Utawala wa Trump umeitangaza Chicago kuwa “eneo la vita” Jumapili kama sababu ya kuhalalisha kutuma wanajeshi kinyume na matakwa ya viongozi wa eneo hilo wanaotoka chama cha Democratic, huku jaji akizuia Ikulu ya White House kutuma wanajeshi katika jiji jingine linaloongozwa na Wademocrat.
Mzozo wa kisiasa unaendelea kushika kasi nchini Marekani, ukiwahusisha Rais Donald Trump anayefanya msako dhidi ya uhalifu na uhamiaji haramu na chama cha upinzani cha Democratic, ambacho kinamtuhumu kwa kutaka kujitwalia mamlaka kwa misingi ya kiimla.
Katika hatua mpya ya mvutano huo, Jumamosi usiku Trump aliidhinisha kutumwa kwa askari 300 wa Jeshi la Walinzi wa Taifa (National Guard) kwenda Chicago — jiji la tatu kwa ukubwa Marekani — licha ya kupingwa na viongozi waliochaguliwa akiwemo meya na gavana wa jimbo, JB Pritzker.
Waziri wa Usalama wa Ndani, Kristi Noem, alitetea uamuzi huo Jumapili kupitia Fox News akidai kuwa “Chicago ni eneo la vita.”
Lakini Gavana Pritzker, akizungumza katika kipindi cha “State of the Union” cha CNN, aliwashutumu Warepublican kwa kutaka “kuleta vurugu ndani ya jiji hilo.”
“Wanataka kuunda eneo la vita ili wapate kisingizio cha kutuma wanajeshi zaidi,” alisema, akiongeza: “Wanapaswa kuondoka kabisa.”
Utafiti wa maoni wa CBS uliochapishwa Jumapili ulionyesha kwamba asilimia 42 ya Wamarekani wanaunga mkono kutumwa kwa walinzi wa taifa mijini, huku asilimia 58 wakipinga hatua hiyo.
Trump — ambaye wiki iliyopita alizungumza kuhusu kutumia jeshi kwa “vita vya ndani” — anaonekana kutokuwa na mpango wa kuachana na msimamo wake mkali.
Katika kauli isiyo sahihi aliyoitoa Jumapili, alisema: “Portland inateketea kwa moto. Ni waasi kila mahali.”
Mshirika wake wa karibu, Mike Johnson, Spika wa Baraza la Wawakilishi, alirudia maneno hayo Jumapili kwenye kipindi cha “Meet the Press” cha NBC, akisema wanajeshi wa National Guard waliotumwa katika mji mkuu, Washington, walikuwa wakikabiliana na “eneo halisi la vita.”
Hapana kwa ‘sheria ya kijeshi’
Hata hivyo, kampeni ya Trump ya kutumia jeshi ndani ya nchi ilikumbwa na pingamizi Jumamosi usiku huko Portland, Oregon, baada ya mahakama kuamua kuwa hatua hiyo ilikuwa kinyume cha sheria.
Trump amekuwa akiita Portland “mji uliokumbwa na vita,” lakini Jaji wa Mahakama ya Wilaya, Karin Immergut, alitoa zuio la muda akisema: “Uamuzi wa rais haukuwa na msingi wowote wa ukweli.”
“Hii ni nchi ya utawala wa Katiba, si ya sheria ya kijeshi,” aliandika jaji huyo katika uamuzi wake.
Ingawa Portland imeshuhudia mashambulizi madogo dhidi ya maafisa na mali za serikali, serikali ya Trump ilishindwa kuthibitisha “kwamba matukio hayo ya vurugu yalikuwa sehemu ya jaribio lililopangwa la kuipindua serikali kwa ujumla” — jambo ambalo lingehalalisha matumizi ya nguvu za kijeshi, alisema jaji.
Mshauri wa karibu wa Trump, Stephen Miller, aliuita uamuzi wa jaji huyo kuwa “uasi wa kisheria.”
Tukio la risasi Chicago
Mbali na kutuma wanajeshi, kampeni ya Trump ya kudhibiti uhalifu inaongozwa na Idara ya Uhamiaji na Forodha (ICE), ambayo imepanuliwa haraka kwa kuongeza watumishi na majukumu mapya.
Misako ya ICE katika miji mbalimbali — hasa inayoongozwa na Democrats — imehusisha makundi ya wanaume waliovaa barakoa, wakiwa na silaha katika magari yasiyo na alama, wakilenga mitaa ya makazi na biashara, jambo lililosababisha maandamano.
Hali ya taharuki katika mjini wa Chicago iligeuka kuwa vurugu Jumamosi wakati afisa wa serikali ya shirikisho alipompiga risasi dereva ambaye Wizara ya Usalama wa Ndani (DHS) ilisema alikuwa amejihami na kujaribu kugonga gari lao la doria.
Maafisa wa DHS wamesema pia maafisa wa ICE walimpiga risasi na kumuua Silverio Villegas Gozalez, mwenye umri wa miaka 38, wakati wa ukaguzi wa magari mnamo Septemba 12, wakimtuhumu kwa kujaribu kukimbia eneo la tukio na kumvuta afisa wa ICE na gari lake.
Chanzo: AFP