
Chanzo cha picha, Sylvia Bloom family album
-
- Author, Isabel Caro
- Nafasi, BBC News Mundo
Tarehe 11 Septemba 2001, mwanamke mmoja alikuwa njiani kuelekea ofisini kwake karibu na Jumba la Biashara la World Trade Center jijini New York.
Hata hivyo, mashambulizi ya kigaidi yalikatiza siku yake kama zilivyokatizwa maisha ya maelfu ya watu.
Mwanamke huyo alikuwa Sylvia Bloom, ambaye alikuwa na umri wa miaka 84 wakati huo.
Akiwa amejaa hofu kama wengi, aliambiwa na mamlaka arejee nyumbani. Hivyo, aliabiri basi na kurudi alikotoka.
Mwanamke huyo hakuwa maarufu, wala hakuwa mtu wa siasa au mjasiriamali mashuhuri.
Maisha yake ya kawaida yalificha siri kubwa na alikuwa milionea aliyejikusanyia utajiri wake kimyakimya kwa zaidi ya miongo sita.
Kwa wale waliomfahamu, tukio hilo lilielezea vyema tabia yake, mtulivu, mwenye nidhamu, na asiyependa makuu.
Ingawa alikuwa na utajiri wa mamilioni ya dola, aliishi maisha ya kawaida kabisa, bila anasa wala majivuno.
Katika kipindi cha maisha yake, Bloom alikusanya utajiri mkubwa kupitia njia isiyo ya kawaida, aliiga uwekezaji wa mabosi wake wa kazi, wanasheria wa kampuni ya Cleary Gottlieb Steen & Hamilton, ambako alihudumu kama katibu kwa muda wa miaka 67.
Kila mara bosi wake alipomwagiza anunue hisa fulani kupitia dalali wa soko la hisa, Sylvia naye angenunua sehemu ndogo ya hisa hizo kwa niaba yake binafsi.
Kwa mfano, kama bosi aliagiza anunue hisa 1,000 za AT&T, Sylvia naye angenunua 100 tu kwa kutumia mshahara wake mdogo.
Licha ya kuwa hakuwa na elimu ya juu ya kifedha, uamuzi huo mdogo ulizaa matunda makubwa.
Alijifunza kwa kutazama, na akawekeza kwa subira na hatimaye, utajiri wa zaidi ya dola milioni 9 ukajikusanya bila ya mtu yeyote kujua.
Hadithi yake haikujulikana hadi 2018, miaka miwili baada ya kifo chake, wakati iligunduliwa kuwa sehemu ya utajiri wake ingetolewa kwa Makazi ya Henry Street katika Upande wa Chini Mashariki mwa New York, ili kufadhili ufadhili wa masomo kwa vijana wasiojiweza.
Mchango huo ulifikia $6.24m, zawadi kubwa zaidi ya mtu binafsi katika historia ya zaidi ya miaka 125 ya shirika.
Dola 2m za ziada zilitolewa kwa mashirika mengine ya kutoa misaada.
Lakini huyu New Yorker alikuwa nani, na ni nini kilimsukuma kujenga utajiri kimya kimya kwa manufaa ya wengine?
Mwerevu na mjanja
Sylvia alizaliwa mwaka 1919 huko Brooklyn, New York.
Akiwa binti wa wahamiaji kutoka Ulaya Mashariki, alikulia katika mazingira ya taabu wakati wa Great Depression kipindi cha mdororo mkubwa wa uchumi duniani.
Licha ya changamoto hizo, alikamilisha masomo yake kupitia shule za serikali, na hata kusomea chuo kwa usiku ili aweze kufanya kazi mchana.
Mwaka 1947, alijiunga na kampuni mpya ya sheria iliyokuwa inaanza wakati huo Cleary Gottlieb Steen & Hamilton iliyokuwa Wall Street.
Hapo ndipo alipoanza safari yake ya maisha ya kazi, akihudumu kwa uaminifu na bidii kwa karibu miongo saba.

Chanzo cha picha, Getty Images
“Alikuwa New Yorker mwerevu na mjanja,” alikumbuka mpwa wake Jane Lockshin, akizungumza na BBC mnamo 2018.
“Katika … miaka ya 1940 na 1950, alipoanza kufanya kazi, makatibu walifanya kila kitu kwa wakubwa wao: walisawazisha vitabu vya hundi, kulipa bili, na wakati bosi alitaka kununua hisa, angeweza kusema, ‘Piga simu wakala wangu na ununue hisa elfu za AT&T.’ Sylvia angempigia simu wakala wake na kujinunulia hisa mia moja za AT&T,” Lokshin alisema.
Ingawa alitamani kuwa mwanasheria, hakuweza kutimiza ndoto hiyo.
Badala yake, aliolewa na Raymond Margolies, mwanazimamoto wa jiji ambaye baadaye aligeukia kazi ya ualimu.
Waliishi kwenye nyumba ya kupanga ya kawaida yenye chumba kimoja huko Brooklyn.
Hawakuwa na watoto, lakini walifurahia maisha yao walipenda kusafiri, kutazama opera, na mara kwa mara walitembelea Las Vegas, ambapo Sylvia aliwahi hata kumwona Elvis Presley akitumbuiza.
Bloom alistaafu akiwa na umri wa miaka 96 na akatumia siku zake za mwisho katika nyumba ya kulelea wazee.
Alifariki dunia mwaka 2016.
Katika ibada ya ukumbusho wake mwaka wa 2016, wageni walimkumbuka mwenzao akisema, “Angekuwa mwanasheria bora, mwerevu, mchambuzi, mvumilivu, mwenye hekima na mwaminifu.”
Wale waliomjua walimkumbuka kwa furaha ” kicheko cha kuambukiza na tabasamu zuri.” Wengine walisifu tabia na maadili yake: “Mtaalamu, mwaminifu, mnyenyekevu, mwaminifu, mkarimu, aliyejitolea na mwenye maadili ya kazi yasiyopungua.”
“Alikuwa mkweli na fikra huru kabisa. Akili yake ilikuwa kali, na maneno yake yalikuwa sahihi.”
Cha kustaajabisha
Ilikuwa ni wakati wa maandalizi ya wosia wake ambapo siri ya utajiri wake ilifichuka.
Mpwa wake, Jane Lockshin, aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi yake, alibaki kinywa wazi alipokagua akaunti za shangazi yake.
“Nilianza kutengeneza jedwali la mali zake dola milioni 3 katika kampuni moja ya udalali, milioni 1 katika nyingine na mwishowe, alipofariki, alikuwa na zaidi ya dola milioni 9. Nilishangaa sana,” alisema Lockshin katika mahojiano na BBC mwaka 2018.
Sylvia alikuwa mtu wa faragha sana, na hata mumewe hakujua kiwango cha utajiri alichokuwa nacho.
Bi Lockshin alieleza kuwa Bloom na mumewe waliishi katika nyumba ya chumba kimoja huko Brooklyn.
Walisafiri mara nyingi, mjomba wake alipenda kucheza kamari, na walitembelea Las Vegas mara kwa mara.
Sylvia, shabiki wa Elvis Presley, hata alimwona akiigiza huko. Pia walisafiri Ulaya na kufurahia opera. “Waliishi vizuri, lakini sio kwa ubadhirifu,” alisema.
Paul Hyams, ambaye alifanya kazi na Bloom kwa miaka kadhaa, alionyesha mshangao wake aliposikia juu ya utajiri aliokuwa amejikusanyia kimya kimya.
“Hakuwahi kuzungumza kuhusu pesa, na hakuishi maisha ya juu,” alisema. “Hakuwa mcheshi na hakutaka kujionyesha.”
Ingawa ukubwa wa kiwanja hicho ulimshtua Bi Lockshin na familia nzima, matumizi yaliyokusudiwa ya pesa hizo hayakufanyika.
Kama mtoto aliyezaliwa wakati wa Great depression kipindi cha uchumi kudorora bidhaa ya elimu ya umma, ilionekana kawaida kwamba Bloom angetaka bahati yake kusaidia vijana bila njia ya kuendelea na masomo yao.
“Shangazi Sylvia, ambaye alipata digrii yake ya chuo kikuu kupitia masomo ya usiku, kila wakati alithamini elimu. Alitaka mali yake ifaidi wale ambao hawakuweza kuipata,” alisema Bi Lockshin.
Ufadhili
Akiwa mweka hazina wa wakfu wa Henry Street Settlement, Bi Lockshin ndiye aliyewasilisha habari za furaha za mchango wa shangazi yake wa milioni kwa shirika.
“Sote hatukuwa na la kusema, tulishangaa tu,” akakumbuka David Garza, mkurugenzi mtendaji wa wakfu wakati huo katika mahojiano na gazeti moja nchini Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa msaada wa mchango huo, uliundwa Mfuko wa Ufadhili wa Bloom-Margolies, unaolenga kusaidia wanafunzi kuanzia kidato cha tatu hadi wanapohitimu chuo kikuu.
Mpango huu unajumuisha ushauri wa masomo, maandalizi ya mitihani ya kujiunga na vyuo (SAT), ziara za vyuo, na msaada wa kitaaluma hadi kufuzu.
Kiasi hicho kikubwa pia kilitolewa kama mfuko wa kudumu wa uwekezaji ili riba yake iendelee kufadhili ufadhili huo milele.
Mwaka 208 alipoulizwa Bloom nakituo cha utangazaji cha CBC angejisikiaje Sylvia kuhusu umaarufu aliopata baada ya kifo chake kutokana na mchango huo mkubwa, mpwa wake alijibu:
“Angechukizwa. Angejificha. Lakini naamini angekubali kuwa umaarufu huo unasaidia kuangazia mashirika na wanafunzi aliowalenga kusaidia. Na hilo lingeleta tabasamu moyoni mwake.”
Sehemu za makala haya zilitokana na mahojiano yaliyofanywa na kipindi cha Outside Source kwenye BBC
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid