t

Chanzo cha picha, REUTERS/Jonathan Ernst

“Mimi nilizuia vita saba,” alisema Rais wa Marekani, Donald Trump, alipohutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni akirudia kauli ambayo ameitoa mara kadhaa hapo awali.

Hata hivyo, kauli hiyo imepingwa vikali na watu wengi, huku kikosi maalum cha BBC kinachofuatilia ukweli kikichapisha makala yaliyouliza kama kweli Trump alihusika moja kwa moja kusitisha vita hivyo.

Pamoja na utata huo, uteuzi wa Trump kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka huu umeungwa mkono na baadhi ya viongozi mashuhuri wa kimataifa.

Siku chache kabla Kamati ya Nobel kutangaza mshindi wa mwaka huu, kundi moja linalopigania kuachiliwa kwa mateka waliokuwa wakishikiliwa na Hamas huko Gaza kwa miaka miwili, lilimpendekeza Trump apokee tuzo hiyo.

Kundi hilo lilisema kuwa Trump anastahili tuzo hiyo “kwa mchango wake mkubwa katika amani ya dunia.” Liliandika barua kwa Kamati ya Nobel ya Norway, likieleza kuwa mpango wa Trump wa kumaliza mgogoro wa Gaza unajumuisha pia kuachiliwa kwa mateka.

“Kwa mara ya kwanza baada ya miezi mingi, tuna matumaini kuwa jinamizi letu litakwisha,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.

Kwa sasa, Hamas inashikilia mateka 48 katika Ukanda wa Gaza, ambapo inasadikiwa kuwa 20 kati yao bado wako hai.

Chini ya mpango wa Trump, mateka hao wangetolewa kwa kubadilishana na mamia ya wafungwa wa Kipalestina walioko magerezani.

“Katika kipindi cha mwaka uliopita, hakuna kiongozi wala taasisi yoyote iliyochangia amani duniani zaidi ya Rais Trump,” waliandika.

Mnamo tarehe 7 Oktoba 2023, wanamgambo wa Kipalestina wakiongozwa na Hamas walivamia maeneo ya kusini mwa Israel, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 kuchukuliwa mateka.

Jeshi la Israel lilijibu kwa mashambulizi makali kwa anga na baadaye kwa vikosi vya ardhini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas, watu zaidi ya 66,000 wameuawa tangu operesheni hiyo ianze.

Mwezi Agosti, chombo cha Umoja wa Mataifa kilithibitisha kuwepo kwa baa la njaa mjini Gaza madai ambayo Israel ilikanusha.

Mapema mwezi Oktoba, tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilihitimisha kuwa Israel imefanya mauaji ya kimbari (genocide) huko Gaza.

Soma pia:

Nani alimteua Trump kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel?

Uteuzi wa Trump ulianza nchini Pakistan.

Tarehe 21 Juni, serikali ya Pakistan ilitangaza kuwa inapanga kumteua Trump kuwania Tuzo ya Amani ya Nobel, ikieleza kuwa alisaidia kusuluhisha mzozo wa muda mfupi kati ya India na Pakistan.

Kupitia taarifa rasmi iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, serikali hiyo ilisema:

“Trump anastahili tuzo hiyo kwa kutambua uongozi wake wa kidiplomasia na mchango wake muhimu katika kutuliza mgogoro wa hivi karibuni kati ya India na Pakistan.”

Hata hivyo, India ilikanusha kuwa Marekani ilihusika katika kusitisha mzozo huo wa kijeshi ulioibuka mwezi Mei.

Aidha, Pakistan haikufafanua kama iliwahi kuwasilisha rasmi uteuzi huo kwa Kamati ya Nobel.

Wanaomuunga mkono

Mwezi Agosti, wazo la Trump kupewa Tuzo ya Amani liliungwa mkono na Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev, na Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan.

Baada ya viongozi hao wawili kusaini makubaliano ya amani jijini Washington mbele ya Trump kumaliza mzozo wa miongo mingi kuhusu eneo la Nagorno-Karabakh, walieleza kuwa Rais wa Marekani anapaswa kupewa Tuzo ya Nobel.

“Rais Trump ametekeleza muujiza ndani ya miezi sita,” alisema Aliyev.

Baadaye, mawazo hayo yaliungwa mkono pia na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, pamoja na Rais wa Gabon, Brice Olighi Nguema.

Je, Trump ana nafasi ya kushinda Tuzo ya Nobel mwaka huu?

Mwandishi wa BBC mjini Washington, Bernd Debusman Jr., anasema kwamba si siri kuwa Rais Trump anatamani sana kupata Tuzo ya Amani ya Nobel.

Hata hivyo, alipoulizwa maoni yake kuhusu mapendekezo yote yaliyotolewa kumhusu, Trump alisema mnamo tarehe 4 Septemba:

“Sina la kusema kuhusu hilo.”

“Ninachofanya ni kuzuia vita.”

“Sitafuti sifa; ninachotaka ni kuokoa maisha,” alisema katika mahojiano na CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani.

Kwa mujibu wa wasia wa Alfred Nobel muasisi wa tuzo hizi Tuzo ya Amani hutolewa kwa mtu aliyefanya juhudi kubwa au bora zaidi katika kuendeleza amani baina ya mataifa.

Mara ya mwisho kwa Rais wa Marekani kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel ilikuwa mwaka 2009, ambapo Barack Obama alipewa heshima hiyo.

Mwaka huu, Kamati ya Nobel ilipokea jumla ya uteuzi 338. Wajumbe watano wa Kamati hiyo sasa wanateua mshindi wa mwaka huu.

Ingawa wanachama wengi wa Kamati ya Nobel wanajulikana kuwa wapinzani wa kisiasa wa Trump, sababu kuu ya yeye kukosa nafasi mwaka huu ni ya kiutaratibu.

Tarehe ya mwisho ya kuwasilisha majina ya wagombea ilikuwa mwezi Januari, wakati Trump alikuwa tu ameanza kampeni zake za kugombea urais kwa muhula mwingine.

Hivyo, uteuzi wowote uliotolewa baada ya muda huo unaweza tu kuzingatiwa kwa Tuzo ya Amani ya mwaka 2026.

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka huu atatangazwa rasmi tarehe 10 Oktoba.

Pia unaweza kusoma:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *