
Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yisrael Katz alisema Jumamosi kwamba jeshi “linazidisha mashambulizi yake huko Gaza na kusonga mbele kufikia hatua muhimu,” akibainisha kuwa “zaidi ya wakazi 750,000 wamefurushwa kutoka mji wa Gaza kuelekea kusini.”
“Ikiwa Hamas haitawaachilia mateka wote na kuweka chini silaha zake, Gaza itaangamizwa na Hamas itaondolewa,” aliongeza katika chapisho kwenye jukwaa la X.
Wizara ya afya ya Gaza ilitangaza siku ya Jumamosi kwamba idadi ya waliofariki imeongezeka hadi 65,926 na majeruhi 167,783 tangu kuanza kwa vita vya Gaza.
Wizara hiyo ilisema katika ripoti yake kwamba “miili ya watu 77 na majeruhi 265 walifika katika hospitali za Ukanda wa Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita.”

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati huo huo maelfu ya Waisraeli waliandamana mjini Tel Aviv wameandamana wakishinikiza makubaliano ya kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza, siku mbili kabla ya mkutano uliopangwa kufanyika kati ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na Rais wa Marekani Donald Trump mjini Washington.
Walipokusanyika katika uwanja wa Hostage {Mateka}, waandamanaji waliinua bendera kubwa iliyosomeka, “Mateka wote, warudisheni nyumbani sasa.”
“Kitu pekee ambacho kinaweza kutuzuia kuteleza kwenye shimo ni makubaliano kamili na ya kina ambayo yanamaliza vita na kuwarudisha mateka wote na wanajeshi makwao,” alisema Lishay Miran Lavi, mke wa Omri.