Waandamanaji waliojifunika nyuso zao wakiwa wamevalia miwani nyeusi na kofia wakiwa wamejifunika barabarani

Chanzo cha picha, Gamma-Rapho via Getty Images

    • Author, Omega Rakotomalala
    • Nafasi, BBC Monitoring
    • Author, Wycliffe Muia
    • Nafasi,

Maelfu ya raia wa Madagascar wamekuwa wakiandamana katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa zaidi ya wiki moja sasa, katika kile kinachoelezwa kuwa wimbi kubwa zaidi la maandamano kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa zaidi ya miaka 15.

Kilichoanza kama malalamiko dhidi ya upungufu wa bidhaa za msingi kimekua kwa kasi na kuwa changamoto kubwa kwa Rais Andry Rajoelina, ambaye yuko madarakani kwa mara ya pili tangu mwaka 2018.

Mnamo Jumatatu, Rajoelina alivunja serikali yake kama njia ya kujibu hasira ya wanarika wa Gen Z, lakini hatua hiyo haikuweza kuwatuliza waandamanaji.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watu wasiopungua 22 wamepoteza maisha na zaidi ya 100 kujeruhiwa katika machafuko hayo.

Hata hivyo, serikali ya Madagascar imekanusha takwimu hizo na kuzitaja kuwa ni “uvumi na taarifa potofu.”

Chanzo cha maandamano

Shinikizo lilianza kuongezeka kufuatia kukamatwa kwa wanasiasa wawili mashuhuri wa jijini Antananarivo mnamo tarehe 19 Septemba, waliokuwa wamepanga kufanya maandamano ya amani kupinga matatizo sugu ya ukosefu wa umeme na maji.

Kampuni ya umma ya huduma, Jirama, imekuwa ikishindwa kutoa huduma hizo kikamilifu, na kusababisha kukatika kwa umeme na maji kwa saa nyingi kila siku.

Wengi waliona hatua ya kuwakamata viongozi hao kama jaribio la kunyamazisha sauti za upinzani, jambo lililozua hasira kubwa miongoni mwa raia.

Mashirika ya kiraia yalijiunga na harakati hizo, na kundi la vijana mtandaoni lijulikanalo kama Gen Z Mada likaibuka kuwa mstari wa mbele.

Maandamano yamesambaa kutoka mji mkuu Antananarivo hadi miji mingine minane kote nchini, na hakuna dalili za kutulia.

Waandamanaji wamekuwa wakibeba mabango wakilaani kukatika kwa umeme na kuituhumu serikali kwa kushindwa kutimiza wajibu wake wa msingi.

Wanaharakati pia wameikosoa Jirama kwa kile wanachodai kuwa ni ufisadi unaochochea mgogoro wa umeme.

Pia unaweza kusoma:

Nani wanaandamana?

Mwandamanaji akiwa amefunika uso kwa barakoa ameshikilia bango linalosema 'Gen Z'

Chanzo cha picha, Getty Images

Awali, Gen Z Mada walikuwa wakiratibu maandamano kupitia mitandao ya kijamii kama Facebook na TikTok.

Kamati maalum iliundwa baada ya mkutano kati ya Gen Z Mada, mashirika ya kiraia na viongozi wa kisiasa ili kupanga maandamano zaidi.

Makundi mengine yaliungana na vuguvugu hilo lilipoanza kushika kasi.

Vyama mbalimbali vya wafanyakazi, ikiwemo Umoja wa Vyama vya Wafanyakazi wa Madagascar, viliunga mkono harakati hizo zinazoongozwa na vijana.

Mashirika ya kiraia yametoa wito wa mazungumzo yanayoongozwa na makanisa ili kuzuia nchi isijikute katika machafuko au vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kiongozi wa upinzani Siteny Randrianasoloniaiko na Rais wa zamani Marc Ravalomanana waliunga mkono maandamano hayo katika taarifa ya pamoja, hatua nadra katika siasa za nchi hiyo.

Wote wawili wamekataa kujiunga na serikali ya Rajoelina, wakisema kufanya hivyo ni “usaliti kwa wananchi wa Madagascar.”

Matakwa ya waandamanaji ni yepi?

Ingawa hawajatoa waraka rasmi wa madai yao, maandamano haya yamegeuka kutoka kuwa malalamiko ya huduma duni hadi kuwa mwito wa mabadiliko ya kisiasa kwa ujumla.

Vijana wengi, wanaokumbwa na ukosefu wa ajira za kudumu na mishahara midogo, wanamtaka Rais Rajoelina ajiuzulu, wakimlaumu kwa matatizo yanayowakabili.

Siku ya Jumatano, waandamanaji walionekana wakibeba bendera na mabango yaliyoandikwa “Rajoelina jiuzulu.”

Msemaji wa Gen Z Mada aliambia shirika la habari la AFP kuwa wanataka rais ajiuzulu na pia kufanyike “usafi” katika Bunge la Kitaifa.

Pia wanamtaka Rajoelina awajibike kwa vifo vya raia waliouawa na vikosi vya usalama.

Vilevile, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wametoa wito wa kuvunjwa kwa tume ya uchaguzi na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo.

Je, majibu ya serikali ni yapi?

Mwanamume aliyevalia magwanda ya kijeshi na kinyago cheusi cha kuteleza akiwa ameshikilia bunduki ya kiotomatiki kifuani mwake.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Vikosi vya usalama vimekuwa vikitanda katika mitaa ya Antananarivo na miji mingine mikuu, huku polisi wakitumia gesi ya kutoa machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya waandamanaji.

Serikali iliweka marufuku ya kutotoka nje kuanzia jioni hadi alfajiri katika mji mkuu, kufuatia ripoti za ghasia na uporaji, ikiwemo kuchomwa kwa ofisi za wizara ya fedha.

Rais Rajoelina, alipoivunja serikali yake, aliwalaumu baadhi ya mawaziri wake kwa uzembe na kushindwa kutimiza majukumu yao.

Alitoa wito wa utulivu na kuahidi kuwa Benki ya Dunia itasaidia katika kukabiliana na tatizo la umeme.

Pia aliahidi kusaidia biashara zilizoathiriwa na uporaji na kuelezea nia ya kufanya mazungumzo na vijana.

Hata hivyo, hatua hizo hazijatosha kutuliza hasira ya raia, ambayo imechochewa zaidi na ukandamizaji wa maandamano.

Shule nyingi jijini Antananarivo na maeneo ya karibu zilifungwa wiki iliyopita kwa hofu ya kuongezeka kwa machafuko.

Mamlaka zinasisitiza kuwa mikusanyiko isiyoidhinishwa rasmi inahatarisha usalama wa umma.

Hali ya maisha Madagascar

Madagascar ni moja ya nchi maskini zaidi duniani, ambapo asilimia 75 ya watu wanaishi chini ya mstari wa umaskini, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.

Ni takriban thuluthi moja tu ya watu milioni 30 wanaopata huduma ya umeme, kwa mujibu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Mmoja wa waandamanaji aliambia AFP kuwa:

“Hali ya maisha ya wananchi wa Madagascar inazidi kuwa mbaya kila siku.”

Je, Rais Rajoelina yuko hatarini?

Mwanasiasa na mwanaharakati wa haki za binadamu Ketakandriana Raftoson alisema kuwa maandamano haya yanaweza kuendelea na kuwa makubwa zaidi endapo serikali itaendelea kutumia nguvu badala ya kuwajibika.

Alionya kuwa matokeo yanaweza kuwa mgawanyiko wa kisiasa, kuongezeka kwa hisia za utaifa dhidi ya kile kinachoonekana kama kuingiliwa kutoka nje, na pia madhara makubwa ya kiuchumi.

Hata hivyo, kwa kuanzisha marufuku ya usiku na kupuuza taarifa za vifo kutoka Umoja wa Mataifa, serikali huenda inaonyesha kuwa inaelekea kuongeza ukandamizaji badala ya kufanya maridhiano.

Wachambuzi wanasema kuwa udhibiti wa serikali kwenye vyombo vya habari na taasisi muhimu unaweza kumsaidia Rajoelina kustahimili upinzani wa sasa.

Wataalamu wa uongozi wanasema kuwa hatua ya kijeshi kukataa kutekeleza amri za kuwazima waandamanaji inaweza kuwa kipimo muhimu cha mwelekeo wa mgogoro huu.

Msemaji wa rais, Lova Ranoromaro, aliandika kwenye mitandao ya kijamii:

“Hatutaki mapinduzi ya kijeshi, kwa sababu mapinduzi huharibu taifa letu, na huharibu maisha ya watoto wetu.”

Madagascar imeshuhudia maasi kadhaa tangu ilipopata uhuru mwaka 1960, ikiwemo maandamano ya mwaka 2009 yaliyomlazimu Rais wa zamani Marc Ravalomanana kujiuzulu, na kumuingiza madarakani Rajoelina kwa mara ya kwanza.

Rajoelina alichaguliwa tena mwaka 2018 na akashinda uchaguzi wa mwaka 2023, uliosusiwa na upinzani na kuibua utata mkubwa.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *