
Aliyekuwa rais wa Senegal Macky Sall, wakati wa mahojiano yake nje ya nchi, amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu deni lililoikabili Senegal. Baada ya kuondoka kwa rais huyo wa zamani, mamlaka ya Senegal ilitangaza “deni lililofichwa” la karibu dola bilioni saba lililokusanywa kati ya mwaka 2019 na 2024. Macky Sall, ambaye analenga kwa uwazi kushikilia nafasi za kimataifa, alikuwa na hamu ya kujieleza.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Macky Sall ambaye alikuja haswa kuwasilisha kitabu chake kipya , Africa at Heart, alifanya mahojiano ya saa moja kwa Baraza la Atlantiki (Atlantic Council). Mkuu huyo wa zamani wa nchi, ambaye anaeleza kwamba anajitenga na siasa za Senegal, hata hivyo anarejea kwenye “deni hili lililofichwa,” ambalo analiona kuwa “upuuzi”: “Nilikuwa wa kwanza kusikia mazungumzo ya deni lililofichwa. Ni upuuzi.” Deni la umma, kwa ufafanuzi, haliwezi kufichwa.”
“Tunawezaje kuficha haya yote?”
Macky Sall, ambaye anajivunia mafanikio yote ya urais wake: umeme, treni za mwendo kasi, anaonyesha kwamba haelewi jinsi yeye, idara za serikali, mamlaka za kikanda, na IMF hawakuarifiwa kuhusu deni hili: “Tunawezaje kuficha haya yote, bila ufuatiliaji wa kudumu wa kimataifa wa IMF, bila mimi, Rais wa Jamhuri, kuwa na ufahamu au kuarifiwa tuhuma hizi. Au Mahakama ya Senegal kukosa kufahamu hili; inawezekanaje?”
Ukaguzi unaendelea
Katika mitandao ya kijamii, Waziri wa Uchumi, Abdourahmane Sarr, alionyesha kuwa malipo ya moja kwa moja nje ya nchi yaliyotolewa na serikali iliyopita hayakuzingatiwa katika akaunti zilizowasilishwa, haswa, kwa benki ya BCEAO, ambayo inaweza kuelezea deni lililofichwa. Macky Sall, ambaye anapendekeza kuwa anaweza kuwa mgombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anahitimisha kwa kutamka kuwa anataka “kuelewa” deni hili la dola bilioni saba linatoka wapi na pia anabaini kwamba anasubiri ukaguzi ulioombwa na mamlaka.