Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa tamko kali la kulaani kauli na video zinazodaiwa kusambazwa mitandaoni zikihamasisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujiingiza kwenye siasa kwa njia ya mapinduzi.
TEF imesema kitendo hicho ni hatari kwa utulivu wa taifa na linapongeza hatua ya haraka ya JWTZ kutoa taarifa kwa umma kukemea vikali madai hayo.
“JWTZ linapenda kuutaarifu umma wa Watanzania kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake kikatiba kwa uaminifu, utii na uhodari kwa kuzingatia kiapo chetu,” ilisema taarifa ya jeshi hilo.
Taarifa ya JWTZ ilifuatia vidio iliyosambaa mitandaoni ikumuonesha mwanajeshi aliejitambulisha kama Kapteni John Charles Tesha kutoka kikosi cha anga cha JWTZ, akihamasisha jeshi hilo kuchukua udhibiti wa nchi, huku akidai kuwa inakoelekea ni mbaya na kutoa shutuma dhidi ya viongozi wa zamani kuhusika na kifo cha aliekuwa rais wa taifa hilo John Magufuli.
Tamko la TEF limebainisha kuwa Tanzania imejenga misingi imara ya kutenganisha jeshi na siasa tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, na kwamba majaribio ya mapinduzi yaliyowahi kutokea nchini humo miaka ya 1964, 1969 na 1982 yalishindwa kutokana na hekima ya viongozi na umoja wa wananchi.
“Wanajeshi wa Tanzania hawaruhusiwi kuwa wanachama wa vyama vya siasa,” imesema TEF, katika tamko lake lililosainiwa na Mwenyekiti wake Deodatus Balile, ikiongeza kuwa msingi huo ndiyo ngao ya amani na utulivu wa taifa.
Jukwaa hilo limeonya kuwa kauli za kujaribu kuchochea uasi ndani ya jeshi ni hatari, zinavunja misingi ya kitaifa na zinaweza kusababisha machafuko kama ilivyotokea katika nchi nyingine.
Jukumu la vyama vya siasa na mitandao ya kijamii
TEF imevitaka vyama vya siasa visijihusishe kwa namna yoyote na fikra za mapinduzi kama njia ya mkato ya kushika madaraka, bali vijenge vyama imara vyenye ushindani wa kisera na vinavyoamini katika nguvu ya sanduku la kura.
Aidha, imeviasa vyama visikae kimya mbele ya matamko ya uchochezi, bali vijitokeze wazi kuyalaani kwa lengo la kulinda umoja, maisha na mali za Watanzania.
Katika tamko hilo, TEF imetoa angalizo maalum kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii, likisema majukwaa hayo yamekuwa yakitumika kusambaza taarifa za upotoshaji, picha na matusi dhidi ya viongozi.
Limewataka wananchi kuwa makini, kuchunguza ukweli kabla ya kushiriki kusambaza taarifa, na kuweka mbele maadili, uzalendo na uwajibikaji badala ya kugeuza mitandao kuwa vyanzo vya chuki na hofu.
Wito wa kulinda amani kuelekea uchaguzi
“TEF tunakemea vikali kauli za kuchochea mapinduzi, tunalipongeza JWTZ kwa uaminifu wake kwa Katiba, na tunawasihi Watanzania wote kulinda amani na umoja wa taifa letu, muda wote,” limesema jukwaa hilo katika tamko lililosainiwa na mwenyekiti wake Deodatus Balile mnamo Oktoba 5, 2025.
Wakati Tanzania ikiekelea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, hali ya kisiasa imekuwa ya joto zaidi, hasa baada ya chama kikuu cha upinzani Chadema kukataa kushirikia uchaguzi huo kikidai mageuzi makubwa katika mfumo wa uchaguzi na kushinikiza kuwepo na katiba mpya.
Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu ambaye aliwania nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka 2020 dhidi ya hayati John Magufuli, anakabiliwa na kesi ya uhaini ambayo inaambatana na adhabu ya kifo.
Malumbano makali yanashuhudiwa kwenye mitandao ya kijamii ambapo wafuasi wa upinzani wamekuwa wakiitumia kuelezea hasira zao, lakini wakati mwingine hutumia mitandao hiyo kutoa maneno ya kuwadhalilisha viongozi wa sasa na wa zamani wakiwashtumu kuipeleka kubaya nchi hiyo.
