
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amepongeza pendekezo la hivi karibuni la Rais wa Colombia wakati wa hotuba yake mbele ya Umoja wa Mataifa la kuundwa ‘jeshi la kimataifa’ litakalopewa jukumu la kuikomboa Palestina kutokana na uvamizi na uporaji wa ardhi unaoungwa mkono na Marekani.
Mahdi al-Mashat aliyasema hayo jana Jumanne, na kulitaja pendekezo hilo kuwa la “ujasiri na la kihistoria,” na kusisitiza tena utayarifu wa Yemen wa kutoa uungaji mkono wa aina zote kwa ajili ya ukombozi wa Palestina.
Afisa huyo wa Yemen amesema yeye binafsi, jeshi la nchi yake, na watu wake “wanajivunia” msimamo wa Rais Gustavo Petro wa Columbia.
Al-Mashat amebainisha kuwa, Yemen tayari “imeshiriki katika vita dhidi ya adui wa Mzayuni,” akitolea mfano mzingiro wa jeshi la majini la Sana’a dhidi ya manowari na meli za Israel zinazoelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Afisa huyo mwandamizi wa Yemen amevipongeza Vikosi vya Wanajeshi vilivyoendesha operesheni nyingi za kuonyesha mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambao wamekuwa chini ya vita vya mauaji ya halaiki ya Israel tangu Oktoba 2023.
Akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni, Rais Petro alitoa mwito wa kijasiri na uthubutu wa kuundwa jeshi lenye nguvu la mataifa ambayo hayakubali mauaji ya halaiki. “Lazima tukusanye silaha na kuandaa majeshi. Ni lazima tuikomboe Palestina,” alisisitiza Rais wa Colombia.
Marekani, mshirika mkubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel, iliamua kufuta viza ya Petro baadaye, ambapo kiongozi huyo wa Colombia alitoa radimali kwa kusema, “Sijali.”