
Chanzo cha picha, Getty Images
Hakuna mtu anayependa kufikiria kuhusu mwisho wa maisha yake.
Lakini katika nyakati ngumu pale ambapo tiba hushindwa, na maneno hayawezi kueleza, muziki huwa ni lugha pekee inayobaki kueleweka.
Watu wengi wameanza kuunda orodha za nyimbo, si kwa ajili ya burudani tu, bali kama njia ya kutazama maisha yao kwa upendo, heshima, na kumbukumbu.
Hizi nyimbo si tu sauti, bali ni alama za maisha yaliyoguswa, kupendwa na kuishi kwa maana.
Kwa miaka mingi, DJ wa burudani, Dave Gilmore, alihusika katika kuchangamsha usiku wa watu kwenye baa na kumbi za starehe.
Lakini sasa, anaandaa orodha ya nyimbo ya pekee kabisa, nyimbo zilizogusa maisha yake zitakazomsindikiza katika safari ya kukabiliana na ugonjwa ambao utakatisha ndoto na maisha yake.
Miongoni mwa nyimbo hizo ni November Rain na Sweet Child O’ Mine za Guns N’ Roses, Apache ya The Shadows, wimbo uliomvutia kuanza kupiga gitaa pamoja na Comfortably Numb ya Pink Floyd.
Pia kibao cha Will You? ya Hazel O’Connor, aliyoitolea kwa mke wake na mama wa watoto wao wawili mwaka 1980.
Njia ya mvutano wa kimapenzi lakini wenye nguvu, inajulikana kwa saksafoni yake pekee – ala ambayo Dave pia alijifunza kucheza.
“Ni wimbo wetu tangu tulipoanza kuwa pamoja,” Dave anasema huku akitabasamu na kupiga miguu sakafuni. Mke wake, Kate, anaongeza kwa upole: “Ilikuwa mapambano, lakini yalistahili.”

Chanzo cha picha, Kate Gilmore/BBC Morning Live
Wakati nyimbo hizo zinapocheza, zinarejesha kumbukumbu, na huleta hali ya ukaribu, hata katika kipindi kigumu.
Muziki una nguvu ya kipekee ya kuunganisha watu kihisia, hasa unapokaribia kufa.
Katika huduma za afya ya wagonjwa wa mwisho wa maisha (palliative care), muziki unatambuliwa kama njia yenye nguvu ya kutuliza, kuleta kumbukumbu, na kusaidia wagonjwa na familia zao kupita katika kipindi hicho kwa hali ya utulivu.
Sarah Metcalfe, mkurugenzi wa Music for Dementia, anaeleza kuwa muziki “huangaza” sehemu nyingi za ubongo kwa wakati mmoja kihisia na kimwili. Hata sehemu za ubongo zikidhoofika, muziki bado unaweza kufikia sehemu nyingine na kusababisha athari nzuri.”
“Hata kama sehemu moja ya ubongo imeathirika, muziki bado unaweza kufika kupitia njia nyingine.”Sarah anasema.

Chanzo cha picha, Kate Gilmore
Shirika la misaada la Uingereza Marie Curie lilichunguza watu wazima 1,000 ambao wapendwa wao walikuwa wamepokea huduma katika hatua za mwisho za maisha.
Tafiti kutoka shirika la hisani la Uingereza, Marie Curie, zimeonesha kuwa kusikiliza muziki pamoja kunaleta hali ya ushirikiano, huruma, na ukaribu baina ya mtoa huduma na mgonjwa au familia.
Kwa mfano, Kate alieleza jinsi muziki wa asili ya Wenyeji wa Marekani ulivyomsaidia Dave kupata usingizi baada ya kurudi nyumbani akiwa amechoka na mwenye wasiwasi:
“Alikuwa mwenye hofu na hakupumzika, lakini mara tu nilipopiga muziki alioupenda, alitulia na kuanza kulala.”
Katika hospitali ya Marie Curie huko Glasgow, muuguzi na mwanamuziki Diana Schad ameweka piano kwa ajili ya wagonjwa na wahisani. Kwake, muziki ni sehemu ya huduma:
“Kila mara jiulize: Hii ni hisia gani ningependa mgonjwa apate sasa hivi?” anasisitiza.
Jinsi ya kuunda orodha ya nyimbo ya faraja (Palliative Playlist)
Wataalamu wanapendekeza:
- Chagua nyimbo kutoka kipindi cha ujana (miaka 10–30) — ambapo kumbukumbu nyingi hujengwa.
- Jumuisha nyimbo zinazohusiana na matukio muhimu — mapenzi, harusi, likizo, au sehemu za kipekee.
- Zingatia hisia nyimbo zinazoleta — huzuni, matumaini, au faraja.
- Tambua kuwa hata kwa wagonjwa wenye shida za kumbukumbu (kama dementia), muziki unaweza kuchochea sehemu hai za kumbukumbu.
- Usipuuze nyimbo zisizotarajiwa — kama nyimbo za vipindi vya TV au matangazo ya zamani ambayo yanaweza kuwa na maana ya pekee.
Chanzo: Muziki kwa mkurugenzi mkuu wa Dementia, Sarah Metcalfe

Chanzo cha picha, Marie Curie
Daktari Sam Murphy, mtaalamu wa masuala ya kifo na maombolezo, anasema kuna ushahidi kuwa kusikia ni hisia ya mwisho kupotea, hivyo muziki unaweza kumfikia mtu hata akiwa hana fahamu.
Muziki baada ya kifo: Faraja inayoendelea kuishi
Muziki unaweza kusaidia vile vile kwa wapendwa baada ya mtu kufariki.
“Nadhani ni usumbufu mwingine kwa watu hao ambao wanaomboleza mpendwa,” Dk Murphy anasema. “Lakini kuna faraja hiyo kwa kujua kwamba wanasikiliza kitu ambacho mpendwa wao angesikiliza kwa miaka mingi.”
Anna-Kay Brocklesby alimpoteza mume wake Ian mwaka 2023 kutokana na saratani ya tezi dume.
Anasema familia yao ilitumia nyimbo kumsaidia Ian kubaki na matumaini kila asubuhi aliimba Oh, What a Beautiful Morning, huku akitengeneza chai.
“Ilikuwa kama njia yake ya kusema: Hii leo itakuwa nzuri.”
Nyimbo za Frank Sinatra, Nat King Cole, na Elton John zilikuwa sehemu ya faraja yao.
Miaka miwili tangu kifo chake, Anna-Kay bado hupata tumaini kupitia muziki waliokuwa wakishiriki pamoja.
“Ian bado anaishi ndani yetu kwa njia nyingi,” anasema. “Lakini muziki hutuchukua hadi pale tulipokuwa pamoja naye.”
Mtazamo wa kiafrika kuhusu muziki na mwisho wa maisha
“Muziki ni lugha ya roho; hutufungulia milango ya hisia ambazo maneno hayawezi kufikia.”
Msanii maarufu kutoka Zimbabwe, Oliver Mtukudzi, alisema.
Katika tamaduni nyingi za Kiafrika, muziki si tu burudani au sauti rahisi, bali ni sehemu ya maisha yenye nguvu za kiroho na kijamii.
Hii inaonyesha jinsi muziki unavyoweza kuwakilisha safari nzima ya mtu kuanzia furaha za utotoni, changamoto za maisha ya mtu mzima, hadi kumbukumbu za mwisho kabla ya kuaga dunia.
Kwa mtu anayeishi na ugonjwa hatari au anayejiandaa kwa kifo, muziki huwa njia ya kuwasiliana na hisia zao za ndani, faraja, na hata matumaini.
Ni kama sauti ambayo inaunganisha roho na dunia, na kuwapa wanaoachwa nyuma njia ya kuenzi kumbukumbu na kupona kiroho.
Katika mazingira haya, muziki unakuwa si tu nyimbo au sauti, bali ni hadithi ya maisha yenye utu, heshima, na upendo usiohofu.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid