Laila Rajab Khamis

Chanzo cha picha, Laila

    • Author, Na Rehema Mema, Zanzibar
    • Nafasi,

Katika historia ndefu ya siasa za Zanzibar, jina la Laila Rajab Khamis sasa limeandikwa kwa herufi kubwa si kwa sababu ya nafasi aliyopewa, bali kwa nafasi aliyoamua kuichukua mwenyewe. Mwaka 2025, Laila amekuwa mgombea pekee wa urais mwanamke visiwani Zanzibar, na wa kwanza katika historia yote ya uchaguzi wa visiwa hivyo. Hatua yake imevunja ukimya wa miaka mingi ulioweka uongozi wa juu mikononi mwa wanaume.

“Kwanza nilijisikia furaha,” anasema Laila kwa sauti tulivu lakini yenye uthabiti. “Tulianza mchakato wanawake watatu, bahati mbaya wenzangu hawakuingia. Hilo niliniuma, lakini pia nilipothibitishwa (na Tume), nikasema hapa mwanamke niko peke yangu, sitaki kuwaangusha wanawake wenzangu. Nitapambana kwa juhudi zangu zote angalau nami nitokee mshindi wa pili.”

Kuwaza kupata nafasi ya pili, inakupa picha namna siasa za Zanzibar zilivyo ngumu kwa mwanamke ‘kufurukuka’, lakini uwepo wake kwenye uchaguzi wa mwaka huu, tayari kumebadilisha historia.

Laila ni mgombea wa chama cha NCCR-Mageuzi, moja kati ya vyama 11 vilivyosimamisha wagombea wa urais Zanzibar mwaka huu. Ni mwanamke pekee katika orodha hiyo, hatua inayomfanya kuwa ishara ya matumaini mapya kwa wanawake wa Visiwani humo.

Mwanamke katika dunia ya siasa ‘dume’

Laila

Chanzo cha picha, Laila

Kwa muda mrefu, siasa za Zanzibar zimekuwa zikichukuliwa kama uwanja wa wanaume hasa kwa nafasi ya Urais. Mfumo wa kisiasa na utamaduni wa visiwa hivyo umekuwa ukilenga zaidi wanaume katika nafasi za juu za uongozi. Mwanamke kuonekana kwenye karatasi ya kura ya urais ilikuwa kama jambo lisilowezekana.

“Mfumo na siasa za Zanzibar ni dume,” anasema Amir Issa, mwananachi na mfuatiliaji wa siasa za visiwa hivyo. “Kutokana na mila na utamaduni wake wa miaka mingi, nafasi ya juu kushikwa na mwanamke haikutazamwa sawa kwa muda mrefu.”

Lakini Laila anasema Rais wa sasa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekuwa msukumo wake mkubwa. Samia, mzaliwa wa Zanzibar na rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania, amekuwa mfano wa kile kinachowezekana pale mwanamke anapopewa nafasi, kwa mujibu wa Laila.

“Kwanza niliwaza, mama Samia ni mwanamke. Kwanini na sisi hapa Unguja tusiingie? Tukakomboe wanawake wenzetu? Yale ambayo hayajayafanya kama mwanamke, na mimi ninaweza kuyaendeleza yale aliyoyasahau,” anasema Laila.

Kutoka Kengeja kijijini hadi Urais

Zbar

Chanzo cha picha, Laila

Laila alizaliwa katika kijiji cha Kengeja, Pemba mwaka 1969. Akiwa mtoto wa tatu kati ya watoto kumi, alisoma hadi darasa la 11 kabla ya kuolewa.

“Nilipomaliza darasa la 11 sikuendelea, nikaolewa. Nilivyoolewa nilikaa mpaka mwaka 2007 nilivyoanza harakati za siasa,” anasema.

Mwaka huo huo, alijiunga na chama cha NCCR-Mageuzi, na kuanza kujijenga hatua kwa hatua. Mwaka 2015, alichaguliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama, nafasi aliyoendeleza hadi mwaka 2020, na baadaye kuwa mjumbe wa Kamati Kuu na Bodi ya Wadhamini ya chama.

Mnamo 2024, aligombea na kushinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kwa Zanzibar, kabla ya kuchukua hatua ya kihistoria ya kugombea urais

Changamoto za kifedha na kimfumo

Kama mwanasiasa wa upinzani, Laila anakiri kushindana na chama tawala, CCM, si rahisi.

“Changamoto kubwa kwa sie wanasiasa tunaogombea kwakweli. Hatuwezi kushindana na CCM,” anasema kwa uhalisia. “Changamoto yetu ni fedha. Kama vyama vingine havina ruzuku, huwezi kushindana nayo kweli. Watu wanataka fulana we huna, wanataka hiki we huna, pale ndipo wanapotuweza peke yake. Lakini hivyo hivyo tunaenda, na Mungu atatusaidia.”

Licha ya changamoto hizo, anasisitiza kuwa nguvu ya chama na imani ya wanachama wake ndizo zimempa uthabiti.

“Nimepambana na chama, chama kimenisaidia kwa hali na mali. Hatulali usiku na mchana,” anasema kwa tabasamu dogo lenye uzito wa matumaini.

Si Zanzibar hata Tanzania kwa ujumla uchaguzi wa mwaka huu umeshuhudia ongezeko la wagombea wanawake watatu akiwemo Rais Samia wa CCM, Mwajuma Noty Mirambo wa UMD na Saum Hussein Rashid wa UDP. Ni ishara kwamba siasa za Tanzania nzima zinapitia kipindi cha mabadiliko ya kihistoria.

“Upinzani mkali ni kawaida,” anasema. “Kila mtu yeye anataka awe yeye.”

Laila anaamini kwamba uwepo wake kwenye kinyang’anyiro cha urais si kwa ajili ya ushindani pekee, bali kuamsha imani kwamba mwanamke pia anaweza.

Ndoto yake ni kuona Zanzibar yenye usawa zaidi, yenye fursa sawa kwa wanawake, vijana na watoto.

Safari ya Laila inaakisi mapambano ya wanawake duniani kote wanaojaribu kupenya kwenye mifumo dume ya kisiasa. Kutoka kwa Ellen Johnson Sirleaf, rais wa kwanza mwanamke Afrika (Liberia), hadi Michelle Bachelet wa Chile na Sahle-Work Zewde wa Ethiopia, kila mmoja ameacha alama ya mabadiliko katika jamii zao.

Zanzibar sasa inaingia katika hatua kama hiyo. Hata kama hatashinda, hatua ya Laila kugombea ni historia ya kipekee kwa kisiwa hicho. Ni alama kwamba kizazi kipya cha wanawake wa Visiwani kinaweza kuota zaidi ya mipaka ya kijinsia.

,
.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *