
Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
-
- Author, Paul Njie
- Nafasi, BBC Africa
Kiongozi wa nchi mwenye umri mkubwa zaidi duniani – Paul Biya mwenye umri wa miaka 92 amewaahidi wapiga kura wa Cameroon “maisha bora zaidi bado yanakuja” anaposaka muhula wa nane wa urais siku ya Jumapili hii.
Paul Biya tayari amekuwepo madarakani tangu 1982 ambapo akipata mamlaka kwa miaka saba mingine inaweza kumfanya atawale kwa miaka 50 hadi atakapokuwa akikaribia miaka 100.
Alipuuzilia mbali wito wa kujiuzulu na amekosolewa kwa kujitokeza kwenye mkutano mmoja tu, akitumia muda mwingi wa kampeni kufanya ziara ya faragha ya siku 10 kwenda Ulaya.
Video iliyoandaliwa kwa kutumia teknolojia ya akili mnemba ilizua mvutano nchini Cameroon , hasa wapinzani wake walipokuwa wakiwashawishi wapiga kura Biya alilazimika kuelekea kwake kaskazini mwa nchi.
Katika jiji tajiri la Maroua siku ya Jumanne Biya alihutubia umati wa wafuasi wa chama chake akiwafikia hasa wanawake na vijana, akiahidi kutoa kipaumbele kwa changamoto zao katika kipindi kijacho akichaguliwa.
“Nitatimiza ahadi yangu,” alisisitiza, akiwasihi “niungeni mkono kwa mara nyingine tena”.
Hata hivyo mchambuzi wa masuala ya kisiasa Immanuel Wanah anaiambia BBC kwamba tangu Biya aingie madarakani, kipaumbele chake kikuu kimekuwa ni kuendelea kusalia madarakani, “mara nyingi kwa gharama ya jitihada za kuboresha hali ya maisha ya wananchi.”
Ni maoni yaliyoungwa mkono na Dk Tilarius Atia, mchambuzi mwingine wa kisiasa, ambaye mchambuzi mwingine wa siasa, anayehusianisha hali hiyo na jaribio la mapinduzi lililoshindikana dhidi ya Biya mnamo mwaka 1984.
Hii inamaanisha kwamba kwa raia walio wengi, Biya ndiye rais pekee waliowahi kumjua- zaidi ya 60% ya watu milioni 30 wa Cameroon wako chini ya umri wa miaka 25.
Mwanaharakati wa kisiasa Marie Flore Mboussi anatamani sana “damu changa” kwani anaamini “kukaa muda mrefu madarakani bila shaka hupelekea aina fulani ya uvivu”.
“Baada ya miaka 43, watu wamechoka,” anaiambia BBC.
Uchaguzi wa urais unakuja huku kukiwa na wasiwasi unaoongezeka kuhusu mfumuko wa bei, changamoto za usalama, huduma duni za kijamii, rushwa na ukosefu wa ajira.
Ukosefu wa ajira kwa vijana umekuwa gumzo hasa kwa wagombea wengi wanaoshiriki uchaguzi huu.

Chanzo cha picha, Michel Mvondo/BBC
Takriban asilimia 40 ya vijana wa Cameroon wenye umri wa kati ya miaka 15 na 35 hawana ajira, huku 23% ya vijana wahitimu wakikabiliwa na changamoto za kupata ajira rasmi, kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM).
”Vijana wana mwelekeo zaidi wa kuhamia nje ya nchi kwa sababu wanazotaja kwamba ndani ya nchi hawana nafasi ya kuwa watu wa maana,” anasema Vanina Nzekui, mhitimu mwenye umri wa miaka 26, alipoongea na BBC
“Wanajiambia kuwa nyadhifa zote zinashikiliwa na wazee,” anasema, akiongeza kuwa hii inakuja kwa gharama ya kutumia ujuzi wao kusaidia kuendeleza nchi.
Lakini Aziseh Mbi, 23, anaamini umri haufai kuwa kigezo cha uongozi.
Kuhusu suala la Biya, mwanaharakati wa mashirika ya kiraia anasema, rais ameweza kufanya “mambo muhimu,” akitoa mfano wa mikakati kadhaa iliyowalenga vijana.

Chanzo cha picha, Reuters
Mbali ya ukosefu wa ajira kwa vijana, mchakato wa uchaguzi pia umezua utata, haswa kwa kutengwa kwa Maurice Kamto kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Mnamo Julai baraza la uchaguzi lilimzuia kiongozi huyo wa upinzani mwenye umri wa miaka 71 kugombea kwa sababu kambi ya upinzani ya chama kilichomuidhinisha iliwasilisha mtu mwingine kama mgombea.
Kutengwa kwake, kulikothibitishwa na Baraza la Katiba, kulikosolewa vikali kama njama ya kuzuia changamoto yoyote kali kwa Rais Biya.
Baada ya kushika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa 2018, Kamto alidai ushindi na kuandaa maandamano.
“Kutengwa kwa Prof Kamto kunadhoofisha uhalali wa demokrasia yetu kwa sababu tulipaswa kusimamia haki vya kutosha na kuruhusu kila mtu kushiriki,” asema Dkt Atia.
Bw Wanah anaafiki kwamba kukosekana kwa kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo “kunaimarisha dhana kwamba uchaguzi wa haki hauwezi kufanyika nchini Cameroon”.
Wagombea 12 wameidhinishwa kugombea nafasi ya juu nchini humo, akiwemo Issa Tchiroma Bakary na Bello Bouba Maigari – wote washirika wa zamani wa Biya kutoka kaskazini mwa nchi. Walijiuzulu nyadhifa zao za uwaziri serikalini ili kumkabili kiongozi wao.
Mbunge Cabral Libii, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Social Democratic Front (SDF) Joshua Osih na Patricia Tomaïno Ndam Njoya ambaye ni mgombea pekee wa kike – pia wako kwenye kinyang’anyiro hicho.
Katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi, wagombea wawili, akiwemo wakili mashuhuri wa kupambana na ufisadi Akere Muna, walijiengua katika kinyang’anyiro ili kumuunga mkono Maigari wa chama cha NUDP.
Hii ina maana watu 10 sasa watagombea urais.

Chanzo cha picha, Michel Mvondo / BBC
Kabla ya uchaguzi huo – ambao utakuwa na mzunguko mmoja pekee kwakuwa mgombea atakayeibuka na kura nyingi ndiye atakayeshinda – kumekuwa na sauti nyingi za wito wa upinzani kuwasilisha mgombea mmoja ili kumpinga Biya, ambaye hajawahi kushindwa katika uchaguzi.
Tchiroma Bakary amepata kuungwa mkono na chama cha Union for Change, muungano wa zaidi ya makundi 50 ya kisiasa na mashirika ya kiraia yaliyomtambulisha kama mgombea aliyepitishwa na upinzani.
Lakini mpango huo umeshindwa kupata kauli moja, huku wengine wakikataa kumuunga mkono.
Kamto alisema amefanya mazungumzo na baadhi ya wagombea , wakiwemo watu wawili wkutoka kaskazini Tchiroma Bakary na Maigari, kuwahimiza kuungana.
Kwa vile hakuna aliyeonekana kuwa tayari kuachia ngazi, aliwasihi wananchi wa Cameroon kumpigia kura yeyote wanayemkubali.
Dkt Atia anafikiri kushindwa kuidhinisha mgombeaji mmoja chini ya muungano mmoja kutagharimu upinzani kwenye sanduku la kura.
Katika kampeni, Tchiroma Bakary mwenye umri wa miaka 76, msemaji wa zamani wa serikali, amekuwa akivutia umati mkubwa wa watu – huku baadhi ya wachambuzi wakimtaja kiongozi wa chama cha Cameroon National Salvation Front kama mpinzani mkuu wa Biya.
Siku ya Jumapili, maelfu ya wafuasi walisubiri kwa muda mrefu bila kujali mvua iliyokuwa ikinyesha ili kumuona katika mji huo mkuu wa kiuchumi wa Douala.
Ameahidi kurekebisha mfumo ambao amekuwa sehemu yake kwa miongo miwili.
Licha ya Tchiroma Bakary kuungwa mkono upande wa kaskazini, wachambuzi wanasema huenda Biya akamshinda yeye na wagombea wengine wa upinzani.
“Rais Biya anahitaji tu kiasi kidogo cha kura ili kushinda uchaguzi, na ninamuona akishinda licha ya juhudi zinazofanywa na upinzani,” anasema Dk Atia.

Chanzo cha picha, Michel Mvondo / BBC
Katika mikoa ya Kaskazini-Magharibi na Kusini-Magharibi ya Cameroon inayozungumza Kiingereza, ambapo mzozo wa muda mrefu wa kujitenga unaendelea, kumeshuhudia wengine wakisusia uchaguzi , na kudumaza shughuli za biashara, harakati na elimu.
Wanaotaka kujitenga wametishia kumlenga yeyote atakayepiga kura.
Tangu 2017, wale wanaotaka kuunda serikali huru wamekuwa wakipigana na vikosi vya serikali. Wamekasirishwa na kile wanachokiona kama kutengwa kwa jumuiya ya wachache wanaozungumza lugha ya Kingereza nchini Cameroon na serikali inayoongozwa na wazungumzaji wa Kifaransa.
Mzozo huo hadi sasa umesababisha vifo vya takriban watu 6,000 na kuwalazimisha wengine karibu nusu milioni kuyahama makazi yao, kwa mujibu wa UN.
Kwa mujibu wa mwanaharakati wa mashirika ya kiraia Abine Ayah, uwezekano wa kutengwa kwa sehemu kubwa ya jumuiya inayozungumza Kiingereza inaweza kudhoofisha uhalali wa uchaguzi huu.
Ingawa Biya anasema serikali yake imefanya juhudi kubwa kutatua mzozo huo, wapinzani wake katika kinyang’anyiro cha urais wanaendelea kukosoa namna anavyoshughulikia hali hiyo.
Baada ya uchaguzi wa Jumapili, Baraza la Katiba lina siku 15 kutangaza matokeo.
Waziri wa mambo ya ndani tayari ameonya kuwa hakuna mgombea anayeruhusiwa kutangaza ushindi kabla.
Paul Atanga Nji alitoa maoni hayo usiku wa kuamkia siku ya mwisho ya kampeni.
“Wale ambao watajaribu kujitangazia matokeo ya uchaguzi wa urais au ushindi wowote kwa kukiuka sheria za jamhuri watakuwa wamevuka mstari mwekundu na wanapaswa kuwa tayari kukabiliana na hatua zitazolingana na uhalifu wao.”
Taarifa ya ziada ya mwandishi wa BBC Michel Mvondo huko Yaoundé.
Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Ambia Hirsi