
Watu zaidi ya 60 wameuawa katika kambi ya wakimbizi kwenye mji wa El-Fasher nchini Sudan siku ya Jumamosi, baada ya kushambuliwa na ndege mbili za kijeshi, zisizokuwa na rubani.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Shambulio hilo lililenga kambi ya Dar al-Arqam, iliyowapata hifadhi maelfu ya watu waliokimbia maakazi yao kwa sababu ya vita vinavyoendelea kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF jimboni Darfur.
Watoto, wanawake pamoja na wazee ndio waliouwa katika shambulio hilo ambalo watatezi wa haki za binadamu wanasema ni mauaji ya halaiki katika mji huo, wakati dunia, ikiendelea kusalia kimya.
Mji wa El-Fasher, umekuwa kitovu kipya cha makabiliano kati ya RSF na wanajeshi, katika mauaji ambayo yanadaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa RSF ambao wanalenga kudhibiti jimbo lote la Darfur.
Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Volker Turk, ameshtumu pande zote zinazohusika kwenye vita nchini Sudan kwa kuendelea kuvunja sheria za Kimataifa kwa kuendelea kutekeleza mauaji ya raia wa kawaida.
Tangu Aprili mwaka 2023, jeshi na wanamgambo wa RSF wamekuwa wakikabiliana, katika vita ambavyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu, na kuwaacha mamilioni bila makaazi na wengine zaidi ya Milioni 25 wanakabiliwa na baa la njaa.