Kikosi cha Nane cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TANBAT 08) kinacholinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) chini ya mwavuli wa MINUSCA, kimetunukiwa nishani za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa (UN) kwa mchango wake mkubwa katika operesheni za kudumisha amani.
Hafla hiyo ilifanyika tarehe 6 Oktoba mwaka huu mjini Berberati, ambapo wanajeshi zaidi ya 500 walipokea tuzo hizo kama ishara ya kutambua juhudi zao katika kuwalinda raia na kuimarisha utulivu katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.
Naibu Mkuu wa Vikosi vya Kulinda Amani vya Umoja wa Mataifa nchini CAR, Meja Jenerali Maychel Asmi, amewapongeza wanajeshi wa TANBAT 08 kwa nidhamu, uongozi na mshikamano wao wa kipekee.
‘
Amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika operesheni za ulinzi wa amani duniani kutokana na weledi wa wanajeshi wake na ushirikiano mzuri na wananchi wa maeneo wanayohudumia.
Kamanda wa TANBAT 08, Luteni Kanali Theofil Nguruwe, amesema nishani hizo ni heshima kubwa kwa JWTZ na taifa kwa ujumla, akibainisha kuwa kikosi chake kimehudumu kwa weledi, uaminifu na moyo wa kizalendo.
Kwa zaidi ya miongo mitatu, Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa mataifa kinara duniani katika kutoa vikosi bora vya ulinzi wa amani, ikithibitisha dhamira yake ya kuchangia utulivu na usalama wa kimataifa kupitia ushiriki wake katika operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa.
#AzamTVUpdates
✍Mariam Songoro
Mhariri | John Mbalamwezi