
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Waisraeli wamekusanyika nchini kote kuadhimisha
miaka miwili tangu shambulio lililoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023, huku
mazungumzo yakiendelea nchini Misri kuhusu kumalizika kwa vita huko Gaza.
Shambulizi hilo lilishuhudia zaidi ya watu 1,200
wakiuawa na wengine 251 kurudishwa Gaza kama mateka. Ilikuwa siku moja mbaya
zaidi kwa Wayahudi tangu mauaji ya Holocaust.
Israel ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi ya
kijeshi huko Gaza ambayo yameua zaidi ya watu 67,000, kulingana na wizara ya
afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Takwimu zake zinaonekana kuwa
za kuaminika na UN na mashirika mengine ya kimataifa.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu
alisema katika taarifa yake kwamba pamoja na “maumivu makubwa”,
Israel imeonesha “ustahimilivu wa kimiujiza”.
Wakati huo huo, timu za
mazungumzo za Israel na Hamas zilikutana katika eneo la mapumziko la Bahari ya Shamu
la Misri la Sharm el-Sheikh kwa siku ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa
moja kujadili masharti ya pendekezo hilo.
Afisa mkuu wa Palestina
anayefahamu mazungumzo hayo aliiambia BBC kwamba kikao cha asubuhi kilimalizika
bila matokeo yanayoonekana, huku kukiwa na kutoelewana kuhusu mapendekezo ya
ramani ya Israel ya kujiondoa kutoka Gaza na juu ya dhamana ya Hamas inataka
kuhakikisha Israel haianzishi tena mapigano baada ya awamu ya kwanza ya mpango
huo.
Aliongeza kuwa mazungumzo hayo
ni “magumu na bado hayajaleta mafanikio yoyote ya kweli,” lakini
alibainisha kuwa wapatanishi wanafanya kazi kwa bidii ili kupunguza mapengo
kati ya pande hizo mbili.
Hapo awali, afisa wa Palestina
alisema mazungumzo hayo yalilenga katika masuala matano muhimu: usitishaji vita
wa kudumu; kubadilishana mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas kwa wafungwa
wa Kipalestina na wafungwa kutoka Gaza; kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka
Gaza; mipango ya utoaji wa misaada ya kibinadamu; na utawala wa baada ya vita
wa eneo hilo.
Unaweza kusoma;