Katika hatua inayoonekana kama kuunga mkono wazi wazi mauaji ya kimbari ya Wapalestina huko Gaza, Marekani imetangaza kuwa itafuta visa ya Rais wa Colombia, Gustavo Petro, kutokana na kauli aliyotoa wakati wa maandamano ya kuunga mkono Wapalestina huko New York.
Petro alijiunga na waandamanaji huko New York, akiwa na mwanamuziki wa Uingereza Roger Waters, wakati Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Petro ameuambia umati mkubwa wa watu: “Kinachotokea Gaza hakina mjadala—ni mauaji ya kimbari,” akiongeza kuwa kura ya turufu ya Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa imeharibu kabisa matumaini ya diplomasia.
Amesema kuwa wiki iliyopita, wakati Marekani ilipoweka turufu kwa azimio la kutaka kusitishwa kwa vita Gaza kwa mara ya sita, “diplomasia ilifika ukingono.”
Rais wa Colombia amebaini kuwa: “Historia ya binadamu imetuonyesha kwa milenia kwamba diplomasia ikifika ukingoni, tunapaswa kuingia katika awamu nyingine ya mapambano.”
Rais Petro pia aliwaomba wanajeshi wa Marekani wasitii amri za Rais Donald Trump.
Rais Colombia amesema: “Kutoka New York, nawaomba wanajeshi wote wa jeshi la Marekani msitumie nguvu dhidi ya watu. Kataa amri ya Trump, tii amri ya ubinadamu.”
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Colombia, Armando Benedetti, aliandika kwenye X kwamba visa ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ndiyo iliyopaswa kufutwa badala ya ya Petro.

Aliongeza: “Lakini kwa kuwa ubeberu unamlinda, inamwadhibu rais pekee aliyekuwa na ujasiri wa kumwambia ukweli usoni.”
Vyombo vya habari vya Colombia viliripoti kuwa Petro alikuwa tayari safarini kurejea Bogota kutoka New York Ijumaa jioni wakati , Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kubatilisha visa yake.
Wakati Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa Israel alipokuwa akihutubia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ijumaa, waandamanaji mitaani New York walijitokeza kwa wingi kumpinga.
Waandamanaji walianza kukusanyika Times Square, mbali kidogo na jengo la Umoja wa Mataifa, mapema asubuhi. Bendera ya Palestina ilipepea hewani huku baadhi ya waandamanaji, wengi wao wakiwa vijana, wakibeba mabango yaliyoandikwa “Sitisha msaada wote wa Marekani kwa Israel,” “Mkamateni Netanyahu” na “Acheni kuinyima Gaza chakula sasa!”
Umati ulishangilia wakati waandaaji walipotangaza kuwa wakuu wa karibu nchi zote duniani walitoka nje ya ukumbi wa Mkutano Mkuu Umoja wa Mataifa wakati Netanyahu alianza kuhutubu.
Waandamanji walisikika wakipaza sauti na kusema: “Netanyahu huwezi kujificha, tunakushitaki kwa mauaji ya kimbari!”