Urusi ilisema siku ya Alkhamis (Oktoba 9) kuwa ilikuwa imefurahishwa na hatua hiyo, ambapo kwa msemaji wa Ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, alinukuliwa na shirika la habari la TASS akibainisha uungaji mkono kikamilifu wa Rais Vladimir Putin kwa  “makubaliano kati ya Israel na Hamas  juu ya awamu ya kwanza ya kuumaliza mgogoro wa Gaza.”

Saudi Arabia, taifa tajiri zaidi miongoni mwa mataifa ya Kiarabu na yenye Waislamu wengi, ilisema kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni kwamba ilikuwa inatarajia hatua hiyo muhimu ingelipelekea kwenye amani ya kudumu.

 “Tunatarajia kutakuwa na hatua za haraka kukomesha mateso yanayowasibu Wapalestina, kukamilisha kuondoka kikamilifu kwa wanajeshi wa Israel kwenye ardhi ya Palestina, kurejesha usalama na utulivu na kuanzisha hatua za vitendo ili kufikia amani kamili iliyojikita kwenye suluhisho la madola mawili huru.” Ilisema wizara hiyo.

Ujerumani yafurahia kuachiwa mateka

Ujerumani  – ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa Israel – ilielezea kutiwa moyo na maendeleo yaliyopatikana kwenye hatua hii, huku Kansela Friedrich Merz akisema hatimaye kulikuwa na matumaini ya mateka wote wa Israel walio mikononi mwa wanamgambo wa Kipalestina watarudi nyumbani.

Israel Tel Aviv 2025 | makubaliano ya Gaza | Hostage Square
Waisraili wakionesha hisia zao baada ya kutangazwa kwa makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya jeshi la nchi yao na wanamgambo wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza siku ya Alkhamis (9 Oktoba 2025).Picha: Maya Levin/AFP/Getty Images

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba mateka hao wataachiliwa wiki hii na kwamba jeshi la Israel litaondoka kwenye Ukanda wa Gaza kama ilivyokubalika kwenye mpango huo wa vipengele 20 wa Rais wa Marekani na serikali ya Israel.” Alisema Kansela Merz.

Mbali na kupongeza kufikiwa kwa makubaliano hayo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer , aliyekuwa ziarani nchini India, alisema “sasa ni wakati wa makubaliano hayo kutekelezwa kikamilifu bila kuchelewa na kufuatiwa na uondoshwaji wa vikwazo vyote vinavyokwamisha kufikishwa kwa misaada ya kibinaadamu kwenye Ukanda wa Gaza.”

Ulaya yaahidi kusaidia utekelezaji

Rais wa Kamisheni ya Ulaya , Ursula von der Leyen, alizitaka pande zote kuheshimu vifungu vyote vya makubaliano hayo, huku mkuu wake wa sera za nje, Kaja Kallas, akiandika kwenye mtandao wa X kwamba “Umoja wa Ulaya utafanya kila uwezalo kusaidia utekelezwaji wa mpango huo.”

Palestina Khan Younis 2025 | Hamas na Israel
Wapalestina kwenye kitongoji cha Khan Younis, Ukanda wa Gaza, wakifurahia kutangazwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na makundi ya wanamgambo wa Kipalestina siku ya Alkhamis (9 Oktoba 2025).Picha: AFP/Getty Images

Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, aliyaita makubaliano hayo kuwa habari njema zisizo za kawaida, naye pia akitoa wito wa utekelezwaji wake kikamilifu, huku Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uholanzi, David van Weeel, akielezea matumaini yake kwamba makubaliano haya sasa yangelikuwa “chanzo cha kupatikana amani kwenye eneo zima la Mashariki ya Kati.”

Qatar, Uturuki na Misri, ambazo pamoja na Marekani, zimekuwa wapatanishi wakuu, zilisema sasa makubaliano hayo yanaingia hatua muhimu ya utekelezaji. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *