
Wapiga kura milioni nane wanapiga kura kumchagua rais wao mpya katika uchaguzi wa duru moja. Kulingana na Elecam, chombo kinachosimamia kuandaa uchaguzi, baadhi ya vituo 31,000 vimepangwa kufunguliwa saa 2:00 asubuhi saa za Yaoundé (saa 9:00 saa za Afrika ya Ufaransa). Vitafungwa saa 12:00 jioni (saa 1:00 usiku saa za Ufaransa). Rais aliye madarakani Paul Biya anawania muhula wa nane.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Baada ya miaka 43 ya kuwa madarakani Cameroon, Paul Biya, 92, anatafuta muhula mwingine wa miaka saba ambao unaweza kumfikisha hadi kwnye umri wa miaka 99 akiwa madarakani. Akigombea kwa muhula wa nane, Rais wa Jamhuri anaweza kutegemea uwezo wa uhamasishaji wa chama chake, Cameroon People’s Democratic Movement (CPDM), ambacho kiko kote nchini, anaelezea mwandishi wetu maalum huko Douala, Amélie Tulet.
Kuna wagombea kumi na wawili rasmi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi huu wa urais, lakini wawili wamejiondoa. Wakati wa wiki mbili za kampeni rasmi, rais aliyeko madarakani alifanya mkutano mmoja tu, huko Maroua, Kaskazini ya Mbali, mojawapo ya mikoa mitatu ya kaskazini.
Wapinzani wawili wakuu wa Paul Biya katika uchaguzi huu walikuwa, miezi michache tu iliyopita, wajumbe wa serikali. Hao ni Issa Tchiroma Bakary, wa Cameroon National Salvation Front (FSNC), ambaye alivutia watu wengi kwenye mikutano yake, na Bello Bouba Maïgari, ambaye anaweza kutegemea chama chake, National Union for Democracy and Progress (UNDP).
Pia katika kinyang’anyiro hicho kuna mtu aliyesababisha mshangao mwaka wa 2018: Cabral Libii, kiongozi wa Chama cha Cameroon cha Maridhiano ya Kitaifa (PCRN), ambaye alichukuwa nafasi ya tatu katika uchaguzi uliopita wa rais. Joshua Osih, mrithi wa kiongozi wa upinzani marehemu Ni John Fru Ndi, anapeperusha bendera ya chama cha Social Democratic Front (SDF), huku Patricia Hermine Tomaïno Ndam Njoya, kiongozi wa chama cha Cameroon Democratic Union (UDC) na meya wa Foumban, ndiye mwanamke pekee kwenye uchaguzi huu wa urais.
Maurice Kamto aondolewa kwenye uchaguzi
Katika siri ya sanduku la kupigia kura, wapiga kura pia wataweza kuchagua kati ya Serge Espoir Matomba wa chama cha People United for Social Renewal (PURS), Pierre Kwemo wa chama cha Union of Socialist Movements (UMS), mwanauchumi Jacques Bougha-Hagbe wa chama cha Cameroon National Citizens’ Movement (MCNC), na Samuel Iyodiian wa chama cha the young Democratic Front of the Cameroon.
Hata hivyo, uchaguzi huu wa urais unafanyika bila Maurice Kamto, kwani ugombea wa kiongozi wa upinzani aliyeshika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa 2018 ulibatilishwa.
Kwa CPDM na mgombea wake Paul Biya, lengo la uchaguzi ni kurefusha utawala wao wa takriban miaka hamsini. Kwa kuzingatia hili, chama cha rais kimefanya kazi kwa bidii, katika muda wa wiki mbili za kampeni, kutumia umri wa rais, kumtambulisha kama mtu mwenye uzoefu, dhamana ya utulivu, sharti muhimu kwa azma yoyote ya maendeleo.
Kwa upinzani, hata hivyo, lengo ni kukomesha mamlaka ambayo imedumu kwa muda mrefu sana, kuunda mfumo wake wa utawala na kufungua ukurasa mpya katika historia ya Cameroon. Tatizo pekee: katika uchaguzi wa duru moja, mchakato unaendelea kwa mkanganyiko, baada ya kushindwa kukubaliana kuhusu mgombea wa makubaliano, anaripoti mwandishi wetu wa Yaoundé, Polycarpe Essomba.
Katika muktadha huu, huenda kiwango cha ushiriki kikachukua jukumu muhimu, hasa kutokana na shauku iliyoonekana wakati wa baadhi ya mikutano ya wagombea. Je, upinzani utafaulu kuwavutia watu wengi waliojizuia kupiga kura mnamo mwaka 2018 na kuwashawishi wapiga kura wapya karibu milioni 2 waliojiandikisha? Je, kuhusu mhimili wa Kaskazini-Kusini, ambao kwa kiasi fulani ulimwezesha Paul Biya kuhakikisha maisha yake marefu madarakani, unaweza kustahimili ugombeaji wa watu wawili kutoka Kaskazini, ambao ni Issa Tchiroma Bakary na Bello Bouba Maïgari, washirika wawili wa zamani wa Mkuu wa Nchi ambao wameingia upinzani?
Elecam Imejitayarisha kikamilifu kuhakikisha uchaguzi salama
Mwisho, ni matokeo yapi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi na kijamii ambapo uchaguzi unafanyika? Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya watu milioni 10 kati ya watu milioni 28 wa Cameroon wanaishi chini ya mstari wa umaskini, wakati nchi hiyo pia inakabiliwa na mashambulizi ya makundi yenye uhusiano na Boko Haram Kaskazini ya Mbali, pamoja na mgogoro wa miaka minane katika mikoa miwili ya nchi hiyo inayozungumza Kiingereza.