Picha ya bendera

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, Mwandishi BBC Swahili

Wiki hii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilifunguliwa rasmi jijini New York, likiwakutanisha wakuu wa nchi na wanadiplomasia kutoka mataifa 193 wanachama, pamoja na mataifa mawili yenye hadhi ya waangalizi.

Hata hivyo, licha ya dhamira ya Umoja wa Mataifa kuwa ya kimataifa, baadhi ya mataifa hayatakuwa na uwakilishi rasmi kwenye mkutano huo wa kila mwaka.

Tofauti na waangalizi wasio na haki ya kupiga kura kama Vatikani (Holy See) na Jimbo la Palestina, kuna mataifa kadhaa ambayo hayatakuwapo kabisa kwa namna yoyote ya kiuwakilishi rasmi.

Katika kuangalia ni nchi gani si wanachama wa UN, ni muhimu kufafanua tunamaanisha nini kwa taifa kuitwa nchi.

Kuna maeneo mengi ambayo yangependa kuwa nchi na kutambuliwa kama hivyo.

Sealand na Liberland zinakuja akilini.

Wanatamani kuwa nchi lakini sio uwezekano wa kutembelea au kuishi huko.

Katika hali nyingine kuna nchi ambazo hapo awali zilikuwepo kwa kujitegemea kama vile Scotland na Catalonia.

Wamechukuliwa na nchi kubwa, jirani. Ingawa inawezekana kutembelea na kuishi huko sio mataifa huru tena.

Tunachovutiwa nacho hapa ni nchi zinazofanya kazi kama nchi za ukweli.

Nchi ambazo tunaweza kutembelea au kuishi lakini si wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kila nchi kubwa na karibu kila nchi ndogo ni mwanachama wa UN.

Hata majimbo madogo kama Monaco na San Marino ni wanachama wa UN.

Kwa ujumla, tunapoangalia ni nchi gani si wanachama wa UN ni lazima tuangalie nchi ambazo zina migogoro ya aina fulani na majirani zao au nchi ambazo zimejitangazia uhuru lakini bado hazijatambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Haya ni mataifa ambayo, licha ya kutotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa, mara nyingi huwa na ushawishi mkubwa kimataifa kuliko inavyotarajiwa.

1. Taiwan (Jamhuri ya China)

Watu wengi wa Taiwan wanaona kisiwa chao kama taifa tofauti

Chanzo cha picha, AFP

Taiwan, inayojulikana rasmi kama Jamhuri ya China, inatambuliwa na mataifa 21 wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na Vatikani kuwa ni serikali halali ya China.

Ni mrithi wa serikali ya kikatiba ya China iliyoundwa mwaka 1912, kabla ya kufurushwa na wanamapinduzi wa Kikomunisti wa Mao Zedong na kulazimika kuhamia Taiwan.

Kwa upande wa China, Taiwan huchukuliwa kama jimbo lililoasi ambalo linapaswa kurejeshwa chini ya mamlaka ya Beijing kwa nguvu za kijeshi iwapo itahitajika.

Hadi mwaka 1971, Taiwan ilikuwa inawakilishwa katika Umoja wa Mataifa kama serikali rasmi ya China na ilikuwa na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama.

Mwaka huo, Umoja wa Mataifa ulitoa uanachama wa Taiwan na kukabidhi kiti chake kwa Jamhuri ya Watu wa China (PRC), na tangu hapo Taiwan haijapata nafasi tena katika taasisi yoyote ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa.

2. Jamhuri ya Somaliland

Wakati wa kampeini za Somaliland

Chanzo cha picha, AHMED KADLEYE

Somaliland ni eneo lililojitangaza kuwa taifa huru, liko kaskazini mwa Somalia, kandokando ya Bahari Nyekundu.

Likiwa koloni la zamani la Uingereza, Somaliland ilipata uhuru wake mnamo tarehe 26 Juni 1960, lakini siku chache baadaye tarehe 1 Julai liliungana na sehemu ya kusini ya Somalia (iliyokuwa koloni la Italia) kuunda Jamhuri ya Somalia.

Baadaye, Somaliland ilijutia uamuzi huo, hasa baada ya Somalia kuporomoka kisiasa mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Mwaka 1991, baada ya kuanguka kwa serikali ya kati ya Somalia, Somaliland ilifanya kura ya maoni na kujitangaza rasmi kuwa huru.

Leo, Somaliland ina sifa nyingi za taifa: uchaguzi huru, serikali inayofanya kazi, na utawala wa sheria.

Hata hivyo, hakuna nchi inayotambua rasmi uhuru wake kwa hofu ya kuvuruga juhudi za amani Somalia.

Licha ya hayo, majirani kama Djibouti na Ethiopia huruhusu raia wa Somaliland kuvuka mipaka kwa kutumia pasipoti ya Somaliland.

3. Jamhuri ya Nagorno-Karabakh (NKR)

Takriban watu milioni moja walihamishwa na vita mwanzoni mwa miaka ya 1990

Chanzo cha picha, Getty Images

Nagorno-Karabakh ni jamhuri iliyojitenga katika eneo la Kusini mwa Caucasus, ambayo kimataifa inatambuliwa kuwa sehemu ya Azerbaijan.

Licha ya hivyo, idadi kubwa ya wakaazi wake ni wa kabila la Kiarmenia, na eneo hilo huungwa mkono na Armenia.

Mgogoro huu ni miongoni mwa migogoro iliyo “shindikana”, ambapo hakuna maendeleo makubwa tangu kusitishwa kwa vita mwaka 1994.

Mwezi Agosti, Rais wa Azerbaijan alitoa matamshi makali katika mitandao ya kijamii, karibu na kutangaza vita dhidi ya Armenia.

NKR inatambuliwa tu na jamhuri nyingine tatu zilizojitenga kutoka kwa iliyokuwa Muungano wa Kisovieti: Abkhazia, Ossetia ya Kusini, na Transnistria (PMR) zote zikiwa na uhusiano wa karibu na Urusi.

4. Transnistria (Jamhuri ya Moldova ya Pridnestrovian – PMR)

Kusherehekea taifa ambalo halipo

Chanzo cha picha, Loop Images/Getty Images

Mnamo tarehe 22 mwezi Septemba mwaka 2025 Rais wa Moldova Maia Sandu ameonya kuwa uhuru wa nchi yake na mustakabali wa Ulaya uko hatarini baada ya polisi kuwakamata makumi ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na njama ya kuchochea ghasia zinazodaiwa kuungwa mkono na Urusi.

Transnistria ni eneo lililojitenga mashariki mwa Moldova, karibu na mpaka wa Ukraine.

Baada ya kusambaratika kwa Umoja wa Kisovieti, eneo hili lilitangaza uhuru wake na kusababisha mapigano mafupi ya kijeshi.

Kwa sasa, linaendesha serikali yake, lina jeshi na hata fedha yake, huku likiwa na wanajeshi wa Urusi wanaojulikana kama “walinda amani”.

Hata hivyo, Urusi yenyewe haijalitambua rasmi kama taifa huru.

Mwaka huu, Transnistria ilitangaza nia ya kufanya kura ya maoni kama ile ya Crimea, ili kujiunga na Urusi licha ya kutopakana nayo moja kwa moja.

Inatambuliwa tu na Abkhazia, Ossetia ya Kusini, na Nagorno-Karabakh.

5. Jamhuri ya Kosovo

Kosovo ilitangaza uhuru wake kutoka Serbia mwaka 2008

Kosovo ilitangaza uhuru wake mwaka 2008, licha ya upinzani mkali kutoka kwa Serbia, ambayo bado inadai kuwa Kosovo ni sehemu ya ardhi yake ya kitaifa.

Tangu wakati huo, Kosovo imetambuliwa na zaidi ya mataifa 100 ya Umoja wa Mataifa pamoja na Taiwan, yakiwemo Marekani na nchi nyingi za Ulaya.

Hata hivyo, haijapata uanachama wa Umoja wa Mataifa kutokana na pingamizi kutoka kwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama.

Nchi tano za Umoja wa Ulaya bado hazijaitambua Kosovo ni kama vile Cyprus, Ugiriki, Romania, Slovakia, na Hispania.

6. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahara (SADR)

Brahim Ghali, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (SADR) alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa William Ruto huko Kasarani.2022

Chanzo cha picha, State House Kenya

Ilitangaza uhuru mwaka 1976, na kutambuliwa na mataifa 84 wakati fulani, pamoja na Ossetia ya Kusini.

Hata hivyo, mataifa 39 baadaye yaliondoa utambuzi wao kutokana na shinikizo kutoka Morocco.

SADR ni mwanachama wa Umoja wa Afrika, jambo ambalo liliwahi kusababisha Morocco kujiondoa kwa muda kutoka katika umoja huo.

7. Palestina

gg

Chanzo cha picha, Getty Images

Palestina – ina hadhi ya mwangalizi katika Umoja wa Mataifa, lakini uanachama kamili huzuiliwa na Baraza la Usalama.

Mataifa ya magharibi yameingia kwa mkondo na kuapa kutambua Palestina kama taifa huru.

Uingereza na Ufaransa wamekuja juzi wakiwa wamechelewa.

Kati ya nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa, 144 wamelitambua taifa la Palestina ikiwemo Norway, Hispania na Ireland waliofanya hivyo mwaka jana.

Baada ya Uingereza kuifuata Ufaransa, na hivi punde Canada kuna imani kwamba nchi nyeingine za Ulaya, na Australia zitafuata pia katika kulitambua taifa la Palestina.

Makundi ya mataifa yasiyotambuliwa kikamilifu

Nchi ambazo hazitambuliwi kikamilifu na Umoja wa Mataifa kwa ujumla ziko katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni mataifa yanayotambuliwa kwa sehemu ambayo yametambuliwa na baadhi ya wanachama wa Umoja wa Mataifa lakini si wote.

Kundi la pili ni mataifa ambayo yana majimbo ya ukweli ambayo yanafanya kazi kwa uhuru lakini hayajatambuliwa kote kidiplomasia, hata kutoka kwa wakazi wao wenyewe.

1. Mataifa yanayotambuliwa kwa Sehemu au baadhi ya wanachama wa Umoja wa mataifa (Partially Recognized States):

  • Kosovo – imetambuliwa na mataifa mengi, lakini si yote, hasa kutokana na mvutano na Serbia.
  • SADR – inadai Sahara Magharibi, lakini haijatambuliwa na Umoja wa Mataifa.

2. Mataifa halisi (De Facto States)

  • Taiwan (Jamhuri ya China) – ina serikali inayofanya kazi, lakini Umoja wa Mataifa hutambua Jamhuri ya Watu wa China.
  • Cyprus ya Kaskazini – inatambuliwa tu na Uturuki.
  • Abkhazia na Ossetia ya Kusini – maeneo yaliyotangaza uhuru kutoka Georgia, lakini bila utambuzi mpana kimataifa.

Kwanini kutambuliwa kama taifa ni muhimu?

Mkutano wa Umoja wa Mataifa unaendelea mjini New York

Chanzo cha picha, Getty Images

Kutotambuliwa rasmi kunaweza kuzuia taifa kushiriki katika mashirika ya kimataifa, kushiriki mazungumzo ya kidiplomasia, au kufanya mikataba ya kibiashara.

Mataifa yasiyotambuliwa yanakosa fursa ya kutetea maslahi yao katika jukwaa la dunia.

Mpango wa Umoja wa mataifa: Ulivyoanza na unavyoendelea

Mnamo mwaka 1945, mataifa yalikuwa magofu.

Vita vya pili vya dunia vilikwisha na ulimwengu ulihitaji amani.

Mataifa 51 yalikusanyika huko San Francisco mwaka 1945 kutia saini hati ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa

Hati hii ilikuwa ni mkataba, ukiunda shirika jipya ambalo si jingine bali ni Umoja wa Mataifa.

Miaka 70 baadaye, Umoja wa Mataifa unadumisha amani na usalama wa kimataifa.

Hata hivyo hilo limekosolewa vikali na Rais wa Marekani Donald Trump anayeonekana kukerwa na mustakabali wa Umoja wa Mataifa.

Rais wa Marekani Donald Trump ameukosoa vikali Umoja wa Mataifa wakati akihutubia mkutano wa umoja huo unaendelea jijini New York, Marekani.

Amesema kuna mambo mawili pekee ambayo ameyapata kutoka umoja huo – kuongeza mivutano na teleprompter iliyovunjika.

Rais wa Marekani anasema Umoja wa Mataifa “haukuwepo kwa ajili yetu” wakati wa mazungumzo ya kumaliza vita ambavyo anasema “amevitatua”.

Amehoji “Ni nini madhumuni ya Umoja wa Mataifa?” “Umoja wa Mataifa haujawahi kuishi kulingana na uwezo wake… ni maneno matupu, na maneno matupu hayatatui vita,” amesema Trump.

Trump ametaja vita saba anavyodai kuvimalizika wakati wa muhula wake wa pili hadi sasa, na kusema kuwa “watu walimwambia kuwa migogoro hii haiwezekani kumalizwa.”

Ameorodhesha migogoro kati ya Cambodia na Thailand; Kosovo na Serbia; Pakistan na India; Israel na Iran; Misri na Ethiopia; Armenia na Azerbaijan na mvutano kati ya DR Congo na Rwanda. Hakuna rais mwingine “amewahi kufanya chochote karibu na hilo,” anasema.

Anasema Umoja wa Mataifa “haukujaribu kutatua mzozo wowote kati ya hiyo.” Viongozi wa dunia wanakutana mjini New York wiki hii kwa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *