s

Kwa mara ya kwanza katika historia ya siasa za vyama vingi nchini Tanzania, wagombea urais wanawake wamejitokeza kwa wingi na kwa nafasi ya juu ya kisiasa kuliko wakati mwingine wowote.

Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unashuhudia siyo tu rais mwanamke akitetea kiti chake, bali pia wanawake wengine wawili wakipeperusha bendera za vyama vya upinzani. Ni uchaguzi wenye wagombea urais watatu wanawake, ikitoa ishara ya mabadiliko makubwa ya kisiasa na kijamii.

Wachambuzi wanasema hali hii ni zaidi ya matokeo ya siasa za vyama binafsi. Ni ishara kwamba jamii ya Tanzania, kupitia mjadala wa umma na uzoefu wa miaka ya karibuni, imeanza kuukubali uongozi wa wanawake katika nafasi za juu.

Wakati katika chaguzi zilizopita wanawake walihesabika kwa vidole, sasa 2025 unakuwa mwaka wa kihistoria ambao uwepo wao unaleta uzito mpya katika mijadala ya kisiasa.

Historia fupi ya wanawake kugombea urais Tanzania

Mara ya kwanza jina la mwanamke lilionekana kwenye karatasi za kura za urais ilikuwa mwaka 2005, alipogombea Anna Senkoro kupitia chama cha PPT Maendeleo. Ingawa alishika nafasi ya nane kati ya wagombea kumi, hatua yake ilifungua njia kwa wengine. Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi 1995 na uliofuata wa 2000 hakukuwa na mgombea urais mwanamke.

Miaka kumi baadaye, Anna Mghwira wa ACT alikuja na kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa 2015, hatua iliyoanza kuonyesha uthubutu wa wanawake kwenye nafasi za juu za uongozi wa nchi. Lakini hata hivyo, katika uchaguzi huo na ule wa 2020, nafasi ya wanawake iliendelea kuwa finyu. Cecilia Mwanga (Demokrasia Makini) na Queen Sendiga (ADC) waligombea mwaka 2020, lakini walimaliza katika nafasi za chini.

Hatua kubwa zaidi ilikuja mwaka 2021, wakati aliyekuwa mgombea mwenza wa Rais John Magufuli katika uchaguzi wa 2015 na 2020, Samia Suluhu Hassan alipoapishwa kuwa rais kufuatia kifo cha Magufuli.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania na Afrika Mashariki, nchi iliongozwa na rais mwanamke. Tukio hilo huenda likawa chachu ya mabadiliko ya siasa za Tanzania.Tangu wakati huo, mjadala kuhusu nafasi ya wanawake kwenye uongozi ukapata msukumo mpya.

Mwaka 2025 ni wa rekodi mpya ya wanawake

s

Chanzo cha picha, TBC

Mwaka huu, historia mpya inaundwa. Wapo wagombea urais wanawake watatu: Samia Suluhu Hassan wa CCM, akiwania muhula wake wa kwanza kama mgombea urais baada ya kuingia madarakani baada ya kifo cha Magufuli. Muhula ambao utakuwa wa mwisho pia kikatiba kugombea tena uchaguzi ujao.

Mwajuma Noty Mirambo wa UMD, mwanasiasa aliyeanzia kwenye michezo na baadaye akajitosa kwenye udiwani kabla ya kugombea ubunge mara kadhaa. Safari yake imekuwa ya kupanda na kushuka, lakini sasa anasema amejiandaa kwa nafasi ya juu kabisa.

Saum Hussein Rashid wa UDP, ambaye kwa sasa ndiye Katibu Mkuu wa chama hicho, akisisitiza ajenda ya usawa wa kijinsia na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, ni mgombea mwingine aliyeingia kwenye debe.

Zaidi ya wagombea hao, vyama kumi vimewateua wanawake kama wagombea wenza wa urais. Hii ni mara ya kwanza Tanzania kushuhudia idadi hiyo kubwa ya wanawake kuwania kushika nafasi za juu za uongozi wa nchi. Wakati wagombea wenza mara nyingi hupatikana kwa vigezo vya kisiasa na kijiografia, mwaka huu uteuzi umeonyesha msisitizo wa wazi wa vyama kuonyesha kujali usawa wa kijinsia.

Kwa ujumla, vyama 18 viko kwenye mbio za urais, na hatua ya vyama vidogo kumteua mwanamke imeongeza hamasa kwamba huu ni uchaguzi wa “wanawake.” Ingawa wagombea hao huenda wakakabiliwa na changamoto za kukubalika kwa upana, ishara iliyotumwa tayari ni kubwa na inabadilisha historia ya siasa nchini.

Nini tafsiri yake na kilichobadilika?

S

Chanzo cha picha, CCM

Wachambuzi wanasema uamuzi wa vyama kuwasimamisha wanawake unaakisi mabadiliko ya kijamii na kisiasa yaliyopata nguvu zaidi ndani ya miaka 15 iliyopita.

Elimu, uhamasishaji wa haki za wanawake na mfano wa Rais Samia vinatajwa kama sababu kuu zinazoongeza imani kwa wanawake kushika nafasi za juu.

“Kuna mwamko fulani wa jamii na ni kweli idadi imeongezeka, lakini ukilinganisha na wagombea wanaume kuna kupwaya”, anasema Mohammed Issa, mchambuzi wa siasa.

Wakati mwingine, vyama huona ni busara kisiasa kuonyesha sura mpya kupitia wagombea wanawake, hasa katika zama ambazo wapiga kura vijana na wanawake wanachangia sehemu kubwa ya idadi ya wapiga kura.

Kwa Mwajuma Mirambo, aliyejitosa kugombea ubunge na udiwani katika chaguzi kadhaa zilizopita, changamoto alizokutana nazo zinathibitisha mabadiliko haya. “Miaka ya nyuma ilikuwa vigumu sana, tamaduni ziliwaweka wanawake nyuma. Lakini sasa tunaamini wanawake wanaweza kuongoza, na jamii imeanza kutuamini pia,” anasema. Hali hii, anadai, ndiyo inayompa ujasiri kwamba safari hii kuna uwezekano wa mwanamke kushinda hata kutoka upande wa upinzani.

Wako wengi na changamoto nyingi

S

Chanzo cha picha, INEC

Licha ya maendeleo haya ya idadi ya wagombea urais wanawake, changamoto bado hazijaondoka. Vyama vya siasa nchini Tanzania vimeendelea kutawaliwa na wanaume katika uongozi wa juu, na mara nyingi wanawake hukosa rasilimali za kifedha na mitandao ya kisiasa inayowasaidia kufanya kampeni kubwa. Hali hii inamaanisha kuwa uwepo wa wanawake kama wagombea pekee hauhakikishi nafasi ya kushinda.

“Ukimuondoa mgombea wa CCM, Samia Suluh Hassan, hawa wengine kwenye vyama hivi vya upinzani, unaona kuna kupwaya, lakini kwa ujumla hakuna upinzani mkubwa, kwa kuwa hakuna hata huo ushindani mkubwa baina ya vyama vyenyewe hivi kwa hivyo huweiz kulinganisha vizuri kati ya wagombea wanaume na wagombea wanawake’, anasema Mohammed Issa.

Pia, mfumo wa uchaguzi umekuwa ukilalamikiwa kwa changamoto zake, ikiwemo upatikanaji wa haki sawa kwa vyama vidogo. Kwa wagombea kama Mwajuma na Saum Rashid, kukabiliana na mashine kubwa ya kisiasa ya CCM kunabaki kuwa mtihani mkubwa. Aidha, mitazamo ya kijamii yenye mizizi ya muda mrefu kuhusu wanawake na uongozi bado ipo, hasa katika maeneo ya vijijini.

Hata hivyo, matokeo yatakavyokuwa, uchaguzi huu unaweka alama kwamba siasa za Tanzania haziwezi tena kuzungumziwa bila kujumuisha nafasi ya wanawake. Wakati historia ya Bibi Titi Mohammed, Lucy Lameck na viongozi wengine wa mwanzo inaendelea kukumbukwa, kizazi kipya kinaongeza sura mpya kwenye simulizi ya taifa.

Baada ya Oktoba 2025, Je, huu utabaki kuwa uchaguzi wa kipekee, au mwanzo wa zama mpya za usawa wa kijinsia katika siasa za Tanzania?

s

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *