Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamesimama bega kwa bega katika Ikulu ya White House. Netanyahu anatoa dole gumba kwa mkono wake wa kushoto. Trump amevalia suti ya majini iliyounganishwa na tai ya zambarau iliyokolea, huku Netanyahu akiwa amevalia suti nyeusi na tai ya bluu. Viongozi wote wawili hupiga pini za bendera zinazowakilisha nchi zao.

Chanzo cha picha, Alex Wong/Getty Images

    • Author, Luis Barrucho
    • Nafasi, BBC World Service

Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wameendeleza uhusiano wao wa karibu, walipokubaliana Jumatatu kuhusu mpango wa amani wa Gaza wenye vipengele 20.

Trump alimtaja Netanyahu kama “shujaa,” naye Netanyahu akamwita Trump “rafiki mkubwa zaidi kuwahi kuwa na Israel katika Ikulu ya Marekani.”

Uhusiano wao, mara nyingi unaotajwa kama urafiki wa kisiasa, haujakosa misuguano na tofauti za kimtazamo.

Trump hujiwasilisha kama “rais wa Marekani mwenye uhusiano wa karibu zaidi na Israel,” lakini wachambuzi wanasema ukaribu huu ulionekana zaidi katika muhula wake wa kwanza, ambapo mafanikio ya kisiasa yalidhihirika kwa pande zote mbili.

Katika muhula wa sasa, uhusiano huu unakabiliwa na changamoto mpya.

Ripoti nyingi zinaonesha kuwa Trump ana uhasama wa chinichini na mpinzani wa Netanyahu nchini Israel, huku mivutano ikiongezeka ndani ya kambi yake ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Hugo Lovatt, mtaalamu wa Mashariki ya Kati kutoka Baraza la Ulaya la Mambo ya Nje, mgawanyiko katika kundi la msingi la Trump kuhusu sera za Marekani kwa Israel unachangia kuyumba kwa uhusiano huu.

“Kuna wanaojiita ‘vizuizi na wakosoaji wa Israel’ kama JD Vance, Marjorie Taylor Greene na Tucker Carlson; kisha kuna kundi la pili, linalounga mkono Israel vikali, ambalo bado lina ushawishi mkubwa,” anasema Lovatt.

Licha ya hayo, Dkt. H. A. Hellyer kutoka taasisi ya huduma ya Royal United nchini Uingereza anasema, “Ushirikiano huu wa muda mrefu bado unaonyesha mafanikio zaidi kuliko changamoto.”

Kwa hivyo uhusiano kati ya viongozi hao wawili umekuwaje kwa miaka mingi?

Soma pia:

1.Kilele cha ushirikiano (2017–2020)

Muhula wa kwanza wa Trump uliashiria ukaribu wa hali ya juu kati ya viongozi hao wawili.

Trump alifanya maamuzi yaliyomletea Netanyahu ushindi wa kisiasa ndani ya Israel, naye Netanyahu akamtangaza Trump kuwa mshirika wa kweli wa Israel.

Uhusiano huu ulikuwa wa kirafiki, wa moja kwa moja, wenye manufaa ya kisiasa kwa pande zote, wachanganuzi wanaamini hivyo.

Matukio Muhimu

6 Desemba 2017 – Utambuzi wa Jerusalemu kama mji

Trump alitangaza Yerusalemu kuwa mji mkuu wa Israel. Netanyahu aliita hatua hiyo “ya kihistoria.” Maandamano makubwa yakazuka kote Mashariki ya Kati.

8 Mei 2018 – Marekani yajiondoa kwenye JCPOA

Trump alijiondoa kwenye mkataba wa nyuklia na Iran. Netanyahu alisema: “Rais Trump amefanya jambo sahihi.”

14 Mei 2018 – Ubalozi wahamishiwa Yerusalemu

Netanyahu aliita tukio hilo “siku tukufu.” Wapalestina 60 waliuawa Gaza siku hiyo.

25 Machi 2019 – Utambuzi wa milima ya Golan

Trump alitambua rasmi milima ya Golan kama sehemu ya Israel. Netanyahu alisema: “Israel haijawahi kuwa na rafiki bora zaidi Ikulu.”

15 Septemba 2020 – Makubaliano ya Azimio la Abrahamu

Israel, UAE na Bahrain walikubaliana kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia, mpango uliofadhiliwa na Trump. Morocco na Sudan walijiunga baadaye.

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wakipeana mikono mbele ya bendera ya Israel na Marekani mjini Jerusalem tarehe 22 Mei 2017. Wote wawili wamevalia suti nyeusi na tai za bluu.

Chanzo cha picha, HAIM ZACH / GPO / HANDOUT

2. Kuporomoka kwa mahusiano (2020–2021)

Baada ya Joe Biden kushinda uchaguzi wa urais wa Marekani mnamo 2020, uhusiano kati ya Trump na Netanyahu ulidorora ghafla.

7 Novemba 2020 – Netanyahu alimtumia pongezi Biden kupitia Twitter, saa chache baada ya matokeo kutangazwa. Hili lilimuudhi Trump.

Desemba 2021 – Trump alishambulia hadharani Netanyahu katika mahojiano na mwandishi Barak Ravid, akisema:

“Alifanya kosa kubwa…kumpongeza Biden wakwanza baada ya ushindi, sijawahi kuzungumza naye tangu hapo.”

3. Marejeo ya ushirikiano (2025)

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) uliofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mnamo tarehe 26 Septemba 2025. Amevalia suti nyeusi na tai ya rangi ya machungwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Trump alipoapishwa tena mwaka 2025, Netanyahu alifanya ziara ya haraka Washington.

Tangu hapo, ameshatembelea Ikulu mara nne zaidi ya kiongozi mwingine yeyote wa kigeni.

Ushirikiano wao sasa unaegemea zaidi kwenye mambo ya kiusalama na kisiasa kuhusu Gaza, mpango wa amani, na mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Hata hivyo, tofauti na kipindi cha awali, ushirikiano huu unatawaliwa na busara zaidi, si hisia.

Wachambuzi wanasema kuwa hata ndani ya Ikulu ya Trump, kuna kuchoshwa na Netanyahu.

“Hakuna anayemfurahia sana Netanyahu kwa sasa,” anasema Dkt. Hellyer.

“Lakini bado hali hiyo haijaathiri sera rasmi.”

Wakati huo huo, baadhi ya sauti zenye ushawishi ndani ya harakati ya MAGA zimeanza kumkosoa Netanyahu na hatua za Israel dhidi ya Gaza.

“Israel haijaachana tu na vita Gaza. Imevunja makubaliano ya kusitisha mapigano bila athari. Imeishambulia Qatar, mshirika wa Marekani, bila madhara yoyote. Imeendeleza uvamizi Syria na Lebanon, bado hakuna hatua zilizochukuliwa,” asema Hellyer.

Matukio Muhimu ya 2025

Januari – Netanyahu ampongeza Trump kwa ushindi, akisema ni “mshirika mkubwa wa Israel.”

Februari – Mazungumzo ya awali kuhusu kusitisha vita Gaza yaanza.

Aprili – Trump amkaribisha Netanyahu White House: “vita lazima vikome karibuni.” Netanyahu: “lazima tumalize kazi dhidi ya Hamas.”

Juni – Marekani yashambulia vituo vya nyuklia vya Iran kwa kushirikiana na Israel.

Julai – Trump apendekeza mkataba wa kusitisha mapigano kwa siku 60, na mchakato wa amani kuendelea.

9 Septemba – Israel yashambulia viongozi wa Hamas walioko Qatar; Marekani yakosoa.

25 Septemba – Trump apinga mpango wa Israel kuunganisha Ukingo wa Magharibi.

26 Septemba – Netanyahu atoa hotuba kwenye Umoja wa Mataifa. Zaidi ya wajumbe 100 wa kimataifa waondoka ukumbini kwa kupinga.

29 Septemba – Netanyahu afika Ikulu kwa mara ya nne mwaka huu. Ajadili mpango wa amani wa pointi 20, usimamizi wa muda wa Gaza, na kuachiliwa kwa mateka 48 (takriban 20 wadhaniwa kuwa hai).

Katika mazungumzo ya simu na Ikulu, Netanyahu pia aliomba msamaha kwa Waziri Mkuu wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim al-Thani kutokana na shambulio la Septemba 9.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *