.

Chanzo cha picha, OHSU/Christine Torres Hicks

Wanasayansi wa Marekani, kwa mara ya kwanza, wametengeneza viinitete vya binadamu vya hatua za awali kwa kutumia DNA iliyochukuliwa kutoka kwa seli za ngozi za bonadamu na kisha kuirutubisha na mbegu za kiume.

Mbinu hiyo inaweza kusaidia kukabiliana na utasa kwa sababu ya uzee au ugonjwa, kwa kutumia karibu seli yoyote mwilini kama kianzio cha maisha.

Inaweza hata kuruhusu wapenzi wa jinsia moja kuwa na mtoto mwenye uhusiano naye wa kijeni.

Mbinu hiyo inahitaji uboreshaji mkubwa – ambayo inaweza kuchukua muongo mzima – kabla ya kliniki ya uzazi kufikiria kuanza kuitumia.

Wataalam walisema ilikuwa mafanikio ya kuvutia, lakini inahitajika kuwa na majadiliano ya wazi na umma juu ya kile sayansi walichosaidia kiwezekane.

Uzazi ulitumika kuwa hadithi rahisi ya manii ya mwanaume hukutana na yai la mwanamke. Kisha vinaungana kutengeneza kiinitete, na miezi tisa baadaye mtoto anazaliwa.

Sasa wanasayansi wanabadilisha hilo. Jaribio hili la hivi punde linaanza na ngozi ya binadamu.

Mbinu ya timu ya utafiti ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi ya Oregon inachukua kiini – ambacho kinahifadhi nakala ya kanuni zote za kijeni zinazohitajika kutengeneza mwili – kwa kutumia seli ya ngozi.

Kisha hii huwekwa ndani ya yai la mfadhili ambalo limeondolewa jeni zake.

Kufikia sasa, mbimu hii ni kama ile inayojulikana kama ‘Dolly’, kondoo wa kwanza aliyezaliwa kutoka kwa seli ya mnyama mzima na kuwekwa kwenye seli ya yai tupu iliyogunduliwa mwaka 1996.

Pia unaweza kusoma:
.

Chanzo cha picha, OHSU

Hata hivyo, yai hili haliko tayari kurutubishwa na manii kwa vile tayari lina mkusanyiko kamili wa kromosomu.

Unarithi vifurushi 23 vya DNA kutoka kwa kila mzazi wako kwa jumla ya 46, ambayo tayari yai linayo.

Kwa hivyo hatua inayofuata ni kulishawishi yai kutoa nusu ya kromosomu zake katika mchakato ambao watafiti wameuita “mitomeiosis” (neno hilo ni muunganiko wa mitosis na meiosis, njia mbili za seli kugawanyika).

Utafiti huo, uliochapishwa katika jarida la Nature Communications, ulionyesha mayai 82 yaliyotengenezwa. Yalirutubishwa na manii na mengine yakaendelea hadi hatua za mwanzo za ukuaji wa kiinitete. Hakuna yaliotengenezwa zaidi ya hatua ya siku sita.

“Tulifanikisha jambo ambalo lilifikiriwa kuwa haliwezekani,” alisema Prof Shoukhrat Mitalipov, mkurugenzi wa kituo cha Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Oregon cha matibabu ya seli na chembe za urithi.

Mbinu hiyo bado iko mbali kufikiwa katika ubora wake kwani yai huchagua bila mpangilio ni kromosomu zipi za kutupa. Inahitaji kuishia na mojawapo ya aina 23 ili kuzuia magonjwa, lakini inaishia na mbili kati ya baadhi na hakuna nyingine.

Pia kuna kiwango cha chini cha mafanikio (karibu 9%) na kromosomu hukosa mchakato muhimu ambapo hupanga upya DNA yao, inayoitwa ‘crossing over’ kwa Kiingereza.

Profesa Mitalipov, mwanzilishi maarufu duniani katika utafiti huo, alisema: “Tunapaswa kukamilisha mchakati huo.

“Mwishowe, nadhani hapo ndipo tunapoelekea siku za usoni kwa sababu kuna watu wengi sana ambao hawawezi kupata watoto.”

.

Chanzo cha picha, OHSU/Christine Torres Hicks

Teknolojia hii ni sehemu mojawapo inayolenga kutengeneza manii na mayai nje ya mwili, mchakato unaojulikana kama ‘vitro gametogenesis.’

Mbinu bado iko katika kiwango cha ugunduzi wa kisayansi wala sio majaribio ya kimatibabu, lakini maono ni kuwasaidia wanandoa ambao hawawezi kufaidika na mbinu ya kutungisha mimba nje ya tumbo la uzazi IVF (in vitro fertilisation) kwa sababu hawana manii au mayai ya kutumia.

Inaweza kusaidia wanawake wakubwa ambao hawana tena mayai ya kutosha, wanaume ambao hawatoi manii ya kutosha au watu ambao matibabu yao ya saratani yamewafanya kuwa na ugumba.

Pia mbinu hii inaweka upya sheria za uzazi. Mbinu iliyoelezewa leo sio lazima itumie seli za ngozi za mwanamke – inaweza pia kutumia ya mwanamume.

Hiyo inafungua milango kwa wapenzi wa jinsia moja kupata watoto ambao wana uhusiano nao wa kinasaba na wapenzi wote wawili. Kwa mfano, katika wanandoa wa jinsia moja, wanaume, ngozi ya mtu mmoja inaweza kutumika kutengeneza yai na shahawa ya mwenzi wa kiume kutumika kurutubisha.

“Mbali na kutoa matumaini kwa mamilioni ya watu wenye utasa kutokana na ukosefu wa mayai au mbegu za kiume, njia hii itaruhusu uwezekano wa wapenzi wa jinsia moja kupata mtoto mwenye uhusiano wa vinasaba na wapenzi wote wawili,” alisema Prof Paula Amato, kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi cha Oregon.

Kupata uaminifu na kujenga imani ya umma

Roger Sturmey, profesa wa dawa za uzazi katika Chuo Kikuu cha Hull, alisema sayansi ni “muhimu” na “ya kuvutia”.

Aliongeza: “Wakati huo huo, utafiti kama huo unasisitiza umuhimu wa kuendelea kwa mazungumzo ya wazi na umma kuhusu maendeleo mapya katika utafiti wa uzazi.

“Mafanikio kama haya yanasisitiza hitaji la utawala thabiti, kuhakikisha uwajibikaji na kujenga imani ya umma.”

Prof Richard Anderson, naibu mkurugenzi wa Kituo cha MRC cha afya ya uzazi katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, alisema uwezo wa kuzalisha mayai mapya “utakuwa maendeleo makubwa”.

Alisema: “Kutakuwa na masuala muhimu sana ya usalama lakini utafiti huu ni hatua ya kuwasaidia wanawake wengi kuwa na watoto wao wenye uhusiano nao kijenetiki.”

Soma zaidi:

Imefasiriwa na Asha Juma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *