
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelaani vikali mashambulio ya kijeshi yanayofanywa kila mara na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon na kuendelea kukiuka mamlaka ya utawala na umoja wa ardhi ya nchi hiyo hususan shambulio la jana Jumamosi la ndege zisizo na rubani lililolenga kijiji cha Al-Musayleh.
Shambulio hilo limeteketeza vifaa vinavyotumika katika uondoaji kifusi na ukarabati wa maeneo yaliyoharibiwa katika mashambulio ya huko nyuma yaliyofanywa na utawala huo haramu.
Ismail Baghaei amesema, ukiukaji wa kila mara wa makubaliano ya usitishaji vita unaofanywa na utawala wa Kizayuni na mashambulio ya kijeshi unayofanya dhidi ya umoja wa ardhi na mamlaka ya kujitawala ya Lebanon ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
Baghaei amezikosoa Marekani na Ufaransa ambazo ni wadhamini wa usitishaji vita uliofikiwa kati ya Israel na Harakati ya Hizbullah kwa kushindwa kufanya chochote dhidi ya ukiukaji wa mtawalia wa makubaliano hayo unaofanywa na utawala huo wa kizayuni na akatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali ili kukomesha uvunjaji sheria unaofanywa na utawala huo ghasibu na moto wa vita unaoendelea kuwasha dhidi ya Lebanon na nchi nyingine za eneo.
Vyombo vya habari vya Lebanon vimetangaza kuwa, jeshi la utawala wa kizayuni, jana Jumamosi lilifanya mashambulizi ya anga kwenye sehemu sita za maegesho ya mitambo mikubwa zilizoko kando ya barabara ya Al-Musayleh kusini mwa Lebanon, na kuharibu zaidi ya vifaa 300 vikiwemo vya uchimbaji pamoja na mabuldoza.
Shirika la habari la serikali NNA, likinukuu taarifa ya Wizara ya Afya limesema, raia mmoja wa Syria aliuawa katika shambulio hilo, na mwingine mmoj wa nchi hiyo na sita wa Lebanon, wakiwemo wanawake wawili, wamejeruhiwa.
NNA imeongeza kuwa, uharibifu wa mitambo na vifaa hivyo umesababisha hasara ya mamia ya mamilioni ya dola.
Mbali na vifaa hivyo, majengo na mahema, pamoja na magari mengi yaliyokuwa yameegeshwa katika eneo hilo, pia yaliharibiwa.
Rais wa Lebanon Joseph Aoun amelaani shambulio hilo la anga lililofanywa na utawala wa kizayuni akiliita “kitendo cha wazi cha uchokozi”…/