
Chanzo cha picha, AFP kupitia Getty Images
Katika miaka yako ya mapema ya thelathini, unaweza kupata maumivu kidogo ya goti wakati hali ya hewa inapobadilika, na unaweza kuhisi kukakamaa asubuhi unapoamka. Unaweza pia kusita kabla ya kuinama wakati mwingine, yote haya ni ishara kwamba viungo vyako vya magoti havina umajimaji wa kulainisha kama hapo awali.
Mambo kama vile uzito kupita kiasi, upungufu wa kingamwilini, na vinasaba – yanaweza kuongeza kasi ya matatizo ya magoti.
Maumivu ya magoti ni mojawapo ya matatizo ya mara kwa mara kwa watu wazima baada ya maumivu ya mgongo, na yanaathiri kila kitu kuanzia kutembea hadi ubora wa maisha.
Umuhimu wa magoti

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Goti ni moja ya viungo muhimu zaidi katika mwili,” anasema Anikar Chhabra, daktari wa upasuaji wa mifupa katika Kliniki ya Mayo huko Phoenix, Marekani. “Inabeba uzito wote wa mwili wetu kwa kila hatua tunayopiga.”
Tafiti zinaonyesha kuwa kudumisha uimara wa misuli ya goti, kunaweza kupunguza shinikizo kwenye kiungo hicho na kupunguza maumivu ya magoti.
Alexis Colvin, profesa wa upasuaji wa mifupa katika Kliniki ya Icahn huko Mount Sinai, New York City, anasema mazoezi yanaweza kuboresha afya ya magoti.
“Kuna maji ndani ya magoti yetu ambayo ni kama mafuta ya injini,” Colvin anaelezea. “Mazoezi husaidia kuchochea uzalishaji wa maji hayo, ambayo hupunguza ugumu na kuvimba. Pia husaidia kulainisha magoti.”
Mazoezi yanaweza pia kusaidia kuimarisha mifupa ya goti yenyewe, kupunguza hatari ya kuwa dhaifu au kukonda kwa mifupa karibu na goti.
Dk Chhabra, anasema kuimarisha goti ni muhimu hasa kwa watu wazima, kwa sababu utapata utulivu wa misuli na kupunguza hatari ya kuanguka.
Mazoezi ya goti hutoa faida nyingine zenye kushangaza—kama vile kuboresha uwezo wa kufikiri, hisia na kuuwezesha mwili kutambua mienendo, na mahali uliposimama bila kuhitaji kutazama.
“Mazoezi ya goti husaidia kuongeza ufahamu huu,” anasema Dk. Shabra. “Huuwezesha ubongo wako kuwasiliana na goti lako, kupunguza hatari ya kuanguka.”
Mazoezi sio kwa wazee tu, tafiti juu ya vijana zimegundua kuwa mazoezi ya kuimarisha magoti, hata katika umri mdogo, yana jukumu kubwa katika kupunguza hatari ya kuumia.
Colvin anasema anapendekeza watu kuanza kufanya mazoezi katika miaka yao ya 30.
Anaeleza: “huu ndio wakati tunapoanza kupoteza uzito wa misuli mifupa polepole, kwa hiyo huu ni wakati mzuri wa kuzingatia mazoezi ya kuimarisha misuli.”
Ni mazoezi gani ya kufanya?

Chanzo cha picha, Getty Images
Dk Shabra anashauri kutumia dakika 15 kwa siku, mara tatu hadi nne kwa wiki, kufanya mazoezi mbalimbali ya magoti, hasa yale ambayo yanaweza kufanywa nyumbani bila kuhitaji vifaa maalum.
Pia anapendekeza kuzungumza na mkufunzi ili kuhakikisha kuwa unaifanya kwa usahihi. Hapa kuna mazoezi muhimu ya kufanya nyumbani.
Kuruka kichura. Mazoezi haya husaidia kuimarisha goti, kupunguza maumivu, na kuboresha maisha kwa wagonjwa wenye maumivu ya magoti.
Tafiti zinaonyesha ikiwa mbinu sahihi ya mazoezi inafuatwa, hakuna hatari ya kuumia. Lakini, Shabra anasema kufanya mazoezi vibaya kunaweza kuzidisha shida za goti.
Kuinua mguu. Zoezi hili linahusisha kulalia chali au kupiga goti moja, huku ukiinua na kunyoosha mguu mwingine. Unaweza kufanya hivyo kwa sekunde kadhaa, na kisha kulishusha polepole.
Utafiti umeonyesha kuwa kuinua mguu mmoja mmoja, kunaboresha nguvu za misuli ya goti, na pia kupunguza hatari ya majeraha yanayohusiana na mazoezi.
Dk. Shabra, anaelekeza zoezi la kuimarisha misuli. “Simama kwa kusimamia vidole vyako vya mbele, na polepole inua visigino vyako huku ukiwa umeweka magoti yako sawa, fanya hivyo kwa sekunde, kisha urudi chini.”
Kwa ujumla, kuchukua muda wa kufanya mazoezi ya kuimarisha magoti ni uwekezaji muhimu katika afya ya muda mrefu.