
Kutunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kiongozi wa upinzani nchini Venezuela María Corina Machado kumeibua hisia tofauti katika nchi za Amerika Kusini, huku baadhi ya viongozi wa nchi za eneo hilo wakipongeza hatua hiyo na wengine kulaani vikali kwa kuashiria matamshi na vitendo vya Machado vya kuchochea vurugu na machafuko au hata kuunga mkono kufanywa mashambulio na uvamizi wa kigeni dhidi ya nchi yake mwenyewe.
Rais Josu Raúl Mulino wa Panama, Bernardo Arévalo wa Guatemala na Santiago Pena wa Paraguay wamempongeza kiongozi huyo wa upinzani nchini Venezuela kwa kutunukiwa tuzo za amani ya Nobel wakisema, hatua hiyo hii inaashiria kutambuliwa na kuthaminiwa mapambano yake anayoendesha kwa njia ya amani kwa niaba ya watu wanaopigania uhuru wao.
Hata hivyo Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel, yeye ameponda Corina kutunukiwa tuzo ya amani ya Nobel na kukosoa vikali uamuzi wa kamati ya tuzo hiyo.
“Ni aibu kutoa tuzo hii mwaka 2025 kwa mtu ambaye ametoa wito wa kufanyika uingiliaji wa kijeshi dhidi ya nchi yake, ambaye katika miaka ya nyuma alihimiza kufanyika maandamano ya mitaani ambapo watu walichomwa moto wakiwa hai,” ameeleza Diaz-Canel katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Rais wa Cuba ameongezea kwa kusema: “tunakataa kwa nguvu zote ujanja huu wa kisiasa ambao unalenga kuitenga Venezuela na kudhoofisha uongozi wake wa Kibolivari, chini ya uongozi wa Rais wake halali, Nicolás Maduro Moros”.
Rais wa zamani wa Bolivia, Evo Morales naye pia amepinga kiongozi wa upinzani nchini Venezuela kutunukiwa tuzo ya amani ya Nobel akisema: “Kutoa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mtu ambaye ameshajiisha ukandamizaji, uingiliaji kijeshi katika nchi yake mwenyewe, na mapinduzi ya kijeshi sio tu ni kinyume cha maadili lakini pia kunahamasisha utumiaji nguvu kama njia ya kukiuka haki za binadamu, demokrasia na kuendesha maisha ya kiraia kwa njia za amani”.
Akiwa kiongozi wa upinzani, ambaye kwa sasa anaishi mafichoni kufuatia uchaguzi wa 2024 nchini Venezuela, Machado ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuingilia kati nchini humo ili kumuondoa madarakani rais Maduro. Mnamo mwaka 2018, mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel alimwandikia barua waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu, anayetafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa kuhusika na jinai za kivita na mauaji ya kimbari huko Ghaza akimuomba ampatie “utaalamu na ushawishi” wake…/