Kongamano hilo la siku tatu limejadili namna teknolojia inaweza kuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa kikanda, huku wakuu wa nchi wakihimiza ushirikiano wa karibu katika miundombinu ya kidijitali, usafiri na mfumo wa malipo wa pamoja.

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano, Rais William Ruto, ambaye sasa ndiye mwenyekiti mpya wa COMESA, alisisitiza kuwa Afrika haiwezi kuendelea kutegemea mifumo ya zamani ya kibiashara. Amesema ni wakati wa kupitisha hati na taratibu za kielektroniki, kuunganisha majukwaa ya malipo ya mipakani, na kuhakikisha bidhaa za kikanda zinanufaika na teknolojia ya kisasa.

“Sharti tuimarishe matumizi ya mifumo ya kidijitali katika biashara, kuwekeza kwa pamoja kwenye miundombinu na majukwaa ya malipo ya mipakani, ili kulifanya eneo letu kuwa imara na lenye ushindani zaidi katika biashara barani Afrika”, alisema Ruto.

Tayari nchi kama Eswatini, Malawi, Zambia na Zimbabwe zimeanza kutumia hati za kielektroniki katika biashara ya mipakani, hatua iliyopunguza muda wa usafirishaji kwa zaidi ya asilimia 80 na gharama kwa nusu.

Kuunganisha watu milioni 180 na huduma za kidijitali 

Bunge la Ethiopia mjini Addis Abeba
Mkutano wa 24 wa kilele wa COMESA umefanyika jijini Nairobi na kuwaleta pamoja viongozi kutoka nchi 21 wanachama, wakiwemo marais, mawaziri wakuu na wadau wa sekta binafsiPicha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance

Katibu Mkuu wa COMESA, Chileshe Mpundu Kapwepwe, amesema juhudi za kuwaleta wanawake na vijana kwenye mifumo ya biashara za kidijitali zimepiga hatua kubwa kupitia mradi wa pamoja wa COMESA na Benki ya Dunia wenye thamani ya dola bilioni 2.5.

“Mradi wa pamoja wa COMESA na Benki ya Dunia wenye thamani ya dola bilioni 2.5 unaendelea mwaka huu, ukilenga kuwaunganisha watu milioni 180 na huduma za kidijitali ifikapo mwaka 2030, ukiwapa kipaumbele wanawake, vijana, wakimbizi na mashirika ya umma.”

Mradi huo unalenga kuunganisha watu milioni 180 na huduma za kidijitali ifikapo mwaka 2030, ukiwapa kipaumbele wanawake, vijana, wakimbizi na mashirika ya umma.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Rais wa Burundi na mwenyekiti anayeondoka wa COMESA, Evariste Ndayishimiye, pamoja na Rais Azali Assoumani wa Comoro, Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe (naibu mwenyekiti mpya), Waziri Mkuu Ahmed Abiy wa Ethiopia, Russell Mmiso Dlamini wa Eswatini na Mustafa Madbouly wa Misri.

Kwa mujibu wa COMESA, biashara baina ya nchi wanachama imeongezeka hadi kufikia dola bilioni 14, ikichochewa na uwekezaji katika miundombinu na mageuzi ya kidijitali.

Kenya, ambayo sasa inaongoza jumuiya hiyo, imeahidi kutumia nafasi hiyo kusukuma mbele ajenda ya biashara huru ya bara la Afrika kupitia mkataba wa jumuiya za COMESA–EAC–SADC, eneo linalotajwa kuwa soko kubwa zaidi barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *