Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu (kulia) akipeana mkono na Rais wa Marekani Donald Trump mbele ya waandishi wa habari. Nyuma yao kuna bendera zao za kitaifa.

Chanzo cha picha, EPA

    • Author, Tom Bateman
    • Nafasi, State department correspondent at the White House

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa mpango wake wa kumaliza vita Gaza unaweza kuwa “mmoja wa siku muhimu zaidi katika historia ya ustaarabu wa binadamu,” na kwamba unaweza kuleta amani ya milele katika Mashariki ya Kati.

Kauli hiyo iliyokuwa na uzito mkubwa ilikuwa ya kawaida kwa mtindo wa Trump.

Hata hivyo, pendekezo lake la vipengele 20, alilolitangaza Jumatatu katika Ikulu ya White House akiwa na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, linaweza kuchukuliwa kama hatua muhimu ya kidiplomasia japokuwa haifikii viwango vya kauli zake za kupindukia.

Mpango huo unaashiria mabadiliko ya sera ya utawala wa Trump kuhusu mustakabali wa Gaza baada ya vita, na unaleta shinikizo kubwa zaidi kuliko ilivyowahi kutokea mwaka huu kutoka Washington kwa Netanyahu kukubali makubaliano ya amani.

Lakini utekelezaji wa mpango huo katika wiki zijazo utategemea mambo yale yale ya msingi ambayo yamekuwa kikwazo tangu awali: iwapo Netanyahu na uongozi wa Hamas wanaona faida kubwa zaidi katika kumaliza vita kuliko kuviendeleza.

Hadi sasa, Hamas haijatoa msimamo wake rasmi.

Hata hivyo, kiongozi mmoja wa kundi hilo aliiambia BBC kuwa masharti ya mpango huo hayazingatii maslahi ya Wapalestina, na kwamba Hamas haitakubali mpango wowote usiosurutisha Israel kuondoka Gaza.

Kwa upande mwingine, Netanyahu, akiwa na Rais Trump, alisema Israel inakubali kanuni zote 20 za mpango huo licha ya kwamba baadhi ya viongozi kutoka mrengo mkali wa serikali yake tayari wamekataa baadhi ya vipengele hivyo.

Hata hivyo, kukubali kanuni hizo hakumaanishi kumaliza vita moja kwa moja.

Wapinzani wa Netanyahu wa ndani ya Israel wanamshutumu kwa kuvuruga makubaliano ya amani endapo yataonekana kuhatarisha nafasi yake ya kisiasa.

Kwa hali ilivyo sasa, mpango huu unaweza usiwe wa kutosha kufanikisha kile ambacho Trump anakitamani, mafanikio ya kihistoria.

Bado kuna changamoto kubwa za kisiasa katika pande zote mbili, Israel na Hamas zinazoweza kuzuia kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho.

Moshi unaongezeka wakati wa operesheni ya kijeshi ya Israeli katika Jiji la Gaza mnamo 29 Septemba. Majengo yameharibiwa na ardhi ilikuwa imejaa uchafu

Chanzo cha picha, Reuters

Mpango huu pia una ukungu wa kimantiki unaowapa pande zote nafasi ya kuonekana kama wanaukubali, lakini katika mazungumzo ya baadaye wanaweza kuuchelewesha au kuhujumu huku wakilaumu upande mwingine kwa kushindwa kwake.

Hii si mara ya kwanza hali kama hiyo kutokea katika juhudi za mazungumzo ya amani.

Na ikitokea tena, ni wazi kuwa utawala wa Trump utasimama upande wa Israel.

Trump alimtaka Netanyahu ajue kwamba ikiwa Hamas haitakubali mpango huo, basi Marekani “itamunga mkono kikamilifu kufanya kile unachopaswa kufanya.”

Ingawa Trump aliwasilisha pendekezo hili kama makubaliano ya amani, kwa kweli ni muhtasari wa kanuni au mwongozo wa mazungumzo zaidi.

Si mpango wa kina wa kumaliza vita.

Hali hii inafanana na kile Rais wa zamani wa Marekani Joe Biden alichopendekeza Mei 2024, muundo wa hatua kwa hatua wa kusitisha mapigano na kuweka mwelekeo wa kumaliza vita.

Katika hali ile, ilichukua miezi mingine minane kabla ya Israel na Hamas kutekeleza kusitisha mapigano na kubadilishana mateka na wafungwa.

Trump anapendelea makubaliano ya mara moja ambayo yanahitaji kazi kubwa ya kuweka mipaka ya Israeli, majina ya mateka na wafungwa, masharti ya utawala wa Gaza baada ya vita, na masuala mengine ya msingi.

Hayo yote hayajawekwa wazi kwenye pendekezo hili la pointi 20 na yanaweza kabisa kuvuruga mchakato mzima.

Mpango huu unachota vipengele kutoka kwa mapendekezo ya awali, ikiwemo mpango wa Saudi-Ufaransa uliotolewa Julai, na juhudi za hivi karibuni za Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Sir Tony Blair, ambaye atakuwa sehemu ya Bodi ya Amani inayoongozwa na Trump ambayo itasimamia Gaza kwa muda.

Wakiwa wamebanwa katikati, watoto kadhaa wa Kipalestina wanajaribu kupata chakula kwa vyungu vyao vikubwa vya chuma kutoka kwa jiko la kutoa misaada katikati mwa Ukanda wa Gaza.

Chanzo cha picha, Reuters

Mpango huu uliandaliwa na mjumbe wa Trump, Steve Witkoff, pamoja na mkwe wake, Jared Kushner, baada ya kushauriana na Israel, nchi za Ulaya, na mataifa ya Kiarabu wakiwemo wapatanishi kutoka Qatar na Misri.

Miongoni mwa mambo yanayopendekezwa ni:

  • Kusitisha mapigano mara moja
  • Kuondoka kwa baadhi ya vikosi vya Israel
  • Kuachiliwa kwa mateka wote waliobaki kutoka Hamas
  • Kuachiliwa kwa mamia ya wafungwa wa Kipalestina walioko gerezani Israel
  • Kuundwa kwa serikali ya muda ya kitaalamu kuendesha Gaza, chini ya uangalizi wa Bodi ya Amani yenye makao yake Misri
  • Wanachama wa Hamas watakaoahidi amani na kukabidhi silaha watapewa msamaha; wengine watapelekwa uhamishoni

Kikosi cha kimataifa cha kuhakikisha usalama kitaongozwa na Marekani na nchi za Kiarabu

Utaifa wa Palestina umetajwa, lakini kwa maneno yasiyo wazi.

Mpango unasema kuwa iwapo Mamlaka ya Palestina iliyo Ramallah itafanyiwa marekebisho, basi huenda mazingira yakawa tayari kwa kujitawala na hatimaye kuwa taifa huru.

Mataifa ya Kiarabu yameliona pendekezo hili kuwa hatua ya mbele, hasa baada ya kukataliwa kwa mpango wa awali wa Trump (maarufu kama “Gaza Riviera”) uliolenga kuhamisha kwa lazima Wapalestina.

Pia, mpango huu unasema Israel haitamiliki au kuunganisha Gaza ingawa haijatoa ahadi kama hiyo kuhusu Ukingo wa Magharibi, jambo ambalo linaibua mashaka.

Kwa upande wa Netanyahu, anasema mpango huu unalingana na malengo yake: kuhakikisha Hamas haitakuwa tena na silaha, Gaza haimiliki silaha, na kusiwepo taifa la Palestina.

Hata hivyo, haijulikani kama vipengele hivyo hasa kuhusu kujitawala kwa Wapalestina vitapita ndani ya serikali yake yenye ushawishi mkubwa wa mrengo wa kulia.

Sasa macho yote yanaelekezwa kwa Hamas.

Kama mwandishi mwandamizi wa BBC, Rushdi Abu Alouf, alivyoandika, huu unaweza kuwa “wakati wa ‘Ndiyo, lakini…'” ambapo Hamas itaonesha kukubali mpango huku ikiomba ufafanuzi zaidi.

Hivyo basi, hatari ya kukwama kwa mazungumzo iko palepale kama ilivyokuwa kwa juhudi nyingi zilizopita.

Katika tukio jingine la kushangaza, kabla ya tangazo lao la pamoja, Trump alimshawishi Netanyahu kuomba msamaha kwa Qatar.

Qatar ilikuwa imetaka radhi baada ya shambulio la anga la Israel lililolenga uongozi wa Hamas waliokuwa Doha.

Hii inaashiria kuwa Qatar inaweza kurudi tena kama mpatanishi kati ya Israel na Hamas.

Wakati Trump na Netanyahu walipokuwa wakikutana, mashambulizi ya anga na mizinga ya Israel yaliongezeka jiji la Gaza, ambako kikosi cha tatu cha kijeshi cha Israel kilikuwa tayari kimepelekwa.

Mashambulizi haya yanatajwa kama sehemu ya mkakati wa kuilazimisha Hamas kukubali masharti, lakini yameongeza uharibifu mkubwa kwa raia.

Wakati huo huo, dunia kwa ujumla hususan Ulaya imekuwa ikikosoa vikali hatua za Israel.

Netanyahu bado anakabiliwa na hati ya kukamatwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za uhalifu wa kivita huko Gaza.

Wakati huo huo, kamanda anayesimamia Hamas huko Gaza, Ez al-Din al-Haddad, anajiandaa kwa kile kamanda mmoja wa Hamas alielezea kwa BBC kama “vita vya mwisho” vinavyohusisha wapiganaji wapatao 5,000.

Wakati mataifa ya Ulaya na Kiarabu yakiongozwa na Ufaransa na Saudi Arabia yalikuwa yakitafuta suluhu la kidiplomasia, waliamini kuwa mpango wa mpito unaomshirikisha Trump unaweza kurejesha matumaini ya suluhu ya mataifa mawili hata kama hilo halijasemwa wazi kwenye pendekezo hili.

Kwa sasa, mpango huu umeleta mwelekeo mpya wa mazungumzo.

Lakini bado kazi kubwa inasubiri mbele kazi ya kina, ya makini, na yenye majadiliano ya kweli ili kufanikisha kile ambacho Rais Trump amekieleza kama malengo yake makuu, kumaliza vita na kuleta amani ya kudumu katika ukanda wa Gaza.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *