Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, ili kuiwezesha Serikali kutafuta fedha ndani na nje ya nchi kwa ajili ya maendeleo.
Dkt Samia ametoa ahadi hiyo leo, Jumapili Oktoba 12, 2025 alipozungumza na wananchi wa Mbogwe mkoani Geita, katika mkutano wake wa kampeni za urais.
Amesema Oktoba 29, kila mwananchi aliyejiandikisha ahakikishe anakwenda kupiga kura, huku mabalozi wa mitaa wakipewa jukumu la kuwahamasisha wananchi wao.
“Nasema hivyo kwa sababu tunakwenda kukiheshimisha Chama Cha Mapinduzi, chama hiki kimefanya makubwa kwa nchi yetu, chama hiki kinakwenda kufanya makubwa kwenye nchi yetu,” amesema.
Ameeleza ni muhimu kupiga kura ili kuiwezesha Serikali kutafuta fedha ndani na nje ya nchi, kutekeleza miradi iliyoahidiwa.
Aidha, katika eneo hilo, ameahidi kutekeleza mradi wa Barabara ya Masungwe-Kasosobe yenye urefu wa kilomita 45 kuelekea Makao Mkuu ya Wilaya na kufikisha huduma za kijamii karibu na wananchi.
#StarTvUpdate