Badala yake limetangaza mgomo pamoja na maandamano mapya siku ya Alhamisi. Maandamano ya karibu kila siku yalianza katika kisiwa hicho maskini cha Bahari ya Hindi mnamo Septemba 25, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 22, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa ambazo zinapingwa na mamlaka za ndani.
Rajoelina aliifukuza serikali yake yote wiki iliyopita na kumteua jenerali wa jeshi kuwa waziri mkuu siku ya Jumatatu, kisha akaitisha mkutano wa hadhara katika ikulu ya rais siku ya Jumatano ambapo alisikiliza malalamiko kutoka kwa washiriki kadhaa.
Vuguvugu la Gen Z Madagascar linaloongoza maandamano hayo halikuhudhuria mkutano huo, likieleza kuwa maandamano hayo yalisababishwa na hasira juu ya kukatika kwa umeme na maji mara kwa mara.
Akizungumza na baadhi ya wanachama wa makundi ya kiraia, Rajoelina aliahidi kushughulikia suala la kukatika kwa umeme:
“Nawambia, mbingu na ardhi ni mashahidi, mbele za Mungu nawambia: ndani ya mwaka mmoja, ikiwa bado kutakuwa na kukatika kwa umeme Antananarivo, nitaachia madaraka kama Rais wa Jamhuri.
“Tunakataa mazungumzo haya ya kinafiki,” kundi la Gen Z liliandika kwenye mitandao ya kijamii, likikosoa kile kinachotajwa kama “serikali inayokandamiza, kudhalilisha na kuumiza vijana mitaani.”
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa wanafunzi walioko mstari wa mbele katika maandamano alihudhuria mkutano huo na kumwambia rais, “Ni sera gani mtakayoweka kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaomaliza masomo yao wanapata ajira baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu? Wanafunzi hujiunga na ENS, taasisi inayofundisha walimu kwa lengo la kuwa walimu. Lakini wengi wao hawaishii kufundisha; badala yake wanakuwa wauzaji wa nyanya kwa sababu hawawezi kupata kazi katika utumishi wa umma.”
Miongoni mwa hatua ambazo tayari rais Rajoelina amechukua ni kuteua mawaziri wapya kuongoza wizara tatu zinazohusiana na jeshi, usalama wa umma na polisi, akisema nchi hiyo “haitaki tena vurugu bali amani.”
Matakwa ya Gen Z
Lakini viongozi wa maandamano wamesema uteuzi huo ni changamoto kwao na wametangaza mgomo wa maandamano mapya katika mji mkuu wa Antananarivo siku ya Alhamisi. Aidha vuguvugu hilo linalojumuisha takriban makundi 20 limemkabidhi Rajoelina orodha ya matakwa ikiwemo kuomba msamaha hadharani kwa matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji, lakini haijataja tena wito wa awali wa kumtaka ajiuzulu.
Matakwa mengine ni pamoja na mageuzi ya Mahakama ya Katiba na kuvunjwa kwa Seneti au angalau kuondolewa kwa rais wake, Richard Ravalomanana, ambaye ni jenerali wa zamani wa polisi.
Kisiwa kikubwa chenye watu wapatao milioni 32 ni kinara wa uzalishaji wa vanila na kina rasilimali nyingi za asili, lakini takriban robo tatu ya wakazi wake waliishi chini ya mstari wa umaskini mwaka 2022, kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia.
Maandamano makubwa zaidi
Madagascar, mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani, imekuwa ikishuhudia vuguvugu la wananchi mara kwa mara tangu kupata uhuru mwaka 1960, ikiwemo maandamano makubwa mwaka 2009 yaliyomsababisha rais wa wakati huo, Marc Ravalomanana, kuondolewa madarakani na jeshi kumweka Rajoelina kwa muhula wake wa kwanza.
Rajoelina alishinda tena uchaguzi mwaka 2018 na 2023 katika uchaguzi uliokuwa na utata.
Kundi la kufuatilia migogoro la ACLED limesema mwezi wa Septemba ulikuwa na kiwango cha pili cha juu cha maandamano nchini Madagascar tangu lilipoanza kukusanya takwimu mwaka 1997.