
Chanzo cha picha, Getty Images
-
- Author, Simon Stone
- Nafasi, Chief football news reporter
Vyanzo vya Manchester United vimekanusha madai yaliyotolewa na kiongozi mkuu wa michezo wa Saudi Arabia, Turki Alalshikh, kwamba klabu hiyo iko kwenye hatua za mwisho za mazungumzo ya kuuzwa kwa mwekezaji mpya.
Siku ya Jumatano, Alalshikh, mwenye wafuasi milioni 7.1 katika mtandao wa X aliandika, ”Habari njema nilizosikia leo ni kwamba Manchester United wako kwenye hatua za mwisho kukamilisha mkataba wa kuiuza klabu hiyo kwa mwekezaji mpya.Natumai atakuwa bora kuliko hao waliopita.”
Sasa vyanzo kadhaa vilivyopo karibu na United vinakanusha madai haya, kuwa si kweli.
Alalshikh amebainisha katika ujumbe wa pili wa X siku ya Alhamisi akisisitiza kuwa yeye si mwekezaji mpya na pia amesema huyo mwekezaji hatoki Saudia Arabia.
Jumatano, Turki Alalshikh, ambaye ana wafuasi milioni 7.2 kwenye mtandao wa kijamii X, aliandika: Lakini hapa kuna maswali bila majibu.
Mpango rafiki
Na ingawa haijathibitishwa wazi ikiwa Manchester United wanapanga kucheza dhidi ya klabu ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia (Saudi Pro League) au timu kubwa ya Ulaya yenye hadhi sawa kama AC Milan, kocha mkuu Rúben Amorim alisema wiki iliyopita:
“Tunalazimika kufanya hivyo. Tulijua kwamba baada ya kukosa kushiriki mashindano ya Ulaya, tunahitaji kufidia mambo mengi — ikiwa ni pamoja na mashabiki wetu na bajeti ya klabu. Hivyo basi, tunajaribu kuyaweka mambo yote pamoja ili kufanikisha hilo.”
Siku ya Jumapili Alalshikh alitangaza mpango mpya wa msimu wa Riyadh, lakini haujumuisha chochote kuhusu kandanda, ila alidokeza kuwa kuna mchezo utaongezwa, kwa sasa thamani ya ratiba ya shughuli za michezo anayoandaa imefikia thamani ya dola 3.2bn (£2.39bn).
Familia ya Glazer na Saudi Arabia
Hakujakuwepo kwa makubaliano yoyote yanayoendelea kwa sasa, kuna historia kati ya familia ya Glazer na Saudi Arabia.
Mwaka 2017, Manchester United ilikubaliana na Mamlaka ya Michezo ya Saudi Arabia (GSA) kusaini Makubaliano ya maelewano. Wakati mkataba huo ulipotangazwa, Manchester United ilisema kuwa lengo lilikuwa kusaidia GSA kuendeleza sekta ya soka nchini humo, kama sehemu ya Dira ya 2030 ya taifa hilo, ambayo inalenga kupanua uchumi wake. Klabu hiyo iliahidi kutoa ujuzi wake wa kibiashara na kimichezo kwa vilabu, mamlaka za michezo, na watu binafsi nchini Saudi Arabia.
Mwaka 2008, Manchester United ilisaini mkataba wa udhamini wa miaka mitano na kampuni ya Saudi Telecom, ambao uliongezwa kwa miaka mingine mitano mwaka 2013.
Mikataba hii ilisababisha uvumi kuhusu uwezekano wa familia ya Glazer kuuza klabu hiyo kwa wawekezaji kutoka Saudi Arabia, lakini vyanzo vya ndani vya Manchester United vilikanusha mara kwa mara uvumi huo, na hakuna makubaliano yoyote yaliyowahi kufikiwa
Je, hili linaweza kutokea?

Chanzo cha picha, Getty Images
Huku chapisho la pili la Alalshikh kwenye mtandao wa X likionyesha kuwa hakuna jitihada yoyote ya sasa ya Saudi Arabia kununua Manchester United, bado haijawa wazi iwapo ununuzi kama huo ungeweza kupitishwa na Wamiliki na Wakurugenzi wa Ligi Kuu ya England (Premier League).
Jaribio la Sheikh Jassim la kununua klabu hiyo halikufikia hatua ya kutolewa uamuzi rasmi na ligi. Hata hivyo, kwa kuwa hakukuwa na mmiliki mwingine kutoka Qatar katika Ligi Kuu, ununuzi huo usingekataliwa kwa misingi ya mgongano wa maslahi.
Hali ni tofauti kwa upande wa Saudi Arabia. Mfuko wa Uwekezaji wa Umma wa Saudi Arabia (PIF) umeisimamia Newcastle United tangu mwaka 2021. Zaidi ya hapo, PIF pia unasimamia vilabu vinne vya Ligi Kuu ya Saudi Arabia: Al-Nassr, Al-Hilal, Al-Ittihad, na Al-Ahli.
Kutokana na hali hiyo, inaonekana haiwezekani (au angalau haiaminiki kwa sasa) kuwa Ligi Kuu ya England itakubali umiliki wa vilabu viwili tofauti kutoka kwa chanzo kimoja kikuu cha fedha (PIF), hata kama watu wanaohusishwa na usimamizi wa vilabu hivyo ni tofauti.
Uhusiano thabiti
Katika mahojiano ya podcast na The Times,mmiliki wa Manchester United wa sasa Ratcliffe alielezea jinsi utaratibu wa klabu hiyo ulivyo.
Yeye anamiliki asilimia 30 ya klabu hiyo baada ya kununua hisa hizo mwaka jana, ingawaje wanahusika pia, lakini familia ya Glazer sasa hawana ushawishi wa kufanya maamuzi makubwa zaidi ya Ratcliff.
Kama mfano alipoulizwa kuhusu iwapo Glazers wamemuambia amfute kazi Amorim, Ratcliff alijibu hawawezi kuniambia hivo,tuna uhusiano mwema”
Uwekezaji wa Ratcliffe unajumuisha kipengee cha kisheria kilichoanza kutumika Agosti 2025, kinachoelezea kuwa mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 72 atalazimika kuuza hisa zake iwapo familia ya Glazer itakubali ofa inayozidi dola $33 kwa kila hisa , bei ambayo Ratcliffe alinunulia hisa zake za klabu.
Ratcliffe alizungumzia kifungu hicho wakati wa mkutano na waandishi wa habari mwaka 2024, akisema:”Sidhani kama tutakuwa tunatoa mikataba ya kisheria kutoka kwenye droo ya chini.”
Katika taarifa za kifedha za karibuni zilizotolewa mwezi uliopita, imeelezwa kuwa kuna vikwazo vya ziada vilivyowekwa hadi Februari 2027, vikiwemo:
- Kununua klabu nyingine
- Kulipa gawio kati ya pande hizo mbili
Hata hivyo, moja ya isipokuwa tatu zilizoorodheshwa ni pale ambapo masharti hayo yanahusiana na mabadiliko ya umiliki wa klabu.
Pamoja na hayo yote, maneno ya Ratcliffe hayaonyeshi kuwepo kwa matatizo katika uhusiano wake na familia ya Glazer, ya kiwango ambacho wangeweza kuendelea na mazungumzo ya kuuza klabu bila kumshirikisha. Kinyume chake, maneno yake yanaashiria uhusiano mzuri.
Yote haya yanaturudisha kwenye chapisho la mwanzo la Alalshikh na makanusho yaliyofuata. Huenda tukalazimika kusubiri kwa muda mrefu kupata majibu ya uhakika.
Imetafsiriwa na Ahmed Bahajj na kuhaririwa na Ambia Hirsi