Nchi tatu za Kiafrika zimetangaza kuwa zimehitimisha unachama wao katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Kwa mujibu wa ripoti ya Pars Today, nchi tatu za Kiafrika yaani Burkina Faso, Mali na Niger za magharibi mwa Afrika katika eneo la Sahel zimetoa taarifa ya pamoja na kutangaza kujitoa haraka iwezekanavyo katika mahakama ya ICC yenye makao yake huko Hague nchini Uholanzi. Nchi hizo zimesisitiza kuwa haziitambui rasmi taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa. Viongozi wa nchi hizo tatu wamesisitiza kuwa: Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imeonyesha kuwa haina uwezo wa kufuatilia na kushughulikia jinai za kivita zilizothibitishwa, jinai dhidi ya binadamu, jinai za mauaji ya kimbari na uvamizi. 

Moja ya sababu zilizopelekea Burkina Faso, Mali na Niger kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ni kushindwa kwa taasisi hiyo kuchunguza jinai za Israel dhidi ya Wapalestina. Nchi hizo zinaamini kuwa ICC imechukua hatua na kushughulikia kesi zinazohusu nchi dhaifu hususan nchi za Kiafrika huku ikishindwa kuchukua hatua zozote dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni na mauaji ya kimbari yanayoendelea hivi sasa katika Ukanda wa Gaza. 

Mauaji ya kimbari ya Israel Ukanda wa Gaza

Kushindwa kushtakiwa kesi za jinai za kivita za Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai huku nchi nyingi za Kiafrika zikifunguliwa mashitaka na mahakama hiyo, kumezifanya nchi hizo kuhisi kwamba kwa hakika ICC inafanya kazi kwa kuyapendelea madola ya Magharibi na tawala zinazopewa himaya na kuungwa mkono kimataifa. Kwa hakika, ,Burkina Faso, Mali na Niger zinaona kuwa taasisi hiyo imeshindwa kutekeleza wajibu wake wa msingi ambao ni kufuatilia kisheria na kutenda haki kwa nchi na mataifa yote duniani. 

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliundwa mwaka 2002 kwa lengo la kufuatilia kisheria mauaji ya kimbari, jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita; na hadi sasa takriban kesi 33 zimesikilizwa katika mahakama hiyo, nyingi zikiwa zinahusiana na nchi za Afrika. Mwenendo huu umezifanya nchi za Kiafrika kuhisi kuwa taasisi hiyo inataka tu kuwafungulia mashitaka watu wanaotoka katika nchi dhaifu zaidi, hasa za Kiafrika, huku mataifa makubwa hasa ya Magharibi yakifadika na kinga wanayopewa na hivyo kutochukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mahakama ya ICC 

Tathmini hii imezipelekea nchi nyingi barani Afrika kutokuwa na imani na utendaji kazi wa Mahakama ya ICC na kuihesabu mahakama hiyo kama wenzo cha kuendeleza udhibiti wa mabavu na mashinikizo kwa nchi za Kiafrika. 

Katika upande mwingine, aghalabu ya nchi za Kiafrika zinaamini kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kivitendo imekuwa wenzo wa kisiasa wa nchi za Magharibi na si taasisi huru ya kutenda haki.

Katika uwanja huu, hatua ya nchi tatu za Magharibi mwa Afrika ya kutangaza kujitoa ICC inaweza kutafsiriwa kama sehemu ya harakati kubwa zaidi ya kukabiliana na Ukoloni Mamboleo na kukiuka kujitawala kwa nchi mbalimbali. Hasa kwa kuwa nchi za Burkina Faso, Mali, na Niger zimetangaza kuwa, badala ya kutegemea taasisi za kimataifa, zinataraji kuchukua maamuzi ya kuanzisha mifumo yao ya ndani na ya kieneo ili kufuatilia utendaji haki na kutatua migogoro mbalimbali.  

Nchi hizo zinaamini kuwa ni kwa kutegemea tu njia za ufumbuzi za ndani na ushirikiano wa kikanda ndipo zitakapoweza kukabiliana na matatizo yao ipasavyo na kuacha kuzitegemea taasisi  za nje ambazo kivitendo hazijakuwa na mchango athirifu na matokeo chanya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *