Hii ni kufuatia hatua ya Marekani kupunguza ufadhili wake kwa taasisi hiyo ya kimataifa. Afisa mwandamizi wa Umoja Mataifa aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina kutokana na mazungumzo ya faragha, aliwafahamisha waandishi wa habari kuhusu mpango wa kupunguzwa kwa 25% idadi ya walinda amani duniani, huku Marekani — mfadhili mkubwa zaidi wa Umoja wa Mataifa ikifanya mabadiliko yanayolingana na sera ya Rais Donald Trump ya “Amerika Kwanza.”

Takriban wanajeshi na maafisa wa polisi 13,000 hadi 14,000 kati ya zaidi ya walinda amani 50,000 walioko katika misheni tisa duniani watarudishwa makwao. Ofisi ya msaada ya Umoja wa Mataifa nchini Somalia pia itaathirika. Umoja huo unapanga kupunguza takriban 15% ya bajeti ya dola bilioni 5.4 ya vikosi vya kulinda amani kwa mwaka ujao.

Misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zipo katika nchi mbalimbali zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Lebanon, Cyprus, na Kosovo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema kuwa bajeti ya kulinda amani ni sehemu ndogo sana ya matumizi ya kijeshi duniani, ikiwa ni takriban nusu ya asilimia moja pekee. Aidha, amesisitiza kuwa operesheni za kulinda amani ni mojawapo ya njia bora na za gharama nafuu za kuimarisha amani na usalama wa kimataifa.

Marekani yaapa kutotoa mchango zaidi

DR Kongo Goma 2025 | Kikosi cha kulinda amani cha MONUSCO
Umoja wa mataifa itapunguza 25% ya kikosi cha kulinda amani duniani.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Mabadiliko haya makubwa yanajiri baada ya mkutano kati ya Katibu Mkuu Guterres na wawakilishi wa nchi wafadhili wakuu, ikiwa ni pamoja na Mike Waltz, balozi mpya wa Marekani katika Umoja wa Mataifa. Waltz na maafisa wengine wa utawala wa Trump wamesema kuwa bajeti na mashirika ya Umoja wa Mataifa yamejaa uzito na hayana faida, hivyo wameapa kutotoa mchango zaidi hadi Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani itakapokamilisha tathmini ya ufanisi wa kila shirika au programu zake.

Historia inaonyesha kuwa operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zimeongezeka kwa kiasi kikubwa. Mwishoni mwa Vita Baridi, miaka ya 1990, walinda amani walikuwa 11,000 tu, lakini kufikia 2014 walifikia 130,000 katika operesheni 16. Hivi sasa, takriban walinda amani 52,000 wanahudumu katika maeneo 11 yenye migogoro barani Afrika, Asia, Ulaya, na Mashariki ya Kati.

Marekani imetangaza kuwa itatoa dola milioni 680 kwa misheni tisa inazofadhili, punguzo kubwa kutoka dola bilioni 1 ilizotoa mwaka uliopita. Fedha hizo zitalenga misheni zote zinazoendelea, hasa zile ambazo Marekani ina maslahi maalum, kama vile walinda amani nchini Lebanon na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa afisa mwingine wa Umoja wa Mataifa aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mchango wa Marekani na China unachangia nusu ya bajeti ya kulinda amani, na China imeonyesha nia ya kuendelea kutoa mchango wake kamili kabla ya kumalizika kwa mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *