Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amezungumza kwenye televisheni mnamo Oktoba 4, 2025. Katika hotuba yake, alizungumzia hasa mazungumzo yajayo nchini Misri kwa ajili ya kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa Gaza.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumamosi Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kwamba amewataka wajumbe wa setrikali yake katika mazungumzo kusafiri hadi Misri kufanya mazungumzo juu ya kuachiliwa kwa mateka hao wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Gaza.

“Nimeagiza timu inayofanya mazungumzo kwenda Misri kukamilisha maelezo ya kiufundi. Lengo ni kukamilisha mazungumzo kwa siku chache,” Benjamin Netanyahu alisema katika hotuba yake kupitia televisheni, bila kutaja ni lini mazungumzo hayo yatafanyika.

“Ninatumai kwamba katika siku zijazo, tutaweza kuwarudisha mateka wetu wote […] wakati wa likizo ya Sukkot,” aliongeza, akibainisha kwamba “shinikizo la kijeshi na kidiplomasia” lililazimisha Hamas kukubali kuwaachilia wale waliotekwa nyara wakati wa shambulio la kipekee la vuguvugu hilo la Kiislamu dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023. Likizo ya Kiyahudi ya Sukkot, inaanza Jumatatu, Oktoba 6, na itadumu hadi Jumatatu ya wiki inayofuata.

Wajumbe wawili wa Marekani nchini Misri

Kwa mujibu wa afisa wa Ikulu ya White House, mjumbe Steve Witkoff na mkwe wa Donald Trump, Jared Kushner, wanasafiri kuelekea Misri kukamilisha mipango ya kuachiliwa kwa mateka hao, ikiwa ni sehemu ya mpango wa rais wa Marekani uliotangazwa mwishoni mwa mwezi Septemba kumaliza vita huko Gaza. Kwa upande wake, Al-Qahera News, kituo kinachohusishwa na idara ya ujasusi ya Misri, iliripoti kwamba Israel na Hamas watafanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja mjini Cairo siku ya Jumapili na Jumatatu “kujadili kupanga masharti kwa ajili ya kubadilishana mateka na wafungwa,” ikimaanisha Wapalestina waliofungwa na Israel ambao wataachiliwa kwa kubadilishana.

Benyamin Netanyahu pia aliahidi kuwapokonya silaha Hamas, ama kupitia mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump au kwa njia za kijeshi. “Hamas itapokonywa silaha […] hii itafanyika ama kidiplomasia kupitia mpango wa Trump au kijeshi kupitia sisi,” Waziri Mkuu alitangaza. “Pia nilisema hili kwa Washington. Litakamilika kwa urahisi au kwa shida, lakini litakamilika,” alibainisha.

Wito kwa shinikizo la kiraia

Familia za mateka zina matumaini kwa uangalifu, anaripoti mwandishi wetu huko Jerusalem, Frédérique Misslin. Jana jioni, huko Jerusalem, walitoa wito wa maandamano wa watu wengi katika miji yote ya Israel. Einav Zangauqker, mama wa Matan, mateka huko Gaza, ameelezea hofu yake.

“Hatuwezi tu kumtegemea Trump,” amesema. “Lazima tuingie mitaani.” Mamake Matan ameongeza: “Tuko katika wakati mgumu. Wale wanaotaka kuhujumu mazungumzo hayo wanaweka shinikizo kwa Benjamin Netanyahu,” akimaanisha wanachama wa siasa kali za mrengo wa kulia wa muungano serikali, Bezalel Smotrich, Waziri wa Fedha na Itamar Ben-Gvir, Waziri wa Usalama wa Ndani.

Waziri Mkuu alikuwa na kikao jioni ya leo na mawaziri wake wawili. “Uamuzi wa Netanyahu ni kosa kubwa,” amesema Ben-Gvir na kuongeza: “Ikiwa Hamas itaendelea kuwepo baada ya mateka kuachiliwa, basi tutajiuzulu.”

Mzozo unaendelea. Shinikizo la kiraia litashinda? Hilo ndilo swali. Kulingana na kura za hivi punde, karibu theluthi mbili ya Waisrael wanaunga mkono mpango wa Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *