
Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Mahfouz Zubaide
- Nafasi, Afghanistan producer
Fahima Noori alikuwa na ndoto kubwa alipohitimu kutoka chuo kikuu nchini Afghanistan.
Alikuwa amesomea sheria, alihitimu kutoka kwa programu ya ukunga na hata kufanya kazi katika kliniki ya afya ya akili.
Lakini yote hayo yaliondolewa wakati Taliban ilipoingia madarakani mwaka wa 2021.
Walipiga marufuku wasichana wenye umri wa zaidi ya miaka 12 kupata elimu, waliweka vikwazo vikali vya chaguzi za kazi kwa wanawake na hivi karibuni waliondoa vitabu vilivyoandikwa na wanawake kutoka vyuo vikuu.
Kwa Fahima, mtandao ulikuwa njia yake ya mwisho kwa ulimwengu wa nje.
“Hivi karibuni nilijiandikisha katika chuo kikuu cha mtandaoni na nilikuwa na matumaini ya kumaliza masomo yangu na kupata kazi ya mtandaoni,” alisema.
Siku ya Jumanne, njia hiyo ya kuokoa maisha ilikatwa wakati Taliban ilipozima mtandao kote nchini hali ambayo inatarajiwa kudumu kwa muda usiojulikana.
“Tumaini letu la mwisho lilikuwa kujifunza mtandaoni. Sasa hata ndoto hiyo imeharibiwa,” Fahima alisema.
Jina lake halisi limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, kama vile majina ya wengine wote waliohojiwa kwa makala haya.
”Sote tunakaa nyumbani bila kufanya chochote.”
Katika wiki chache zilizopita, serikali ya Taliban ilianza kukata muunganisho wa mtandao wa fibre-optic katika majimbo kadhaa, ikisema hii ni sehemu ya juhudi za kuzuia ukosefu wa maadili.
Kwa wengi, waliogopa hii inaweza kuwa hatua ya kwanza kuelekea kuzima kabisa kwa mtandao.
Na siku ya Jumanne, hofu yao mbaya zaidi ilitimia. Nchi hiyo kwa sasa inakabiliwa na “kukatika kwa mtandao kwa jumla” kulingana na shirika la Netblocks, hatua ambayo imelemaza huduma muhimu za nchi.
Mashirika ya habari ya kimataifa yanasema yamepoteza mawasiliano na ofisi katika mji mkuu Kabul. Mtandao wa mawasiliano na TV za satelaiti pia zimetatizwa sana kote nchini Afghanistan.
Safari za ndege kutoka uwanja wa ndege wa Kabul pia zimetatizwa, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Kabla ya kufungwa kwa nchi nzima, BBC ilizungumza na baadhi ya watu nchini Afghanistan ambao walieleza kwa kina jinsi kukatika kwa mtandao katika majimbo yao kulivyohatarisha maisha yao.
“Kabla ya hili, nilisomea ukunga, lakini kwa bahati mbaya mpango huo ulipigwa marufuku kwa wanawake… tumaini pekee lililobaki kwetu lilikuwa mtandao na kujifunza mtandaoni,” alisema Shakiba, ambaye anaishi katika jimbo la kaskazini la Tahkar.
“Tunataka kusoma. Tunataka kuelimishwa. Tunataka kuwa na uwezo wa kuwasaidia watu katika siku zetu zijazo. Niliposikia kwamba mtandao umekatika, dunia iliniona gizani.”
Ni hadithi kama hiyo kwa Fahima, ambaye anasema sasa anahisi “hawezi kutatua hili”.
“Dada zangu wawili [na mimi] tulikuwa tunasoma mtandaoni. Tulikuwa tunapata taarifa kuhusu habari na teknolojia kupitia mtandao, lakini sasa hatuwezi kuendelea au kujifunza ujuzi mpya,” alisema mwanafunzi huyo, anayeishi katika jimbo la mashariki mwa Afghanistan.
“Tulikuwa na ndoto ya kumaliza elimu yetu na kumsaidia baba yetu kifedha, lakini sasa … sote tunakaa nyumbani bila kufanya chochote.”
Tangu kutwaa madaraka mwaka wa 2021, Taliban wameweka vikwazo vingi kwa mujibu wa tafsiri yao ya sheria ya Kiislamu ya Sharia.
Mapema mwezi huu waliondoa vitabu vilivyoandikwa na wanawake katika mfumo wa kufundishia wa vyuo vikuu nchini humo ikiwa ni sehemu ya marufuku mpya ambayo pia imeharamisha ufundishaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa kijinsia.
TakribanI vitabu 140 vya wanawake, ikiwa ni pamoja na majina kama “Usalama katika Maabara ya Kemikali”, vilionekana kuwa na “wasiwasi” kutokana na “sera za kupinga Sharia na Taliban”, walisema Taliban.
Serikali ya Taliban imesema inaheshimu haki za wanawake kwa mujibu wa tafsiri yao ya utamaduni wa Afghanistan na sheria za Kiislamu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Lakini si wanafunzi wa kike pekee ambao wameathirika, walimu kama Zabi, ambaye alikuwa akiendesha maisha yake kupitia ufundishaji mtandaoni, wameathiriwa vivyo hivyo na marufuku hiyo.
Zabi anasema hapo awali aliwahi kufanya kazi kama mwandishi wa habari nchini Pakistani, lakini hakupata fursa yoyote katika tasnia hiyo aliporejea Afghanistan.
Aliamua kufungua kituo cha kufundishia Kiingereza, lakini alilazimika kutumia mtandao wakati mamlaka ilipoweka vikwazo kwa taasisi za elimu, anasema.
“Nilikuwa na wanaume na wanawake katika madarasa yangu, hadi wanafunzi 70 au 80 kwa wakati mmoja.
Wanafunzi wangu walikuwa na furaha na masomo yetu yalikwenda vizuri,” alisema. “Wote walikuwa wakijitayarisha kwa IELTS [jaribio la Kiingereza sanifu] na ujifunzaji wao wote ulitegemea mtandao. Utafiti, majaribio ya mazoezi, mitihani rasmi, kila kitu.”
Zabi, ambaye pia anaishi mashariki mwa nchi, anaongeza kuwa hakuna kituo cha IELTS nchini Afghanistan, kwa hivyo chaguo pekee kwa wanafunzi ni kusoma moja kwa moja mtandaoni.
“Siku mbili zilizopita, wanafunzi wangu wapatao 45 walikuwa katikati ya mtihani wakati mtandao ulipokatika. Walikuwa wamejitayarisha kwa miezi kadhaa, lakini walikosa fursa hiyo. Ilikuwa hali ya kuhuzunisha moyo kwao na kwangu kama mwalimu wao.”
Anaongeza kuwa yeye hupokea simu kila mara kutoka kwa wanafunzi wake ambao hawajui la kufanya.
“Wanaendelea kunipigia simu wakiniuliza ‘Mwalimu, tufanye nini?’ Kwa wavulana, bado kuna vituo vya Kiingereza vilivyofunguliwa, lakini kwa wanafunzi wangu wa kike, hii ilikuwa nafasi yao ya mwisho na sasa hata hiyo imepita.
Wengi wa waliohojiwa wanasema kwamba bado kuna chaguo la kuunganishwa kwa data ya simu, lakini ni ghali sana kwa wengi, na nguvu ya mtandao huo ni dhaifu.
Mpango wa kila mwezi wenye 100GB ya data hugharimu 3,500 Afghani, au karibu $50 (£37). Kinyume chake, Wifi ilikuwa ikigharimu takribani Afghani 1,000 kwa mwezi, ambayo inaweza kugawanywa zaidi kati ya wanafunzi wachache.
Kulingana na ripoti ya awali ya UNDP, mapato ya Afghanistan kwa kila mtu yalifikia $306 mnamo 2024.
Zabi anasema atahitaji kuondoka nchini ikiwa mtandao hautarejeshwa hivi karibuni, akisema hana njia nyingine ya kujikimu kimaisha.
Taliban bado haijatoa sababu rasmi ya kuzima. Hapo awali walisema njia mbadala ya ufikiaji wa mtandao itaundwa, lakini hawakutoa maelezo zaidi.
Anas, mbadilishaji fedha katika jimbo la Takhar, anasema biashara yake imekabiliwa na “matatizo makubwa” tangu kuzima kwa mtandao, akisema kuwa kazi yake kubwa inategemea mtandao.
“Biashara yetu imeathiriwa kwa takriban 90%,” anasema. “Jana, kaka yangu ambaye pia ni mshirika wangu wa kibiashara alijaribu kutuma barua pepe kwa mteja. Hakuweza kuipata.”
Lakini wasiwasi wake mkubwa ni binti zake watatu, ambao wote walikuwa wakisoma masomo ya mtandaoni.
“Usiku uliotangulia, tulisikia kwamba Taliban walikuwa wamepunguza ufikiaji wa mtandao huko Mazar, na binti yangu mkubwa alinijia na machozi machoni pake na kusema anahofia hali kama hiyo itatokea hapa.
“Nafasi yao ya mwisho ya kusoma sasa imetoweka. Kuwaona watoto wangu wakiwa wanyonge sana… [hilo lilikuwa] jambo gumu zaidi kwangu. Ni Mungu pekee ndiye anayejua kitakachotokea kwao na kwangu.”