Kutiwa saini kwa makubaliano hayo katika hatua ya kwanza ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu Gaza kunatarajiwa kufanyika saa 0900 GMT sawa na saa sita asubuhi kwa majira ya saa za Afrika Mashariki, chanzo kilichoarifiwa kuhusu maelezo ya makubaliano hayo kiliiambia shirika la habari la Reuters siku ya Alhamisi.

Usitishwaji wa mapigano unatarajiwa kuanza kutekelezwa katika eneo la Gaza mara tu mkataba huo utakapotiwa saini, chanzo hicho kiliongeza.

Qatar, Misri, Marekani, na Uturuki zimetia saini kama wadhamini wa mkataba wa amani wa Gaza, The Jerusalem Post iliripoti.

Israel na kundi la muqawama wa Palestina Hamas wamesema wameafiki makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosubiriwa kwa muda mrefu, awamu ya kwanza ya mpango wa Trump wa kumaliza vita vya Tel Aviv huko Gaza ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya Wapalestina 67,000 na kugeuza eneo la Mashariki ya Kati.

Hata hivyo baada ya tangazo kwamba Israel na Hamas wamekubaliana mpango wa kusitisha mapigano, wakala wa Ulinzi wa Raia wa Gaza uliripoti mashambulizi kadhaa katika eneo hilo.

“Tangu kutangazwa jana usiku kwa makubaliano kuhusu mapendekezo ya mfumo wa kusitisha mapigano huko Gaza, milipuko kadhaa imeripotiwa, haswa katika maeneo ya kaskazini mwa Gaza,” alisema mmoja wa maafisa wa shirika hilo, Mohammed Al-Mughayyir, akitaja “msururu wa mashambulizi makali ya anga” katika mji wa Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *