Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 62, alitoa wito huo alipohutubia jukwaani baada ya Kagame katika Mkutano wa Global Gateway Forum, ambao ni kongamano la uwekezaji lililoandaliwa na Umoja wa Ulaya katika mji mkuu wa Ubelgiji.

“Ninaomba jukwaa hili kuwa shahidi, na kupitia hapa naiomba dunia nzima kushuhudia, ninaponyoosha mkono wangu kwako, Mheshimiwa Rais, ili tuweze kufanya amani. Hii inahitaji uagize wapiganaji wa M23 wanaoungwa mkono na nchi yako waache mara moja mashambulizi haya ambayo tayari yamesababisha vifo vingi. Tuchukue ujasiri wa kuangaliana macho kwa macho, kusema kilicho kibaya na kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya watu wetu.”

Hata hivyo Kagame hakuzungumzia moja kwa moja mgogoro huo katika hotuba yake. Lakini alirejelea kwa kifupi kauli ya awali ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, aliyesema alihisi “nguvu ya kutaka amani” alipowaona viongozi wa Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja.

“Afrika inapaswa kusonga mbele”

Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa DRC Felix Tshisekedi
Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema Afrika inapaswa kusonga mbele, ina uwezo wa kufanya hivyoPicha: Simon Wohlfahrt/AFP

Eneo la Kongo Mashariki, linalopakana na Rwanda na lenye rasilimali nyingi, limekumbwa na machafuko makubwa kwa zaidi ya miongo mitatu kutokana na makundi ya waasi.

Kundi la waasi la M23, ambalo lilianza tena mapigano mwishoni mwa mwaka 2021, limechukua maeneo makubwa kwa msaada wa Rwanda, na kusababisha janga kubwa la kibinadamu.

Mapema mwaka huu, machafuko mapya yalizuka ambapo M23 waliteka miji muhimu ya Goma na Bukavu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mapigano tangu Januari yamesababisha maelfu ya vifo na kulazimisha mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao.

Serikali ya Kongo na waasi wa M23 walitia saini tamko la msingi mnamo Julai 19 huko Qatar, likiwa na azimio la “kusitisha mapigano kabisa”. Tamko hilo lilifuatia makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani kati ya serikali za Congo na Rwanda yaliyotiwa saini Washington mwezi Juni.

Hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa wa polepole, huku waasi wa M23 wakizidi kuimarisha udhibiti wa kisiasa na kiuchumi katika maeneo wanayoyashikilia.

“Afrika inapaswa kusonga mbele, alisema Rais Paul Kagame, na tuna uwezo wa kufanya hivyo,” alisema Tshisekedi, akiongeza kuwa ataahirisha wito wa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Rwanda ili kutoa nafasi kwa mazungumzo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *