Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia zimesaini mkataba wa dola bilioni 25 kwa ajili ya kujenga mitambo minne ya nishati ya nyuklia, kama sehemu ya makubaliano ya muda mrefu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tehran na Moscow katika nyanja mbalimbali.

Mkataba huo wa utekelezaji ulitiwa saini mjini Moscow, Ijumaa, kati ya Kampuni ya Iran Hormoz na Kampuni ya Rosatom ya Russia, kwa ajili ya ujenzi na kuzinduliwa vituo vinne vya kizazi cha tatu vya kuzalisha umeme wa nyuklia katika mji wa pwani wa Sirik, ulioko katika mkoa wa kusini wa Hormozgan.

Nasser Mansour Shariflou, akiwakilisha Kampuni ya Iran Hormoz kwa niaba ya Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), na Dmitry Shiganov, akiwakilisha Kampuni ya REP, tawi la Shirika la  la Rosatom, walisaini mkataba huo wa thamani ya dola bilioni 25 mbele ya balozi wa Iran nchini Russia, Kazem Jalali.

Mradi huu mkubwa, ambao utatekelezwa katika wilaya ya Kuhestak, eneo la Sirik, mkoa wa Hormozgan, kwenye eneo lenye ukubwa wa hekta 500, utakuwa na uwezo wa kuzalisha jumla ya megawati 5,020 za umeme wa nyuklia.

Wakati wa hafla ya utiaji saini, ilitangazwa kuwa makubaliano haya kati ya nchi hizi mbili rafiki  kwa lengo la kuendeleza ushirikiano wa pamoja katika matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia.

Ripoti zimesema kuwa tafiti za kuchagua eneo zimemalizika, na tafiti za kihandisi na kimazingira pamoja zimekamilika.

Kwa mujibu wa makubaliano ya kiserikali kati ya mataifa haya mawili, Russia imepewa kandarasi ya kujenga mitambo minane ya nyuklia nchini Iran, ikiwemo minne katika eneo la Bushehr.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, Mohammad Eslami, awali alitangaza kuanza kwa mradi huu baada ya mkutano na Mkurugenzi Mkuu wa Rosatom, Alexey Likhachev, mjini Moscow, Jumatano, akisisitiza ushirikiano wa kimkakati kati ya Tehran na Moscow katika kuendeleza sekta ya nishati ya nyuklia.

Akitaja mpango wa Iran wa kuzalisha megawati 20,000 za umeme kupitia mitambo ya nishati ya nyuklia, Eslami aliwaambia waandishi wa habari kwamba ujenzi wa awamu ya pili na ya tatu ya mtambo wa nyuklia wa Bushehr unaendelea kwa sasa kwa ushirikiano na Russia

Eslami alisisitiza kuwa mradi huu ni kipaumbele kwa Tehran na Moscow, akiongeza kuwa msisitizo wa marais wa nchi hizi mbili umekuja kuongeza kasi ya utekelezaji wake, na mazungumzo yanayoendelea yatasaidia kurahisisha na kuendeleza jitihada hizi za pamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *