
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema endapo ataaminiwa na Watanzania kuunda serikali, atahakikisha wilaya za Ngorongoro na Monduli zinaunganishwa kwa kiwango cha lami, sanjari na ujenzi wa barabara ndani ya wilaya hizo ili kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza Ijumaa ya Oktoba 3, 2025 jijini Karatu mkoani Arusha, Samia amesema usanifu wa barabara ya Engaruka–Ngaresero yenye urefu wa kilomita 24 umekamilika na serikali ipo katika hatua za kutangaza zabuni.
Aidha, ametaja barabara ya Selela–Engaruka yenye urefu wa kilomita 17 kuwa ipo kwenye maandalizi ya zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi atakayejenga barabara hiyo muhimu, ambayo itaunganishwa na kiwanda cha magadi soda na kutumika pia kwa shughuli za utalii katika Ziwa Natron, wilayani Monduli.