
-
- Author, Sammy Awami
- Nafasi, BBC Swahili
-
Dkt Jane Goodall, mtafiti wa sokwe anayeaminika kuwa na ujuzi mpana na wa kina juu ya viumbe hao kuliko mtu mwingine yeyote yule amefariki dunia, akiwa na umri wa miaka 91.
Taasisi yake ya Jane Goodall Institute imesema Dkt Goodall alifariki kifo cha kawaida akiwa Calfornia nchini Marekani akiwa katika ziara yake ya kutoa mihadhara nchini humo.
Dkt Goodall alianza taaluma yake nchini Tanzania, huko Gombe Mkoani Kigoma mnamo mwaka 1960 akiwa na umri wa miaka 26 tu.
Utafiti wake ulifanya mapinduzi makubwa duniani katika kuzifahamu tabia za Sokwe kwa namna ambayo haikuwahi kufahamika hapo kabla.
Lakini ulifungua pia mlango kwa wanawake wengine kuingia katika fani ya ujuzi wa sokwe inayofahamika kama Primatolojia.
Akiwa chini ya usimamizi wa mwanaanthlopojia Louis S.B. Leakey, Dkt Goodall aligundua kwamba sokwe pia walitengeneza na kutumia nyenzo mbalimbali, suala ambalo watafiti wa awali walidhani lilifanywa na binadamu pekee.
Baadhi watakumbuka majina ya sokwe kama Fifi, Flo, Fint na Bwana McGregor. Haya yalitokana na uamuzi wake wa kuwapa sokwe majina wakati wa utafiti wake, badala yan amba kama ambavyo watafiti wengine walifanya.
Uamuzi wake huu haufurahiwa sana na watafiti wengine, wengi wao wakiwa wanaume ambao walijiona kuwa ndio vinara katika utafiti wa viumbe hawa
Hata katika umri wake wa miaka 80, Goodall alisafiri kwa takribani siku 300 za mwaka, akizunguka duniani kote kueleza si tu ujuzi juu ya sokwe lakini kuhimiza watu – hasa Watoto na vijana – juu ya kutunza mazingira na hatari ya janga la mabadiliko ya tabia nchi inayoukabili ulimwengu.
Hapa Tanzania, alihakikisha elimu na mapenzi ya mazingira inaanzia chini kabisa kwa Watoto, ambapo taasisi yake ya Jane Goodall Institute alianzisha na kuratibu vilabu vya mazingira katika shule za msingi vilivyojulikana kama Roots and Shoots
Ndugu zake wanasema haiba ya udadisi ya Goodall ilianza tangu akiwa na umri mdogo. Wanakumbuka namna gani ambavyo alikijaza chumba chake na minyoo na konokono ambao alipenda kuwadadisi kwa karibu.
Amewahi kuandika pia katika moja ya vitabu vyake namna, akiwa na miaka mitano tu, alitoroka kutoka ndani ya nyumba yao usiku wa manane na Kwenda kukaa katika banda la kuku akitaka kuona namna kuku wanavyotaga.
“Ghafla, kwa mlio wa plop, yai lilianguka juu ya majani makavu. Kwa sauti za furaha, kuku alitikisa manyoya yake, akasukuma yai kwa mdomo wake, kisha akaondoka,” aliandika Goodall takribani miaka 60 baadaye. “Ni jambo la ajabu sana jinsi ninavyokumbuka vizuri sana mfululizo mzima wa tukio hilo.”

Chanzo cha picha, Getty Images
Fursa yake ya kuja Afrika kwa mara ya kwanza iliibuka mnamo mwaka 1956 alipokaribishwa kutembelea shamba moja huko nchini Kenya.
Akiwa anafanya kazi katika kilabu cha pombe, Dkt Goodall alifanikiwa kutunza pesa za kutosha kununua tiketi ya kwenda na kurudi. Huko ndiko alipokutana na Dkt Leakey ambaye tayari alikuwepo Afrika Mashariki kwa miaka kadhaa akitafiti binadamu wa kale.
Dkt Leakey alimweleza juu ya kazi wanazozifanya nchini Tanganyika, kama ambavyo ilikuwa inafahamika wakati ule. Simulizi hizo zilimvutia sana Goodall ambaye baadae Dr Leakey na mkewe walimuajiri Dkt Goodall kuwa katibu wao na baadae msaidizi wao wa kuchimbua mabaki ya binadamu wa kale huko katika mbuga ya Serengeti.
Baadae Dkt Leakey alimweleza Dkt Goodall juu ya haja yake ya kutaka kujifunza zaidi juu ya jamii wote wa sokwe, hasa katika eneo la pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, kazi ambayo ilihitaji udadisi wa karibu na wa muda mrefu.
Dkt Goodall akasema hiyo ni aina ya kazi aliyokuwa akiiota kwa miaka mingi, na kwamba ingeufurahisha sana moyo wake.
Dkt Leakey alimtafutia fedha za masomo Dkt Goodall. Na baada ya kwenda kusoma tabia na maumbile ya sokwe na wanyama wengine wa jamii hiyo alirejea Tanganyika kuanza kufanya utafiti wake.
Sokwe wanakula nyama
Utafiti wake wa kwanza kabisa na wa muhimu ni pale alipogundua kwamba sokwe wanakula nyama pia, tofauti na uelewa wa mwanzo kwamba sokwe wanakula majani pekee.
Hii ilitokea miezi mitatu tu baada ya kuwa amewasili katika hifadhi ya Gombe tayari kwa kuanza kazi ya utafiti ambapo baada ya kunyemelea na kuchunguza kundi la sokwe aligundua walikuwa wanakula kitu kama cha rangi ya pinki vile.
Baadae aliposogea kwa karibu akathibitisha kwamba ilikuwa ni nyama ya nguruwe pori mdogo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sokwe wanatumia zana kuwinda
Wiki mbili baadae, Dkt Goodall alifanya utafiti wa muhimu zaidi ambao ndio ulikuja kusimika vizuri umahiri wake wa utafiti wa sokwe baada ya kumuona sokwe mmoja wa kiume akiwa ameketi kando ya kichuguu cha udongo mwekundu, akichomeka kwa uangalifu kijiti kirefu kwenye tundu, kisha kukitoa na kulisukuma mdomoni mwake.
Baada ya sokwe huyo kuondoka kwa mwendo wa taratibu, Dkt Goodall aliharakisha kwenda kuchunguza vizuri kwa karibu tundu lile. Akachukua kile kijiti kilichoachwa, akakichomeka kwenye tundu lilelile na kikatoka kimefunikwa na mchwa.
Sokwe huyo ambaye baadaye alimpa jina David Graybeard alikuwa akikitumia kijiti hicho kuvulia mchwa.
Hadi wakati huu, watafiti wengi waliamini ni binadamu pekee ndio walikuwa na tabia na maendeleo kama haya
Alipotuma ripoti yake kwa msimamizi wake Dkt Leakey, alijibu: “Sasa lazima tumfafanue upya binadamu, tuelezee upya zana, au tukubali kwamba sokwe nao ni binadamu!”
Baada ya hapa Goodall alifanya tafiti nyingine nyingi kuhusu sokwe ikiwa ni pamoja na tabia zao za kujamiiana, vita kati ya familia na koo moja hadi nyingine, namna sokwe wanavyojenga, kupanua na kulinda himaya zao nk.
Goodall alibahatika kupata mtoto mmoja katika ndoa yake ya kwanza, ambaye alimlea katika Hifadhi ya Taifa ya Gombe hadi alipofikisha umri wa miaka tisa.
Aliwahi kusema kwamba kulea mwanawe katika hifadhi hiyo kulimpa ufahamu kuhusu mienendo ya mama sokwe, na kwamba kuwatazama sokwe wakiishi maisha yao kulimsaidia kuwa mama bora zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sokwe wanapigana vita
Mwaka 1974 mpaka 1978 Dkt Goodall akiwa bado katika utafiti wake Gombe aligundua jambo jingine kubwa kuhusu Wanyama hao ambao awali lilikuwa halijulikani. Kama ilivyo kwa binadamu Sokwe pia huwa na migogoro baina yao. Na migogoro hiyo inaweza kudumu kwa muda mrefu na maafa makubwa hutokea.
Katika miaka hiyo minne, Dkt Goodall alishuhudia jamii moja ya sokwe ikijitenga na kuwa jamii mbili na hatimaye madume ya jamii hizo kupigana vita vikali.
Koo hizo mbili za Sokwe zilizojulikana kama Kahama na Kasekela na zilipigana kuwania eneo, malisho na madaraka. Mwisho wa vita ikawa ni kuuawa kwa madume wote wa jamii ya Kahama na ukoo wa Kasekela kuibuka na ushindi.
Kwa mujibu wa vitabu vya tafiti zake Dkt Goodall anasema kuwa vita hivyo vilimshtua sana hakutarajia kama viumbe hao wangefanana sana na binaadamu kiasi cha kupigana vita.
Viongozi mbalimbali watuma rambirambi

Chanzo cha picha, Stefan Rousseau/AFP via Getty Images
Rais wa Tanzania, ambako Goodall alisomea sokwe, amasema “kazi yake ya Hifadhi ya Kitaifa ya Gombe ilibadilisha uhifadhi wa wanyamapori.”
Utafiti huo “uliweka nchi yetu katika kiini cha juhudi za kimataifa za kulinda sokwe na asili,” Rais Samia Suluhu aliandika kwenye X.
Mwanmfalme Harry na mkewe Meghan walimsifu Goodall kama “mwanasayansi mwenye maono ya kibinadamu, mwanasayansi, rafiki wa sayari na rafiki yetu.”
“Ahadi yake ya kubadilisha maisha inaenea zaidi ya yale ulimwengu uliona, na pia kwa yale ambayo sisi binafsi tulihisi.”
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guttierez. alinukuliwa akisema katika X: Goodall anaacha “urithi wa ajabu kwa ubinadamu na sayari yetu,”
“Nimesikitishwa sana kuhusu kifo cha Jane Goodall, Mjumbe wetu mpendwa wa Amani,” aliongeza, akirejelea nafasi ya heshima aliyoipata Goodall tangu 2002 katika shirika la kimataifa kwa kazi yake ya uhifadhi.
“Zaidi ya yote, Jane alitufundisha kwamba tunapotafuta ubinadamu katika ulimwengu wa asili unaotuzunguka, tunagundua ndani yetu wenyewe,” rais wa zamani wa Marekani Joe Biden alisema.
Mnamo Januari, katika siku za mwisho za uongozi wake, Biden alimtunukia Goodall Nishani ya Rais ya Uhuru — heshima ya juu zaidi ya kiraia katika taifa hilo.