
Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Na Rehema Mema
- Nafasi, Mwandishi
Kila baada ya miaka mitano, macho ya Watanzania na hata ya mataifa jirani huishia Zanzibar. Ingawa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uchaguzi wa Zanzibar hujitofautisha kwa njia nyingi za kipekee zinazofanya matokeo yake kuwa na uzito mkubwa zaidi ya kura. Tofauti hizo zimejikita katika mfumo wa kikatiba, historia ya kisiasa na namna kura zinavyopigwa.
Uchaguzi wa mwaka 2025 haupo mbali, na mara nyingine tena Zanzibar itakuwa kitovu cha mijadala. Ni uchaguzi ambao si tu unahusu nani ataongoza visiwa hivi, bali pia unaonyesha namna taifa linavyoshughulika na urithi wa mfumo wa Muungano na historia ya migogoro.
Serikali mbili, katiba mbili, Tume mbili na kura mbili
Tofauti ya kwanza ya msingi ni muundo wa kikatiba. Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia ni nchi yenye mamlaka ya ndani chini ya Katiba yake. Hii inamaanisha kuwa wakati upande wa Tanzania bara ukiongozwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Zanzibar pia inatumia Katiba yake ya mwaka 1984 ambayo inampa Rais wa Zanzibar mamlaka makubwa katika masuala ya ndani.
Kutokana na hali hii, uchaguzi wa Zanzibar huendeshwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), tofauti na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inayosimamia Tanzania. Hii ndiyo sababu visiwa vinaingia katika uchaguzi wake wa Rais wa Zanzibar na wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi huku pia vikishiriki uchaguzi wa Rais wa Muungano, wabunge na madiwani unaosimamiwa na INEC. Kwa ujumla, wananchi wa Zanzibar hupiga kura tano: Rais wa Muungano, mbunge, diwani, Rais wa Zanzibar, na Mwakilishi wa Jimbo. Tanzania bara, wapiga kura wanapiga kura tatu peke , ya Rais wa Jamuri ya Muungano, mbunge na diwani.
Aidha, Zanzibar imekuwa na utaratibu wa kipekee wa kura ya mapema kwa makundi maalumu kama askari na watendaji wanaohusiana na uchaguzi, jambo ambalo halijazoeleka bara. Hili limekuwa likichukuliwa kama njia ya kuhakikisha usalama na ufanisi, lakini pia limeibua mijadala ya kisiasa kuhusu uwazi na usawa. Wapinzani wanaona kama inaweza kutumika kufanya udanganyifu wa kura.
Ushindani mkali kuliko bara

Chanzo cha picha, IkuluZanzibar
Katika historia ya vyama vingi, chaguzi za Zanzibar mara nyingi zimekuwa na mvutano mkali zaidi kuliko za Tanzania bara. Hii inachangiwa na mambo mawili: udogo wa visiwa na uzito wa historia ya kisiasa. Zanzibar ikiwa na idadi ndogo ya wapiga kura ikilinganishwa na Tanzania bara, inakuwa rahisi kwa kila kura kuonekana kuwa na uzito mkubwa.
Hali hii imeifanya chaguzi za Zanzibar kuwa na ushindani mkali kati ya CCM na vyama vya upinzani. Tofauti ya kura mara nyingi ni ndogo sana, lakini hisia zinazozuka huwa kubwa mno. Karibu kila uchaguzi tangu mwaka 1995 umekuwa ukibishaniwa, mara nyingine ukisababisha ghasia au mivutano mikali ya kisiasa.
Tofauti kubwa na bara ni kwamba uapnde wa bara mara nyingi CCM hukabiliana na upinzani usio na nguvu ya kudumu kitaifa, Zanzibar imekuwa na upinzani thabiti na wa kihistoria, ulioongozwa na marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kwa zaidi ya robo karne. Kwa maana hiyo, ushindani wa Zanzibar si tu juu ya kura, bali juu ya heshima ya vyama na mustakabali wa siasa za kidemokrasia nchini. Inasubiriwa kwa hamu kuona utakuwa uchaguzi wa aina gani, ukifanyika kwa mara ya kwanza bila Maalim Seif aliyefariki mwanzoni mwa mwaka 2021.
Aidha, kutokana na ukubwa mdogo wa visiwa, siasa za Zanzibar huwa za karibu sana na wananchi. Mgombea anaweza kuwafikia wapiga kura ana kwa ana, na hivyo kujenga hisia za karibu zaidi. Hili limechangia chaguzi kuwa na mvuto wa pekee na wakati mwingine kusababisha hisia kali zaidi kuliko za Tanzania bara.

Chanzo cha picha, Getty Images
Historia ya migogoro ya kisiasa
Hakuna sehemu katika Tanzania ambayo historia ya uchaguzi imeandikwa kwa wino mzito wa migogoro kama Zanzibar. Tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, karibu kila uchaguzi umekumbwa na malalamiko ya vurugu, udanganyifu au hila za matokeo. Hali hii imeifanya Zanzibar kuwa kitovu cha mijadala kuhusu demokrasia ya Tanzania.
Kwa mfano, uchaguzi wa 2000 ulimalizika kwa maandamano makubwa yaliyosababisha vifo vya watu kadhaa. Hali kama hiyo ilijirudia mwaka 2015, ambapo matokeo ya uchaguzi yalifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, jambo lililoibua taharuki kubwa. Kila mara, Zanzibar imejikuta katikati ya shinikizo la kisiasa ndani na nje ya nchi.
Migogoro hii pia imekuwa chanzo cha kuundwa kwa serikali za maridhiano na hatimaye Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ambapo mshindi wa kwanza na wa pili wa urais huunda serikali pamoja. Huu ulikuwa mpango wa kipekee wa kupunguza mivutano ya kisiasa. Lakini hata ndani ya mfumo huo, changamoto zimeendelea, kwani baadhi ya wapinzani wameona bado hawanufaiki ipasavyo. Huku nafasi ya Makamu wa Rias ambayo imekuwa chini ya upinzani kama nguvu yake sio kubwa sana.
Hii historia ndefu ya migogoro imeifanya Zanzibar kuwa mfano wa namna siasa za ushindani zinavyoweza kuleta changamoto kubwa katika taifa dogo. Hata hivyo, imeiweka pia mbele kama kielelezo cha mapambano ya kidemokrasia, na kila uchaguzi mpya huonekana kama kipimo cha utulivu na maridhiano ya visiwa hivi.