
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera za rais wa Marekani ziko kwenye mkondo wa kuibua mabadiliko makubwa na vurugu katika eneo lote la Asia ya Magharibi, akionya kuwa Iran itakabiliana na wavamizi wowote kwa nguvu ya juu kabisa iwapo kutatokea uvamizi mpya wa kijeshi.
Masoud Pezeshkian ametoa kauli hiyo katika mahojiano na Shirika la Habari la NBC News la Marekani, Ijumaa. Amebainisha kuwa “Rais [Donald] Trump amesema serikali yake imekuja kuleta amani, lakini njia waliyotumia itawasha moto katika eneo zima.”
Chini ya utawala wa zamani na wa sasa wa Trump, Marekani imeendeleza au kupanua uingiliaji wake wa kijeshi katika eneo hili, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya moja kwa moja na ya mara kwa mara dhidi ya mataifa ya kikanda kama Iran na Yemen.
Rais Pezeshkian pia aligusia msaada wa kijeshi na kijasusi usio na kifani wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, mshirika wake mkuu wa kikanda. Kupitia msaada huo, uliopanda kwa kiwango cha mabilioni ya dola chini ya Trump, Tel Aviv imeongeza kasi ya utekelezaji wa mipango yake ya kupanua ardhi na mashambulizi ya kikatili dhidi ya Ukanda wa Gaza, Syria, Lebanon, Yemen, Iran, na hivi karibuni Qatar.
Rais wa Iran ameashiria kulipiza kisasi Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya Iran mnamo mwezi Juni, na kusemaakisema: “Atakaye tuvamia, tutafanya kila tuwezalo kumpa jibu kali kabisa.”
Ameongeza kuwa licha ya kutoanzisha vita, Jamhuri ya Kiislamu “haioni hofu” ya vita.
Rais Pezeshkian amesema Iran itazidisha uwezo wa ulinzi kila siku ili kuzuia yeyote kuishambulia nchi.
Vita vya siku 12 vilivyodumu kuanzia Juni 13 hadi Juni 25 vilishuhudia Jeshi la Iran likianzisha oparesheni za kujihami kwa ujasiri na mashambulizi ya kisasi kwa kutumia mamia ya makombora ya balistiki, ikiwemo makombora yenye kasi ya juu (hypersonic), pamoja na ndege zisizo na rubani.
Mashambulizi hayo ya kisasi yalilenga maeneo ya kijeshi, nyuklia na viwanda vya kimkakati vya utawala haramu wa Israel na pia kituo cha anga cha al-Udeid , kituo muhimu zaidi cha anga cha jeshi la Marekani katika eneo la Asia Magharibi kilicho nchini Qatar.