu wa mauaji ya kimbari, uchokozi na matumizi ya wapiganaji wa kigeni kuvamia ardhi za mataifa na kuua wananchi wao ukiongezeka.”

Tangu Aprili 2023, jeshi la Sudan limekuwa likikabiliana na kundi la RSF ambalo limekuwa lilipigana kunyakua madaraka nchini humo. Vita hivyo vya ndani vimesababisha maelfu ya vifo na mamilioni kukimbia makazi yao.

Idris pia alitaka kuondolewa mara moja kwa mzingiro wa mji waasi wa RSF dhidi ya mji  wa El-Fasher jimboni Darfur kwani tayari Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshawataka waasi huo kusitisha mzingiro huo..

Alikemea kuendelea kwa ukimya wa kimataifa kuhusu mzingiro huo na mashambulizi ya mabomu kwenye kambi za wakimbizi wa ndani, misikiti, na vituo vya afya na huduma katika maeneo mbalimbali nchini humo.

El-Fasher imeshuhudia mapigano makali kati ya jeshi la Sudan na waasi wa RSF tangu Mei 2024, licha ya maonyo ya kimataifa kuhusu hatari ya vurugu katika mji huo ambao ni kituo kikuu cha kibinadamu kwa majimbo matano ya Darfur.

Idris pia aligusia hali ya maafa katika Ukanda wa Gaza na kusema: “Hakutakuwa na uthabiti wala usalama katika eneo bila suluhisho kamili na la kudumu kwa suala la Palestina, litakalowezesha kuanzishwa kwa dola ya Kipalestina yenye mji mkuu wake huko Al Quds (Jerusalem).

Idris alikemea shambulio la hivi karibuni la Israel dhidi ya uongozi wa Hamas mjini Doha, Qatar, akisema linahatarisha amani na usalama wa kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *