
Chanzo cha picha, Reuters
Inatokea tena.
Mapema mwezi Septemba, mlolongo wa vifo visivyoeleweka vya watoto katika mji mdogo wa Madhya Pradesh uliwafanya wahudumu wa afya kuingiwa na taharuki.
Angalau watoto 11 wenye umri kati ya mwaka mmoja na sita walifariki ndani ya siku chache baada ya kutumia dawa ya kawaida ya kikohozi.
Maafisa wa afya walichunguza kila kitu, kuanzia maji ya kunywa hadi mbu, kabla ya ukweli kufichuka: figo zao zilishindwa kufanya kazi.
Wiki chache baadaye, maabara ya serikali jijini Chennai (kusini mwa India) ilithibitisha hofu kuu.
Dawa hiyo ya kikohozi ilibainika kuwa na asilimia 48.6 ya diethylene glycol ambayo ni kemikali hatari ya viwandani isiyopaswa kuwepo kwenye dawa yoyote.
Kunywa kemikali hii mara nyingi husababisha kushindwa kwa figo.
Lakini janga hili halikuishia Madhya Pradesh.
Katika jimbo jirani la Rajasthan, watoto wawili wadogo walifariki dunia baada ya kutumia dawa ya kikohozi aina ya Dextromethorphan iliyotengenezwa kienyeji na ni dawa ambayo si salama kwa watoto wadogo.
Tukio hilo liliibua hasira kubwa na kuchochea uchunguzi wa serikali.
Kwa India, haya hayakuwa mambo mapya ni hali iliyojirudia mara nyingi.
Kwa miaka mingi, dawa za kikohozi zinazotengenezwa nchini humo zenye diethylene glycol zimekuwa zikiripotiwa kuua watoto.
Mnamo mwaka 2023, dawa hizo zilitajwa kuhusika katika vifo vya watoto 70 nchini Gambia na wengine 18 nchini Uzbekistan.
Kati ya Desemba 2019 na Januari 2020, angalau watoto 12 wenye umri wa chini ya miaka mitano walifariki katika eneo la Jammu, Kashmir inayoongozwa na India wakihusishwa na matumizi ya dawa ya kikohozi.
Wanaharakati walionya kuwa idadi ya vifo huenda ilikuwa juu zaidi.
Pia, dawa za kikohozi zenye codeine ni dawa ya kulevya inayoweza kuleta hali ya ulevyaji wa mara kwa mara ziliwahi kutumika vibaya, licha ya kuwa si salama kwa watoto.
Kila mara mamlaka za usimamizi huahidi kufanya maboresho, lakini dawa zenye sumu hurudi tena sokoni.
Hali hii inaonesha udhaifu wa soko la dawa linalotawaliwa na wazalishaji wadogo, bei nafuu, na ukosefu wa usimamizi madhubuti.
Muda mfupi baada ya vifo hivyo, Wizara ya Afya ya India ilitoa wito wa matumizi “ya busara” ya dawa za kikohozi ikiwataka madaktari kuwa waangalifu zaidi wanapozitoa kwa watoto.
Serikali ilikamata sampuli za dawa, ikasimamisha mauzo, na kuanzisha uchunguzi.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Hata hivyo, wataalamu wanasema tatizo si matumizi kupita kiasi pekee, bali ni mfumo mzima wa udhibiti wa dawa wenye mianya mingi.
Soko la dawa za kikohozi nchini India linatarajiwa kukua kutoka dola milioni 262.5 mwaka 2024 hadi dola milioni 743 kufikia 2035 likikua kwa asilimia 9.9 kwa mwaka, kwa mujibu wa ripoti ya Market Research Future.
Lakini yote haya yasingekuwepo iwapo India na raia wake wangekuwa tayari kuachana na uraibu wao wa muda mrefu wa dawa za kikohozi.
Kwa miongo kadhaa, madaktari wamekuwa wakiandika dawa hizi kiholela, na wagonjwa wamekuwa wakizitumia ingawa nyingi hazina msaada wa maana na zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya.
Zinapotangazwa kama suluhisho la haraka kwa koo zinazouma na kikohozi kisichopona, dawa hizi huwa ni mchanganyiko wa sukari, rangi, ladha na viambato mbalimbali kama antihistamini, dawa za kupunguza msongamano wa hewa, na dawa inayotumika kwa kikohozi kioevu.
Kitaalamu, kila kiungo kina jukumu lake: kimoja hukausha kamasi, kingine hulegeza makohozi, na kingine hupunguza msisimko wa kikohozi. Lakini kwa uhalisia, ushahidi wa manufaa yake ni mdogo. Mara nyingi, kikohozi hupungua chenyewe baada ya siku chache.
Kwa nini dawa za kikohozi zinaibua hofu kuhusu usalama?
Kikohozi kinaweza kuwa matokeo ya maambukizi au mzio.
Kwa kawaida, dawa za kikohozi hugawanyika katika makundi mawili: zile zinazosaidia mtoto kupumzika (sedatives), na zile zinazofungua njia za hewa (bronchodilators). Madaktari huagiza mojawapo, si mchanganyiko.
Kwa mujibu wa Dkt. Rajaram D. Khare, daktari wa watoto kutoka Mumbai, kikohozi cha mara kwa mara kwa watoto katika miji ya India mara nyingi husababishwa na mzio na muwasho wa njia za hewa za chini si maambukizi.
Hii ni kwa sababu mfumo wa kinga hujibu kupita kiasi kwa vichochezi kama vumbi na uchafuzi wa hewa.
Watoto huwa na mafua, kikohozi, pua inayotiririka makamasi, na dalili huzidi usiku au asubuhi.
Dalili hizi hujirudia kila baada ya wiki chache.
Kulingana na Dkt. Khare, hali hii mara nyingi huambatana na bronchospasm (kukakamaa kwa mirija ya hewa), na huitikia vizuri zaidi dawa za kuvuta hewani kama inhalers au nebulizers, ingawa madaktari wengi bado hutegemea na dawa ambazo hazitoi nafuu kubwa.
Kawaida, kikohozi cha watoto hutokana na virusi, na hupotea chenyewe ndani ya wiki moja.
Hakuna dawa inayofupisha muda wa kikohozi.
Kwa hali bora, huweza kumpa mtoto faraja ya muda; kwa hali mbaya, zinaweza kuleta madhara kama utegemezi, sumu, au dozi kupita kiasi.
“Mimi sipendekezi dawa za kikohozi kwa mafua ya kawaida au kikohozi. Labda mara chache, kwa lengo la kumpunguzia mtoto maumivu usiku, lakini si kwa matibabu ya msingi. Lengo kuu huwa ni kumpa nafuu ya muda mfupi, si tiba,” anasema Dkt. Khare.

Chanzo cha picha, NurPhoto via Getty Images
Sababu ya matumizi makubwa ya dawa hizi ni nini?
Moja ya sababu kuu ni udhaifu wa mfumo wa afya ya msingi, hasa vijijini na miji midogo.
Uchafuzi wa hewa unavyozidi kuongezeka, kikohozi kinachotokana na mzio kinachanganyikiwa na maambukizi ya kawaida ya kupumua.
Tatizo ni kubwa zaidi vijijini. Katika maeneo mengi ya vijijini India, hadi asilimia 75 ya huduma za afya hutolewa na wahudumu wasio na mafunzo rasmi maarufu kama RMPs (wahudumu wa afya wa mashinani).
Mahali ambapo kliniki za serikali ziko mbali, hazifanyi kazi au hazina wahudumu, RMPs huwa ndio madaktari wa eneo.
Na dawa za kikohozi ni silaha yao ya kawaida.
Dkt. Kafeel Khan, daktari wa watoto aliyewahi kufanya kazi Gorakhpur, anakumbuka:
“dawa za kikohozi zilikuwa zikitolewa kila mahali hata na watu wasio na ujuzi wowote wa kitaalamu.”
Katika miji mingi midogo, wagonjwa hutegemea yeyote anayeonekana kuwa na maarifa ya tiba iwe ni tabibu wa kienyeji au wauzaji wa maduka ya dawa hata kwa kikohozi cha kawaida.
“Wagonjwa wengi maskini huelekea kwa wauzaji wa dawa, wakidhani mtu aliyeko dukani ni mfamasia. Lakini mara 10 kati ya 10 vijijini India, hiyo si kweli,” anasema Dinesh Thakur, aliyekuwa mtendaji wa kampuni ya dawa na sasa mtaalamu wa afya ya umma.
“Ingawa inaaminika kuwa tatizo hili ni la vijijini, kuna ushahidi kuwa linaenea hadi mijini. Tofauti ni kuwa ubora wa dawa vijijini ni mbovu zaidi.”
Sababu nyingine ni shinikizo kutoka kwa wazazi na mapungufu ya kitaaluma miongoni mwa madaktari.
“Wazazi wengi hawana uelewa wa kutosha. Wao huingiwa na wasiwasi, na kama kikohozi au mafua ya mtoto haviponi haraka, huenda kwa daktari mwingine atakayempa dawa ya kikohozi,” anasema Dkt. Khan.
Maarifa hafifu ya kitabibu huzidisha tatizo hilo. Dkt. Khan anasema ameona hata madaktari waliobobea katika magonjwa ya watoto (madaktari wa watoto wenye shahada ya udaktari wa uzamili) wakiwapendekezea watoto dawa za kikohozi zisizo salama.
“Nimewaona madaktari wa kiwango cha MD wakiwaandikia watoto dawa aina ya ambroxol. Dawa hii imelenga kuvunjavunja kamasi, lakini watoto walio chini ya miaka miwili hawawezi kuitema, hivyo ute huo unaweza kuingia kwenye mapafu na kusababisha nimonia. Hata hivyo, bado inatumiwa sana,” anaeleza.
India inahitaji sera wazi kuhusu matumizi ya dawa za kikohozi, pamoja na kampeni ya kitaifa ya kuelimisha madaktari na wazazi kuhusu matumizi sahihi na salama ya dawa hizi.
Hii si hoja ya kinadharia pekee madhara ya uhalisia ni makubwa.
Daktari aliyewandikia watoto dawa ya kikohozi iliyohusishwa na vifo katika Madhya Pradesh alijitetea kwa kusema:
“Nimekuwa nikipendekeza dawa hii ya kikohozi kwa zaidi ya miaka 15.”
Sio India pekee..
Mwaka jana mwezi Aprili mamlaka nchini Kenya ilichukua hatua kudhibitimadhara yatokanayo na daa za kikohozi miongoni mwa watoto.
Bodi ya ya Dawa na Sumu nchini Kenya (PPB), ilipiga marufuku dawa ya kikohozi ya Benylin kwa watoto sokoni, ikitaja wasiwasi wa usalama wake.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi, Aprili 11, bodi hiyo ilibainisha kuwa bidhaa hiyo, nambari 329,304, iliyotengenezwa na kampuni ya Johnson & Johnson ya Afrika Kusini, ilikuwa na kiwango cha juu kisichokubalika cha diethylene glycol, ambacho kiligunduliwa katika uchambuzi wa maabara.
PPB ilisema imeanza uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kuchukua sampuli za syrups za watoto za Benylin za 100ml ili kubaini kama zilikuwa zimeambukizwa.
Ilivishauri vituo vya afya kuacha kusambaza bidhaa hiyo na kuwataka wananchi walionunua kuzirejesha katika kituo cha huduma za afya kilicho karibu nao.