
Wapatanishi wa Israel na Palestina wanatarajiwa nchini Misri leo Jumapili, Oktoba 5. Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanatarajiwa kuanza kabla ya Jumatatu.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wajumbe wa Marekani pia wametumwa kukamilisha majadiliano kuhusu masharti ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel. Wakati huo huo siku ya Jumamosi ilikuwa siku nyingine mbaya. Huko Gaza, raia walikuwa na matumaini, lakini mashambulizi ya mabomu yaliendelea kwenye eneo hilo, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 50. Jeshi la Israel limetangaza kuwa sasa liko kwenye mkao wa kujilinda tu.
Kabla ya kuanza kwa mazungumzo nchini Misri, Donald Trump alionyesha matumaini yake: Israel imekubali kujiondoa kwenye mstari wa mbele huko Palestina. Hivi ndivyo rais wa Marekani almebainisha katika ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii, anaripoti mwandishi wetu huko Jerusalem, Frédérique Misslin. Kulingana na ramani iliyotolewa, mstari huu wa kujindoa kwa jeshi la Israel unalingana takriban na 70% ya eneo lililodhibitiwa na Israel kabla ya shambulio kuu la Gaza mwezi mmoja uliopita.
Donald Trump aliongeza kuwa “usitishwaji mapigano utaanza kutumika mara moja” mara baada ya Hamas kuthibitisha makubaliano yake, na hii itajumuisha kubadilishana mateka na wafungwa. Siku ya Jumamosi, Oktoba 4, Benjamin Netanyahu alitangaza katika hotuba ya televisheni kwamba anatarajia mateka hao kurejeshwa katika siku zijazo.
Shinikizo la kiraia
Siku ya Jumamosi, maelfu ya Waisrael waliingia barabarani kudai, kama wanavyofanya kila Jumamosi, kukomesha vita na kurudi kwa mateka. “Asante, Trump,” “Walete nyumbani,” maneno haya yaliandikwa kwenye mabango
Familia za mateka hao wanahofia kuwa mawaziri wa siasa kali za mrengo wa kulia wa muungano unaounda serikali watahujumu makubaliano hayo. Itamar Ben Gvir na Bezalel Smotrich walionya: “Usitishaji huu wa mapigano ni kosa, na ikiwa Hamas itaendelea kuwepo baada ya mateka kuachiliwa, tutajiuzulu.” Kwa upande wa Hamas, baadhi ya wachambuzi wanabainisha kwamba pia kuna migawanyiko ndani ya vuguvugu hilo la wanamgambo wa Kiislamu.
Mazungumzo juu ya kuachiliwa kwa mateka wa Israeli na wafungwa wa Kipalestina
Steve Witkoff, mjumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump katika Mashariki ya Kati, na mkwe wake Jared Kushner, wanatarajiwa kukamilisha masharti ya kuachiliwa kwa mateka wa Israel walio hai na waliofariki. Hii ni operesheni tata, kwani mateka hao wanashikiliwa katika maeneo tofauti na makundi mbalimbali ya Kiislamu ya Palestina, anaripoti mwandishi wetu mjini Cairo, Alexandre Buccianti.
Maafisa wa Misri wamevishutumu vyombo vya habari vya Israel kwa kujaribu kuchanganya suala hilo kwa kushiriki katika kampeni ya kupotosha habari, wakitolea mfano mazungumzo yaliyohusisha maafisa wa Israel katika mji wa al-Arish karibu na mpaka wa Gaza.