Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imeonya kwamba Tony Blair hatakaribishwa kuwa na nafasi yoyote ya uendeshaji wa Ghaza kufuatia kuanza kutekelezwa usitishaji vita katika eneo hilo la Palestina.

Akizungumza na televisheni ya Sky News, kiongozi mwandamizi wa Hamas Basem Naim anasema anakaribisha namna Rais wa Marekani Donald Trump alivyojihusisha katika kumaliza vita vya miaka miwili vilivyoanzishwa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza.

Hata hivyo, Naim amesema, waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair hawezi kuwa na nafasi katika uendeshaji wa Ghaza, licha ya Trump kutangaza hapo kabla kwamba anaunga mkono Blair kushirikishwa katika suala hilo.

“Inapokuja kwa Tony Blair, kwa bahati mbaya, sisi Wapalestina, Waarabu na Waislamu, na pengine wengine kote ulimwenguni tuna kumbukumbu mbaya juu yake,” ameeleza afisa huyo wa Hamas.

Amesisitiza kwa kusema: “tungali tunaweza kukumbuka nafasi yake katika mauaji, na kusababisha maelfu au mamilioni ya vifo kwa raia wasio na hatia katika nchi za Afghanistan na Iraq”.

Mwezi uliopita, vyombo mbalimbali vya habari viliripoti kuwa Blair alikuwa katika majadiliano ya kuongoza mamlaka ya mpito katika Ukanda wa Ghaza ikiwa ni sehemu ya mpango unaoungwa mkono na Marekani kwa ajili ya utawala wa eneo hilo baada ya vita.

Kwa mujibu wa vyombo hivyo, mpango huo utaanzisha mamlaka ya mpito huko Ghaza kwa muda wa hadi miaka mitano, bila kujumuisha harakati ya Hamas wala Mamlaka ya Ndani ya Palestina…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *