.

“Amuachie mwanangu (Humphrey Polepole). Kama yupo hai, kama hayupo hai waniletee nizike mwenyewe wasiende kumtupa baharini,” amesema Anna Mary, ambaye ni mama mzazi wa Humphrey Polepole.

Akizungumza na BBC, mama huyo ameiomba Serikali na Jeshi la Polisi nchini Tanzania kufanya jitihada za kuhakikisha mwanae anapatikana.

“Naomba watusaidie apatikane, kama polisi wanajua au hawajui, watusaidie…inasikitisha sana,” alisema mama huyo.

Humphrey Polepole ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana siku ya Jumatatu Oktoba 06, 2025.

Anna Mary anasema, ” Unamsomesha mtoto tangu kichanga hadi amefika mahali unaona anaweza kukusaidia kupata kipande cha khanga, alafu leo wanakuja kukatia msaada ghafla…

“…huyu mtoto nikikwambia siri yake tangu alipozaliwa, alikuwa mtoto wa pekee kabisa, kwanza alipenda kusomea uchungaji na urubani wa ndege lakini sisi wazazi hatukuwa na uwezo wa kumsomesha,” alisema.

Polisi waanza uchunguzi

Mapema leo, Jeshi la polisi litoa taarifa kuwa imefungua jalada rasmi la uchunguzi wa tuhuma za kutekwa kwa mwanadiplomasia huyo.

Katika taarifa ya jeshi hilo, ilieleza kuwa inamtafuta Augustino Polepole (kaka wa Humphrey) ili aweze kutoa ushirikiano na kutoa maelezo ya uthibitisho wa shutuma alizotoa kwamba ofisa wa polisi alihusika katika tukio alilolitolea taarifa katika mitandao ya kijamii

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa inafuatilia uthibitisho kuwa Humphrey Polepole alikuwa mkazi wa nyumba inayodaiwa utekaji kutendeka.

Polepole alijiuzulu nafasi ya ubalozi na kuvuliwa rasmi hadhi ya ubalozi kufuatia kutenguliwa kwa uteuzi wake na Rais Samia Suluhu Hassan.

Uamuzi wake ulifuatia kile alichoeleza kutoridhishwa na mwenendo wa mambo mbalimbali nchini Tanzania akidai hawezi kuwa sehemu ya serikali isiyojali misingi ya haki, sheria na katiba ya nchi.

Ukosoaji wa serikali na CCM

Hata baada ya kujiuzulu na kuvuliwa hadhi ya ubalozi, Polepole aliendeleza harakati zake za ukosoaji wa serikali na chama tawala nchini Tanzania CCM.

Pamoja na masuala mengine Polepole alikosoa utaratibu uliotumika kumteua Samia na Dkt Emmanuel Nchimbi kuwa wagombea wa urais na Makamu wa rais katika uchaguzi mkuu unaopangwa kufanyika Oktoba 29.

“Uchaguzi ule ulikiuka desturi ya CCM inayokifanya chama kuendelea kuwa imara” alisema Polepole.

Haikupita muda, Polepole akaendelea kuporomosha tuhuma moja baada ya nyingine huku akiwataja bayana watu mbalimbali, baadhi yao mashuhuri kwa tuhuma za ufisadi na kujinufaisha na fedha umma kinyume cha taratibu.

Kwa namna ya pekee alikuwa gumzo kwelikweli mtandaoni. Wapo waliompongeza kwa dhati kwa ujasiri wake, pia wapo waliomponda, kumbeza na kumbagaza wakidai hakuwa na hadhi ya kuzungumzia aliyoyaweka hadharani maana alikuwa sehemu ya CCM wakati wa rais Magufuli, na sehemu ya serikali wakati wa Rais Samia. Baadhi ya waliotuhumiwa walijibu pia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *