
Ikulu ya Élysée jana Jumapili imetangaza majina ya mawaziri 18, huku nafasi nyingi muhimu zikiendelea kushikiliwa na waliokuwa wakizishikilia awali. Nafasi ya zamani ya Lecornu kama waziri wa ulinzi itachukuliwa na Bruno Le Maire, aliyekuwa waziri wa uchumi na ni mwanachama wa chama Rais Emmanuel Macron. Kuna mabadiliko pia katika Wizara ya Uchumi, ambapo makamu wa rais wa zamani wa Bunge la Kitaifa, Roland Lescure, anachukua nafasi ya Éric Lombard. Jean-Noël Barrot anasalia kuwa waziri wa mambo ya nje, huku Bruno Retailleau wa mrengo wa kihafidhina akiendelea kuwa waziri wa mambo ya ndani. Gérald Darmanin, aliyewahi kuhudumu kwa miaka mingi kama waziri wa mambo ya ndani na kwa sasa anaongoza Wizara ya Sheria, pia anabaki katika nafasi hiyo. Waziri mkuu wa zamani Élisabeth Borne anabaki kuwa waziri wa elimu. Hotuba ya serikali ya Lecornu katika Bunge la Kitaifa na tangazo la nusu ya pili ya Baraza lake la Mawaziri vinatarajiwa kutolewa Jumanne.